Mwigulu: Mtunza ‘mabilioni’ CCM


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 10 August 2011

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii
LAMECK Nchemba Mwigulu

LAMECK Nchemba Mwigulu (33), ni mmoja wa vijana wanaotarajiwa kuwa hazina ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika miaka ijayo. Ni mbunge wa CCM katika jimbo la Iramba Magharibi.

Jina la Mwigilu liliibuliwa na mwenyekiti wa chama hicho taifa, Rais Jakaya Kikwete, Aprili mwaka huu alipomteua kuwa Mweka Hazina wa chama hicho.

Mwigulu hakuamini haraka kuwa ameteuliwa. Alikuwa miongoni mwa wengi ambao hawakuamini haraka kuwa sasa yeye ndiye katibu wa idara ya Fedha na Uchumi ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).

Katika mahoajino yake na MwanaHALISI wiki hii mjini Dodoma, Mwigulu anakiri, “Binafsi, sikuamini haraka na wala sikutarajia kupewa nafasi hii.”

Anasema, hata pale aliposikia sekretarieti ya chama chake imevunjwa, hakuwahi kufikiria hata mara moja kupewa nafasi hiyo nyeti.

“Kwa kweli, nilishtushwa sana niliposikia naitwa ofisi za chama kukabidhiwa jukumu hili zito la kuwa mweka hazina wa chama chetu. Kutokana na umuhimu wa nafasi hiyo, binafsi nimeona kuwa nimethaminiwa,” anaeleza Mwigulu kwa sauti ya upole.

Pamoja na kwamba kazi aliyopewa ni nzito, hasa katika kipindi hiki cha kupungukiwa mapato ya chama yanayotokana kwa sehemu kubwa na ruzuku kutoka serikalini, lakini anaamini kuwa ataweza kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa.

Anasema, “Ni kweli mapato yamepungua. Lakini kubwa nililopanga kulitekeleza katika muda huu mfupi, ni kubuni miradi mipya ya maendeleo, pamoja na kuboresha miradi iliyopo.”

Anasema mbali na kuboresha miradi iliyopo, amejipa kazi nyingine kubwa ya kusimamia mapato ya chama chake na “kuviangalia upya vyanzo vya mapato yakiwemo malipo ya ada za wanachama.”

Hata hivyo, Mwigulu anakiri kuwa katika eneo hili la udhibiti wa mapato na malipo ya ada za wanachama, atakutana na vizingiti vingi vinavyotokana na utamaduni wa miaka mingi wa kutoheshimu taratibu za fedha. Hata hivyo, anajipa moyo kuwa atafanikiwa.

“Kila penye nia, jua basi pana njia. Pamoja na changamoto hizo, nitafanikiwa kwa kuwa viongozi wangu wakuu ndani ya chama, hasa katibu mkuu Wilson Mukama, makamu mwenyekiti Pius Msekwa, pamoja na mwenyekiti mwenyewe, Rais Kikwete, wote wanaamini ili chama kiweze kufanya shughuli zake vizuri, ni lazima kidhibiti mapato na matumizi yake na kihimize wanachama wake kulipa ada zao,” anasema Mwigulu kwa kujiamini.

Kabla na baada ya kuanzishwa mfumo wa vyama vingi nchini, kwa sehemu kubwa CCM kilikuwa kinategemea mapato yake kutokana na ruzuku inayotolewa na serikali.

Hata hivyo, matokeo ya uchaguzi ya mwaka huu yanaonyesha chama hicho kimepoteza karibu Sh. 500 milioni kutoka zile kilizokuwa kinapata huko nyuma. Hii ni kwa sababu, wananchi wengi walipigia kura upinzani.

Mwigulu anakiri hilo. Bali anasema, “…Lakini hiyo haina maana shughuli za chama zitasimama au kupwaya. CCM kina mapato mengi, hasa yanayotokana na ada za wanachama wake. Hivyo, usiwe na shaka kila kitu kitakwenda vizuri.”

Hata hivyo, Mwigulu hataki kuzungumzia sana masuala ya CCM kwa sasa, kwa maelezo kwamba bado ni mgeni katika nafasi hiyo.

Akizungumzia jimbo lake la uchaguzi la Iramba Magharibi, Mwigulu anasema linakabiliwa na matatizo mengi, miongoni mwao likiwa uhaba wa maji safi na salama kwa matumizi ya binadamu na mifugo.

“Tatizo kubwa Iramba ni ukosefu wa maji. Vijiji vingi havina maji; Singida yote inapata mvua mara moja kwa mwaka. Ukosefu huu wa maji umewalazimisha baadhi ya watoto wa shule za sekondari, hasa wasichana, kushindwa kumudu masomo yao vizuri kutokana na kutumia muda mwingi kufuata maji maeneo ya mbali kutoka shuleni,” anaeleza kwa sauti ya masikitiko.

Anasema, “Ukosefu wa maji unawalazimisha vijana hawa kufuata maji umbali mrefu, tena wakati mwingine inafika saa nane usiku hawajapata huduma hii kutokana na foleni.

Jambo hili limerudisha nyuma, kwa kiasi kikubwa, maendeleo ya vijana wetu kutokana na kutumia muda mwingi kusaka maji, badala ya kusoma.”

Akifafanua, Mwigulu anasema, “Tatizo hili lipo sehemu nyingi, bali ni kubwa zaidi katika vijiji vya Kizonzo, Mseko, Kipuma, Misilango, Tulya, Luono, Kishanita, Nguvu Mali, Mingela, Ng’anguli, Ujungu, Mlandala, Zenzilege, Misuna, Mbelegeze, Uleno na Kinampanda.”

Je, ilikuwaje tatizo hilo likawa kubwa kiasi hicho? Mwigulu anajibu, “Haya ni maeneo ambayo yalikuwa yanatumia mashine za upepo, lakini sasa nyingi zimeharibika na spea zake hazipatikani. Hospitali ina nesi mmoja ambaye ukienda unamkuta ameenda kufuata maji. Hili ni jambo la hatari sana. Nakuambia ndugu yangu, watu wengi wanaamua kuacha kazi kule kwetu kwa sababu ya ukosefu wa maji.”

Anasema kutokana na ukubwa wa tatizo hilo, shughuli nyingi za maendeleo zinasimama. Shule hazijengwi. Kilimo kimedorora. Uvuvi na ufugaji, nanyo vimeathirika vibaya.

Kuhusu barabara, Mwigulu anasema barabara nyingi zilizopo jimboni mwake hazipitiki, ukiondoa barabara ya lami ya Singida kwenda Mwanza kupitia Shelui na Singida hadi Kiomboi kupitia Ushora.

Anayataja maeneo mabaya sana kuwa ni Mtoa, Mtekete, Urugu, Tulya, Kidaru na baadhi ya vijiji vya Luzilukulu, Luluma na Maluga ambako anakotoka.

Anasema wakati anataka kufika kijijini kwao Makinda, inambidi aache gari lake Marugu au Kengenge, karibu kilomita 10 kabla ya kufika kwao. Anasema katika kipindi cha mvua hata pikipiki haiwezi kupita.

Anasema, “Maeneo haya hayana hata vituo vya afya. Hakuna hospitali. Kituo pekee kinachotegemewa ni kile cha Mgogo, jambo ambalo linawapa matatizo makubwa akina mama wajawazito.”

Akizungumzia maendeleo ya elimu hasa ujenzi wa shule za sekondari, Mwigulu anasema pamoja na matatizo yaliyopo, angalau katika eneo hilo kuna maendeleo kwa kuwa kila kata ina shule na baadhi zina hadi shule mbili.

Jimbo la Iramba Magharibi lenye kata 17, lina jumla ya shule 22 za sekondari. Baadhi ya shule hizo, ni Kizago, Mkulu, Ushora, Tumaini iliyopo kata ya Kinampanda, Lulumba, Kinambeu, New Kiomboi na Kisiriri zilizopo kata ya Kiomboi.

Hata hivyo, Mwigulu hafichi tatizo la uhaba wa walimu. Anasema baadhi ya shule hazina walimu wa kutosha na nyingine zinaendeshwa na walimu wa kujitolea.

Tatizo jingine ni uhaba wa madawati. Wazazi wengi hawana uwezo wa kuchangia madawati, jambo ambalo linawafanya baadhi ya wanafunzi kuacha shule badala ya kujiviringisha katika vumbi na wanachofundishwa hakiingii.

Kuhusu nishati ya umeme, Mwigulu anasema eneo lake halijui msamiati wa umeme. Anasema umeme wa gridi ya taifa upo Kiomboi, Ndago, Kinapanda na Shelui tu; maeneo mengine yote ya pembezoni hayana umeme.

Tatizo jingine linalolikabili jimbo lake, ni ukosefu wa hosteli ambako wanafunzi wangekaa huku wakienda shuleni; hasa kwa vijana wa kike. Anasema tatizo hilo limesababisha baadhi ya wasichana kukatisha masomo.

Akizungumzia hospitali ya wilaya ya Kiomboi, Mwigulu anasema anaomba serikali kuiangalia kati ili kupanua hospitali hiyo, kwa kuwa hivi sasa ni ndogo ukilinganisha na mahitaji. Anasema hospitali inakabiliwa na uhaba mkubwa wa wodi.

Hata baadhi ya kata ambazo zimebahatika kuwa na zahanati na vituo vya afya, nako hakuna wataalamu wa kutosha.

Alipoulizwa amefanya nini hadi sasa katika ubunge wake kusaidia angalau kupunguza matatizo yanayowakabili wananchi wake, Mwigulu amesema ameshiriki ujenzi wa kituo cha afya cha Mtekete ambako ametoa mifuko 30 ya saruji, Shehi mifuko 30 na Kidaru ambako ameahidi kusaidia kukamilisha ujenzi wa kituo chao cha afya.

Mwigulu ni mtoto wa Asha Omari na Nchemba Madehu. Alizaliwa tarehe 7 Julai 1978 katika kijiji cha Makunda, tarafa ya Kinampanda, wilayani Iramba.

Alipata elimu yake ya msingi katika shule ya msingi Makunda, wilayani Iramba kati ya mwaka 1987 na1993. Amesoma hadi shahada ya pili ya uchumi katika chuo kikuu cha Dar es Salaam. Ameoa na ana mtoto mmoja.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: