Mwananchi, MwanaHALISI kufungiwa


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 20 October 2010

Printer-friendly version

SERIKALI imeanza upya kuandama MwanaHALISI kwa madai kuwa linaandika habari ambazo “zinaweza kuhatarisha amani.”

Katika barua yake kwa mhariri, Kumb. Na. IH/RN/750/60 ya 15 Oktoba, serikali inasema, “Endapo utaendelea na habari hizo serikali haitasita kukuchukulia hatua za kisheria.”

Onyo la serikali linafuatia barua yake ya awali, Kumb. Na. IH/RN/750/58 ya tarehe 8 Oktoba iliyotaka mhariri ajieleze kwa nini asichukuliwe hatua za kisheria kwa kuandika kile ilichoita habari za uchochezi chini ya kichwa cha habari, “Njama za Kuiba Kura Hizi Hapa.”

Habari hiyo ilichapishwa na gazeti hili toleo Na. 209 la Oktoba 6 hadi 12 mwaka huu.

Pamoja na mhariri kujibu barua hiyo, akieleza kuwa hakuna, popote pale katika habari husika ambako kuna uchochezi, Msajili wa Magazeti amesema katika mawasiliano mapya, kuwa hakubaliani na maelezo.

Ametishia “kuchukua hatua za kisheria.” Kwa mujibu wa sheria katili ya magazeti ya mwaka 1976, waziri aweza kufungia gazeti lolote, wakati wowote, hata bila kutoa taarifa wala sababu za kufanya hivyo.

MwanaHALISI liliwahi kufungiwa kwa siku 90 mwaka 2008 kwa madai hayohayo ya serikali.

Taarifa zilizofikia gazeti hili zinasema gazeti jingine la Mwananchi, nalo limetishiwa kufungiwa au kufutiwa usajili “kwa mujibu wa sheria,” kwa kile serikali imeita “Kuandika habari zenye mwelekeo wa uchochezi wa kudhalilisha.”

Barua ya Msajili wa Magazeti Kumb. Na. ISC/N.100/1/VOL.V/76 ya 11 Oktoba mwaka huu kwenda kwa Mhariri Mtendaji wa Mwananchi, inasema msajili hakuridhishwa na maelezo ya utetezi wa gazeti kuhusu tuhuma za kuandika na kuchapisha “uchochezi.”

Mwandishi huyu ameona nakala ya barua hiyo kwenda kwa Mhariri Mtendaji wa Mwananchi.

Barua zote mbili, kwa MwanaHALISI na Mwananchi, zimesainiwa na Raphael Hokororo, kwa niaba ya Msajili wa Magazeti. 

Habari iliyoleta matatizo kwa MwanaHALISI, ilikuwa inaeleza kuhusu taarifa zilizokuwa zimesambazwa katika miji ya Moshi, Mwanza, Arusha na Dar es Salaam kuwa CCM imefanikiwa kupenyeza wachakachuaji kura katika mchakato wa kupiga na kuhesabu kura.

Maandishi hayo hayakuwa na saini na yalichapishwa kwenye karatasi za ukubwa wa A4.

Vyanzo vya habari vya MwanaHALISI vilikuwa vimearifu kuwa kazi ya kuchakachua matokeo itafanywa kwa ustadi mkubwa kwa ushirikiano na kitengo cha IT katika ofisi isiyo rasmi ya CCM iliyopo Mtaa wa Undali, Upanga, Dar es Salaam.

Akizungumzia tishio la serikali dhidi ya magazeti, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, Absalom Kibanda, amesema, kimsingi tatizo kubwa lipo kwenye sheria nzima ya magazeti ya mwaka 1976 inayompa msajili nguvu ya kufungia vyombo vya habari.

Alisema sheria hiyo ni kandamizi na ndiyo maana wadau katika tasnia ya habari wamekuwa wakiipinga na kutaka ibadilishwe au ifutwe.

Akizungumzia madai ya uchochezi, Kibanda alisema msajili si mamlaka sahihi ya kubaini uchochezi kwa vile hilo ni suala la kisheria zaidi.

Kibanda amesema katika nchi zinazothamini uhuru wa habari, hakuna kitu kinachoitwa uchochezi katika uandishi au vyombo vya habari kwa jumla.

Hata hivyo, amesema tuhuma zozote, na vyovyote zitakavyokuwa zimetungwa, sharti zifikishwe mahakamani kwa uamuzi sahihi wa chambo kinachojulikana kikatiba kuwa kinashughulikia utoaji haki.

“Isije kuwa mwanasiasa au kiongozi wa serikali amekerwa na habari iliyoandikwa na gazeti, halafu anawapa presha MAELEZO na wao wanasema ni uchochezi,” amesema Kibanda kwa njia ya simu.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: