Mwananchi, ng'oa wenyeviti chapombe, wezi


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 01 November 2009

Printer-friendly version

KUNA mlandano wa viongozi wa serikali za mitaa. Aghalabu hawa ni watu wepesi kuonekana kwenye vilabu vya pombe.

Viongozi hawa wanaonekana ni wapiga domo wazuri mfano wa watu waliokosa kazi mahsusi ya kufanya, na matokeo yake wanageuza ofisi za umma kuwa vijiwe vya kujikimu kimaisha.

Hali hii imekuwa hivyo kwenye maeneo mengi ya nchi; mijini na vijijini.

Kwa bahati mbaya wananchi wameamua kuacha iendelee ilivyo kwa kuamini kuwa serikali za mitaa ni uongozi mdogo tu usiokuwa na maana sana kwao, hasa inapokuwa mwananchi mwenyewe amepiga hatua za maendeleo na kujaribu kujikomboa binafsi.

Ni jambo la bahati mbaya kwamba wananchi wengi, tena wakiwamo wasomi, wanapotazama kushindwa kupatikana kwa huduma muhimu mtaani kwao, wanaamini kilichoshindwa ni serikali, tena serikali kuu.

Kila anayelalamika kukosekana kwa amani na usalama mtaani kwake, kutiririshwa maji machafu, kuzagaa kwa uchafu, mazingira mabaya na hata ulevi, anaamini tatizo ni serikali kuu.

Ni kweli serikali kuu ina mkono mrefu unaofika kila kona ya nchi. Ndiyo yenye nyenzo nyingi, inadhibiti dola kwa maana pana ya neno hilo na kubwa zaidi ndiyo yenye mamlaka na kila eneo la nchi.

Pamoja na ukweli huu, yapo mambo mengi ambayo bila ya hata kuihusisha serikali kuu yanaweza kushughulikiwa vilivyo mitaani mwetu.

Chukua usafi wa mazingira; mtaa unaweza kusema ni marufuku taka ziwe ngumu au laini kuonekana zimezagaa; kila nyumba inadhibitiwa kwa taka zake. Hili linawezekana.

Mtaa unaweza kuamua kuanzia kupiga marufuku kusikia kibaka akitajwa mtaani kama kero, na kweli hili linawezekana. Kila kibaka anadhibitiwa na kuchukuliwa hatua stahili na kwa wakati unaofaa.

Mtaa unaweza pia kusema ni marufuku barabara yetu kutopitika mwaka mzima, wakazi wanaunganisha nguvu na kila wakati babarabara husika inatengenezwa. Hilo pia linawezekana.

Haya ni baadhi ya mambo yanayowezekana kutekelezwa chini ya usimamizi wa viongozi wa mtaa. Tena usimamizi ukawa unaozingatia sheria na kanuni za serikali za mitaa.

Yote yanawezekana iwapo uongozi utashirikisha wakazi kupitia vikao vya majadiliano na kuhamasishana na ikibidi hata kuchangishana fedha kwa ajili ya utekelezaji mipango ya maendeleo ya mtaa. Muhimu ni uadilifu kwa kila mhusika.

Mwenyekiti wa kijiji, kitongoji au mtaa anayeweza kuhamasisha haya katu hawezi kuwa chapombe, mzururaji na msambaza majungu kutoka kundi moja hadi jingine. Wapo viongozi wa serikali za mitaa waliofanikiwa kubadilisha maendeleo ya maeneo waliyochaguliwa kuongoza.

Ukitafakari kwa kina sababu mojawapo ya kukwama kwa maendeleo ya mitaani mwetu utagundua ni kukosekana ushirikishaji na uhamasishaji.

Ukiwauliza viongozi wanaochaguliwa watafanya nini au wanaomaliza muda wao walifanya nini, hakika utashangaa kukuta waligombea nafasi hizo kwa sababu zipo, lakini hawakuwa na lolote kichwani la kufanya kwa miaka mitano iliyopita.

Kuna mwanaharakati mmoja alikuwa anazungumzia tangazo la Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) la kuhamasisha uelewa wa watoto wa kike ili waepuke mimba wakiwa shuleni maarufu kwa jina la ‘Sidanganyiki’ na uchaguzi wa serikali za mitaa.

Mwanaharakati huyo alisema wakati mwanafunzi wa kike anayedangayika anabeba ujauzito miezi tisa akisumbuka nayo huku akifukuzwa shule, wapigakura wanaodanganyika kutokana na maneno matamu ya wagombea, watabeba mimba kwa miaka mitano kwa maana hawatapata maendeleo yoyote kwa muda huo.

Hii alisema ni mimba hatari kuliko hata ile ya msichana wa shule ambaye akishajifungua anaweza kurudi shule akaendelea kusoma, lakini mwananchi ukishapiga kura mara moja, hutapata tena fursa ya kujisahihisha kama ulikosea hadi itimie miaka mitano. Hasara kubwa!

Tathimini hii ikitazamwa sambamba na harakati za kusaka kura katika uchaguzi wa ngazi za serikali za mitaa hasa wiki hii ambayo ni ya kampeni, kuna kila sababu ya kuhamasisha umma ukatae kuendelea na utamaduni wa kuwapa watu kura na kubaki kulalamika kuwa waliowachagua wamewasaliti.

Serikali za mitaa mara nyingi zimekuwa vijiwe vya watu wanaoendesha ubazazi, kama vile uuzaji maeneo ya wazi, kubariki uharibifu wa mazingira, lakini baya zaidi, kusaidia kuwapa hifadhi watu waliothibitisha ni kikwazo kwa maendeleo.

Nilitembelea kijiji kimoja mapema mwaka huu nikaambiwa mwenyekiti wake kila siku ipitayo anatengewa pombe ya kienyeji na akinamama wachuuzi wa kinywaji hicho. Nina maana anapata pombe ya bure.

Katika mazingira kama haya ni vipi kwa mfano anaweza kushurutisha vilabu vya pombe visifunguliwe saa za kazi ili watu wafanye kazi za maendeleo na si kuamkia kilabuni.

Au tuseme ni kwa vipi mwenyekiti wa namna hiyo anaweza kudhibiti wachuuzi wakorofi wa pombe hizo wanaopuuza kanuni za usafi na hata pengine kukwepa kulipia leseni za biashara hiyo?

Kwa muda mrefu tumesahau kuwa nyumba imara hutegemea sana msingi imara, uongozi wa serikali za mitaa ndiko mwanzo wa uongozi wa kitaifa. Kama kuna viongozi wa ovyo mitaani ni hakika hata kama ngazi ya taifa kutakuwa na mipango bora kiasi gani ya maendeleo, itakuwa vigumu kufanikiwa.

Sababu kubwa ni hiyo tu: watekelezaji ni watu wasio na ufahamu; wameamkia na kushinda klabuni badala ya kushughulikia maendeleo ya mitaa waliyochaguliwa kuiongoza. Ni chapombe!

Jumapili nilipata bahati ya kushuhudia kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa katika jimbo la Ubungo, nilijifunza kitu kimoja. Kwamba kazi kubwa inayofanyika ni kugawa pombe.

Wapambe wa wagombea wa chama fulani saa 7 mchana tayari walikuwa chakari. Walikuwa wamekunywa pombe nyingi kiasi cha kutisha.

Hawa ndio wanaopita kwenye mitaa kunadi mgombea wao. Swali ninalojiuliza hapa ni kwa kiwango gani chapombe anaweza kuwa mhamasishaji wa maendeleo katika mtaa wake, hata kama ni kuziba mashimo ya maji machafu tu? Bila ya shaka mabadiliko itakuwa ndoto kwake.

Lakini la muhimu zaidi, mgombea asiye shughuli ya maana ya kujiletea kipato halali, anatafuta uenyekiti wa mtaa ili iwe nini? Si anatafuta pa kujikimu maisha?

Ni kwa maana hii, nasihi wananchi wote waliojiandikisha kupiga kura watumie uchaguzi wa Jumapili, kukomesha uongozi wa kibazazi mitaani ili kuleta mabadiliko ya kweli.

Tukianza kwenye uchaguzi huu wa serikali za mitaa, tutakuwa tumejenga msingi imara wa kupata mabadiliko tunayoyataka utakapokuja uchaguzi mkuu wa Oktoba mwakani. Vinginevyo, utabeba ujauzito wa miaka mitano tena.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: