Mwinchande na Tume inayofuata sheria


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 26 May 2009

Printer-friendly version

MWENYEKITI wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Khatibu Mwinchande, kada mkubwa wa Chama cha Mapinduzi (CCM), anasema utendaji wa Tume unazingatia sheria na kanuni tu, si vinginevyo.

Anaaminisha wananchi kwamba chini ya usimamizi wake, ZEC yenye historia mbaya kiutendaji, inatekeleza majukumu yake kwa misingi ya Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar Na. 11 ya mwaka 1985.

Mwinchande anaapa hataki kuburuzwa na vyama vya siasa. Hii ina maana kwamba ZEC haitatenda kazi zake kwa shinikizo la Chama Cha Mapinduzi (CCM), au yeyote yule. ZEC kwa mujibu wa Mwichande, itatenda kazi kwa mujibu wa sheria.

Tambo na msisitizo wa kufanya kazi kwa “sheria na kanuni” ni ishara ya umadhubuti wa kiongozi popte pale, hata mpirani. Ni ushahidi wa namna anavyotambua dhamana aliyopewa.

Mwinchande anazungumzia utendaji adilifu. Kujali sheria na kanuni ni kuheshimu uadilifu. Hata kwenye familia, kutenda au kutekeleza wajibu kwa kuzingatia uadilifu, unaepusha maafa. Ila utendaji huu hutegemea nia njema.

Naamini msimamo wa Mwinchande ni majibu kwa Chama cha Wananchi (CUF) ambacho viongozi wake walishinikiza (sana) Tume itoe Daftari la Kudumu la Wapiga Kura (DKWK) mapema kabla ya uchaguzi mdogo wa jimbo la Magogoni. Uchaguzi huu ulifanyika Jumamosi.

Utendaji adilifu unahitaji usawa na uwazi, pamoja na ile “nia njema.” Kutenda kwa mujibu wa “sheria na kanuni” lazima kufanywe kwa usawa wakati wote na kwa kila jambo. Hivi ni vigezo muhimu vya utendaji adilifu. Ni matumaini ya wananchi tume iwe wazi.

Mtu asipojibu hoja zinazotokana na utendaji wake kila siku anaficha mambo. Anatakiwa siyo tu kujibu, bali kujibu kwa ufasaha na kwa wakati.

Moja: hadi leo Mwinchande hajaeleza sababu za wapiga kura wa Magogoni kupungua kutoka 9,247 walioandikishwa kwa uchaguzi mkuu uliopita kufikia 5,500 walioandikishwa Aprili.

Haijaelezwa kwanini watendaji wa Tume vituoni walikwamisha watu kuandikishwa badala ya kurahisisha utaratibu ili wengi zaidi waandikwe kwa kuwa ni haki ya kila mtu kupata fursa ya kikatiba ya kuchagua na hilo ni jukumu kuu la Tume.

Wakati kuna watu wengi wanaendelea kulalamika walinyimwa haki hiyo na hivyo hawajaingizwa kwenye daftari – hata wale wachache waliopewa haki hiyo mahakamani – imethibitika Tume imebadilisha shahada za wapiga kura 3,600 tu.

Nini maana yake? Ni hujuma. Tume iliandikisha watu hewa mwaka 2005 au kwa makusudi imesaidia watu wanyimwe haki ya kuandikishwa.

Pili: Tume haijaeleza mpaka sasa kwanini kitambulisho cha Mzanzibari kimetumika kushurutisha mtu awe nacho ndipo aandikishwe? Tume hiihii ilikataa mwaka 2005 kitambulisho kuhusishwa na uandikishaji.

Je, Sheria ya Uchaguzi imerekebishwa na sasa kipo kipengele kinachoshurutisha hivo? Tume haijaeleza jambo hili, zaidi ya vile ilivyolazimishwa kupigia magoti serikali ya CCM iliyotoa agizo hilo.

Je, Tume hawajui kwamba hata kitambulisho hicho kilipotolewa 2005, wengi walinyimwa kwa mikakati ya serikali na leo isingekuwa busara kushurutisha mpiga kura kuonesha kitambulisho hiki na kwamba badala yake ingefaa tu akaonesha shahada aliyoitumia kupiga kura 2005?

Mwinchande alikuwa Kamishna wa Tume ya Uchaguzi 200. Je, amesahau tume haikutoa daftari kwa vyama vya siasa ili kuangalia majina ya wapiga kura mapema? Matokeo yake mamia walihangaika kutafuta majina yao dakika za mwisho, na wengi walishindwa kupiga kura.

Amesahau Tume hiihii siku ya mkesha wa uchaguzi mkuu uliopita ndipo iliwapa CUF daftari kwa njia ya mtandao wa kompyuta (disk) tena lisilokuwa na picha za wapiga kura na ambalo lilikuwa na orodha isiyoonesha kituo cha mpiga kura?

Hilo lilikuwa daftari ambalo uhakiki wake ulijaa vichekesho, mzaha, mazonge na mizengwe. Ni daftari lililoleta mtafaruku mkubwa kati ya Tume na vyama kwa upande mmoja; Tume na wahisani; na kati ya Tume na kampuni ya Waymark ya Afrika Kusini iliyopewa kazi hiyo lakini ikadaiwa iliiba orodha.

Gazeti lililotumika kuchafua mambo kwa maslahi ya mabwana wa waandishi waliokuwa wakiliandaa, lilitangazia wananchi kuwa wataalamu wa Waymark walifurushwa baada ya kukutwa katika chumba cha kompyuta wakipekua mfumo wa utunzaji takwimu ili kuziiba. Hatimaye walirudi hotelini Serena Inn mikono mitupu.

Waymark walituhumiwa kuiba orodha ya majina 30,000 ya watu walioandikishwa – badala ya 10,000 walivoruhusiwa kimkataba – na katika kuhakiki, walibaini asilimia 6.7 ya majina hayo, yalikuwa yameandikishwa zaidi ya mara moja.

Kuonesha Tume chini ya Mwinchande haijajitahidi kujenga imani ili iaminike kuwa inatenda kwa “sheria na kanuni,” ilibandika majina ya wapiga kura wa  Magogoni usiku wa Ijumaa, mkesha wa uchaguzi.

Sheria inasema ubandikaji (au utangazaji) majina ya wapiga kura ufanywe angalau siku saba kabla ya siku ya uchaguzi. Je, mwenyekiti Mwinchande “saba” na “saa chache kabla ya uchaguzi” vinalingana? Sheria ipi iliyotumiwa?

Hii ni mifano ya masahibu yanayoikumba Tume. Haijaonyesha khasa “nia njema.” Hapo kupatikana utendaji adilifu ingali mtihani.

Huo ni uchaguzo mdogo tu na wa jimbo moja. Lakini wakuu wa Tume wajue kinachofanywa wakati wwa uchaguzi mdogo, kitachukuliwa kama ishara ya vurugu utapokuja uchaguzi mkuu mwakani.

Yaliyotendeka Magogoni, yamefanywa miezi 17 tu kabla ya Oktoba 2010. Hapana. Ni miezi michache kabla ya Tume kuanzisha utaratibu wa kubadilisha shahada za wapiga kura na kuandikisha wapya waliotimiza umri wa miaka 18. Nini fikra za Mwinchande na wenzake katika wakati ambao inaaminika kuchezea daftari ni msingi mkuu wa kuchezea matokeo ya kura?

Ukiwasikiliza wajuzi wa teknolojia ya kompyuta, utaamini Mwinchande ameshabenwa na serikali ya CCM kwa kuridhia kazi ya kubadilisha shahada za wapigakura kufanywa na kampuni ya Israel – OTI – yenye uhusiano na INFOTECH, iliyolipwa mabilioni mwaka 2005 kwa kazi ya kutoa kitambulisho cha Mzanzibari ambacho mwakani pia kitabadilishwa.

Muda utaamua iwapo kazi hizi mbili tofauti – ubadilishaji shahada na kitambulisho – zitafanywa sambamba. Serikali ya CCM inatuambia inataka kuimarisha umadhubuti wa vyote hivyo, shahada na kitambulisho.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: