Mwanasheria mkuu aache UCCM wake


editor's picture

Na editor - Imechapwa 11 August 2010

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

MARA baada ya Frederick Werema kuteuliwa kushika wadhifa wa mmwanasheria mkuu wa serikali kuchukua nafasi ya Johnson Mwanyika, alitangaza msimamo wake kwamba hafungamani na chama chochote cha siasa.

Akasema atatekeleza majukumu yake bila kujali au kuogopa chama chochote, msimamo uliofurahiwa na watu wengi.

Lakini, mwishoni mwa wiki, alibadilika akavaa ‘magwanda ya CCM’ akidai anakishangaa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa kuanza kampeni kabla ya muda wake.

Hakushangaa tu, bali alifanya juhudi za kumsaka Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, ili kuishtaki Chadema. Anaona staili ya Chadema kuomba udhamini kwa mgombea urais, Dk. Willibrod Salaa kwa mikutano ya hadhara ni ukiukwaji wa taratibu.

Hapa ndipo nasi tunamshangaa mwanasheria mkuu huyu kwamba alipodai yeye si mwanachama wa chama chochote cha siasa ilikuwa danganya toto; kwa kauli hii amejifunua yeye ni CCM, na hapendi kuona chama kingine kikifanya kupita chama chake.

Tunahoji kwa nini mwanasheria mkuu anaishupalia Chadema wakati baada ya mkutano mkuu wa CCM kuwapitisha Rais Jakaya Kikwete kugombea urais huku mgombea mwenza akiwa Dk. Mohamed Gharib Billali, na Dk. Ali Mohamed Shein kupitishwa kuwania urais Zanzibar, walifanya mikutano minne ya kampeni Bara na Visiwani?

CCM walifanya kampeni Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, pili waliwapa mapokezi makubwa Dar es Salaam na wakawa na mkutano wa hadhara katika viwanja vya Mnazi Mmoja.

Baada ya hapo Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume aliwapokea Dk Shein na Dk. Bilali na kufanya mikutano ya kuwatambulisha Unguja na Pemba. Tofauti iko wapi ya CCM na Chadema?

Katika mikutano hiyo, wagombea wa CCM walijinadi na kupiga kampeni huku wakiviponda vyama vya upinzani. Mwanasheria alikuwa wapi kuzuia?

Aidha, katika mikutano hiyo, walitangaza mikakati mizito ya kufanya kampeni za nyumba kwa nyumba hadi kieleweke. CCM imechapa matangazo na kubandika kwenye magari yakisema “Chagua Kikwete 2010”. Mwanasheria haoni?

Tunafurahi kwamba, waandaaji wa shughuli za uchaguzi—Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)—wamepuuza kwani wanaona wanachofanya CCM ndicho wanafanya Chadema.

Tunamshauri mwanasheria mkuu kwamba kama anataka kulinda taratibu basi awe na ujasiri wa kuinyoshea pia kidole CCM siyo wapinzani tu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: