Mwanamke ampeleka jela ‘mzungu’


Yusuf Aboud's picture

Na Yusuf Aboud - Imechapwa 15 December 2010

Printer-friendly version
Jamvi la Weledi

ADELINA John Katunzi (32), ameshinda kesi. Ni kesi ya jinai iliyomhusu David Human, mkuu wa ulinzi ndani ya mgodi wa Geita Gold Mines (GGM).

Haikutarajiwa na wengi, lakini ndivyo ilivyotokea ndani ya mahakama kuu mjini Mwanza wiki iliyopita.

Mahakama Kuu imemhukumu Human, kifungo cha miaka miwili jela na kumlipa Adelina shilingi milioni mbili (Sh. 2,000,000).

Ilianza kama mzaha. Adelina alifukuzwa kazi mgodini GGM tarehe 5 Machi 2007. Alikuwa akifanya kazi katika kampuni ya kutoa huduma za chakula mgodini.

Hii ilikuwa siku tatu baada ya Adelina kurudi kazini akitokea hospitali ya Mwananchi, mjini Mwanza ambako alikuwa amelazwa kwa operesheni ya kidoletumbo (Apendiksi).

Barua ya kufukuzwa kazi aliyopewa mama huyo ilisema waajiri wake hawana “imani naye tena.”

Sokomoko lilianzia hapa. Akijua hajajaza fomu za kudai mafao yake kutoka mfuko wa hifadhi ya jamii (NSSF), Adelina alikataa kurudisha kitambulisho cha kazi, ili awe anakitumia kuingia mgodini kufuatilia madai yake.

Kwanza Adelina aliomba fomu za kujaza ili adai mafao yake. Akanyimwa. Akadai mafao yenyewe. Akanyimwa. Akajiridhisha kwamba atakuwa anakwenda mgodini kudai alimradi alikuwa na kitambulisho.

Alipokuwa anataka kutoka getini, akazuiwa kwa madai kuwa arejeshe kitambulisho. Akakataa.

Ndipo mkuu wa ulinzi Human alipowaamuru walinzi watatu wa getini, wote wanaume, wampekue na kumnyang’anya kitambulisho. Walinzi walikataa kwa maelezo kuwa mwanamke sharti apekuliwe na mwanamke.

Mahakama ya wilaya ambako kesi hiyo ilianzia, ilielezwa kuwa baada ya walinzi kukataa kumgusa Adelina, Human alikwenda mwenyewe kumkabili Adelina.

Mama huyo alinukuliwa akisema kuwa Human alimkabili getini, akambana kifuani, akampapasa kwenye matiti na hatimaye kutumbukiza mkono ndani ya chupi yake na kugusa uke wake, kwa madai ya kutafuta kitambulisho.

Hata hivyo, mahakama ya wilaya Geita ilitupilia mbali kesi hiyo kwa maelezo kuwa ushahidi uliotolewa ulikuwa unasigana na maelezo aliyotoa kwa polisi.

Mazingira ya shambulio na hatua za awali za kwenda mahakamani, viliandikwa kwa urefu na mwandishi huyu wa gazeti hili katika uchunguzi wa hali ya wananchi wanaoishi karibu na migodi nchini; mradi ambao unafadhiliwa na Tanzania Media Fund (TMF).

Katika hukumu yake ya tarehe 18 Agosti 2008, ya kesi Na. 147 ya 2007, hakimu Zabron M. Kesase wa mahakama ya wilaya Geita, alisema anayepaswa kulaumiwa ni Adelina mwenyewe na wala si Human.

“Ni shahidi wa kwanza (Adelina) anayepaswa kulaumiwa kwa kusababisha yote haya; angekuwa amerejesha kitambulisho kwa wakubwa zake, yote haya yasingetokea. Hivyo namwona mshitakiwa hana hatia na namwachia huru,” alisema hakimu Kesase wakati akisoma hukumu.

Adelina alikata rufaa kwenye mahakama kuu kanda ya Mwanza. Lakini haikuwa rahisi kwake kukata rufaa, kwani anasema mara nyingi, wakili wa mzungu alikuwa akimwambia kuwa hata akikata rufaa hatashinda.

Kuna madai pia kuwa hata mkuu wa upelelezi wa wilaya Geita alimwambia hana haki ya kukata rufaa.

“Mkuu wa upelelezi wa wilaya aliniambia sina haki ya kukata rufaa, lakini mwanasheria wa serikali, baada ya kusoma hukumu ya hakimu wa wilaya, aliniambia nina haki na kila sababu ya kukata rufaa,” anasimulia Adelina.

Sasa Adelina ni mshindi. Hatimaye Ijumaa ya 10 Desemba 2010, Jaji Aishieli Sumari wa mahakama kuu kanda ya Mwanza, alitoa hukumu ya kesi hiyo Na. 82 ya 2009.

Jaji Sumari alimhukumu mzungu kifungo cha miaka miwili na kumlipa Adelina shilingi milioni mbili kama fidia.

Tarehe 24 Machi, mwaka huu gazeti hili liliandika mkasa mzima wa Adelina na mzungu. Makala ilibeba kichwa kisemacho, Dhahabu, mzungu na chupi ya Adelina.

Makala hiyo haikuwafurahisha mabosi wa GGM akiwemo wakili wa Human, Silwan Mwantembe Gallati.

Gallati alipeleka gazeti mahakamani kama ushahidi wa Adelina kuzungumza na vyombo vya habari. Kilichomuuma zaidi ni kichwa cha makala, Dhahabu, mzungu na chupi ya Adelina.

Kila jambo lina mwisho wake. Yawezekana huu ndio mwisho wa kesi hii kwani wakili wa mshitakiwa hajaeleza iwapo atakata rufaa katika mahakama ya rufaa.

Naye Adelina anasema, “Ninajisikia furaha sana. Nimeamini haki inaweza kutendeka. Nilikatishwa tamaa wakati nikifuatilia kesi hii. Wengi hawakuamini kama ningeweza kumshinda mzungu; lakini Mungu amenisaidia kupata haki yangu.”

Akihojiwa mara baada ya hukumu ya mahakama kuu, Adelina alisema, “Human alikuwa akinikejeli, hata leo (siku ya hukumu) tulipokuwa tunaingia mahakamani, alikuwa akinizomea na kunicheka kwa kejeli. Alikuwa akiniambia siwezi kushinda.”

Pamoja na kesi ya hii ya jinai kumalizika kwa Adelina kupata ushindi, bado kuna kesi nyingine ya madai ambapo Adelina ameshitaki Human na GGM.

Kesi hiyo Na. 52 ya 2007 itaendelea tena 19 Januari 2011 katika mahakama ya mkoa wa Mwanza.

Adelina ameshinda dhuluma na udhalilishaji. Kwa kesi hii, wanawake pia wameshinda. Hata MwanaHALISI, lililong’ang’ania kutoa taarifa bila woga wala aibu, nalo limeshinda.

Hivi sasa Adelina anaishi na mtoto wake Kelvin Christian (11) kwa dada yake, kitongoji cha Ilemela, mjini Mwanza.

“Kesi ndiyo ilikuwa inanisumbua. Sasa niko huru; nimeanza kutafuta kazi,” ameeleza.

0
No votes yet