Mwinchande na Tume inayofuata sheria


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 19 May 2009

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

MWENYEKITI wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Khatibu Mwinchande anaapa yeye na wenzake hawatakubali kusikiliza maelekezo au kufuata shinikizo za vyama vya siasa au mtu yeyote iwapo kuyafuata ni kuvunja sheria ya uchaguzi na kanuni zake.

Katika ufafanuzi wake, anasema “Si kama tunawanyima kwa utashi wetu. Hakuna kipengele katika Sheria ya Uchaguzi kinachoruhusu vyama vya siasa kupewa daftari la wapiga kura kabla ya uchaguzi. Haki hiyo iko kwa wananchi pekee kwa wakati uliobainishwa.”

Msimamo wa Tume kutokuwa tayari kuburuzwa na yeyote, si mpya. Amepata kuutoa huko nyuma kama ambavyo baadhi ya makamishna walivyopata. Kauli hiyo ilianza kutolewa Tume ilipokutana kwa mara ya kwanza na viongozi wa vyama vya siasa mwaka 2007.

Ni maneno mazito. Kwa kuyatafakari, unapata picha kwamba Mwinchande na wenzake wamejidhatiti kuendesha mambo kulingana na Sheria ya Uchaguzi Na. 5 ya mwaka 1985 pamoja na kanuni zilizotungwa kusaidia utekelezaji wake.

Baada ya hapo, mtu unatarajia hata mwenendo wa Tume kiutendaji uwe unaozingatia msimamo huo.

Mwinchande ametoa majibu ya kilio cha Chama cha Wananchi (CUF) cha kutaka kipatiwe daftari la kudumu la wapiga kura kwa ajili ya kutazama majina ya wapiga kura wa jimbo la Magogoni, Wilaya ya Magharibi, Unguja watakaoshiriki uchaguzi mdogo wa uwakilishi hapo 23 Mei.

Viongozi wa chama hiki, wamekuwa wakishinikiza Tume itoe daftari hilo ili kuangalia majina ya wapiga kura. Tume inasema kisheria majina ya wapiga kura hubandikwa baada ya uandikishaji ili watu waweke pingamizi kwa yale waliyodhani si halali. Vinginevyo, Tume inawajibika kubandika majina hayo siku nane kabla ya siku ya uchaguzi.

Kwanini CUF wanadai kupatiwa daftari kabla? Viongozi wao wanasema wamekuwa na wasiwasi idadi kubwa ya wapiga kura hawamo katika daftari kwani kulikuwa na mbinu nyingi za kuzuia watu kutumia haki yao ya kikatiba kuandikishwa.

Wanataja uzoefu uliopo wa Tume kutokuwa wazi na adili katika utendaji kazi wake. Kumbukumbu za yaliyotokea mwaka 2005 na kabla ya hapo, ni vigezo kwao kuamini utamaduni wa rafu, hasa kwa kuwa haikusikiliza malalamiko ya walionyimwa kuandikishwa.

Mwinchande anaposhikilia kufuata sheria na taratibu hajakosea. Lakini anapaswa kuangalia upande mwingine. Iwapo hakuna sheria inayoruhusu daftari kutolewa mapema, ipo inayokataza? Na katika mazingira haya ya Tume kutoaminika, haoni kuachia baadhi ya mambo yasiyozuiwa na sheria, ni jambo jema kwa faida ya kujenga imani kwa watu?

Hata kama sheria hairuhusu, kwa vile pia haikatazi, Tume ina mamlaka ya kutoa maamuzi yanayoelekea katika kudhihirisha ilivyo wazi na adili kiutendaji.

Lakini hebu wasomaji kwanza mjueni huyu Mwinchande ni nani hasa na ametoka wapi. Ni kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) aliyekuwa mtumishi serikalini kwa muda mrefu. Aliteuliwa na rais baada ya kupendekezwa jina lake na CCM, kama mmoja wa makamishna wawili wa Tume kutoka CCM kwa ajili ya kusimamia uchaguzi mkuu wa 2005.

Tume hiyo, chini ya Mwenyekiti Masauni Yussuf Masauni, ofisa mstaafu wa Idara ya Uhamiaji ilishutumiwa kwa kutenda kwa maelekezo ya CCM na serikali yake na ilithibitisha hilo kwa kulalamika katika ripoti yake baada ya uchaguzi, kwamba pamoja na matatizo mengine, iliingiliwa kiutendaji na serikali na taasisi zake nyakati tofauti za mchakato wa uchaguzi.

Rais Amani Abeid Karume alipounda tume mpya ya kusimamia uchaguzi mkuu wa 2010, alimtaja Mwinchande mwenyekiti. Makada wenzake katika Tume hiyo ni pamoja na Said Bakari Jecha, waziri katika serikali zilizopita za CCM na mtu ambaye rekodi yake ya utumishi ya tangu serikali ya kwanza baada ya mapinduzi ya 12 Januari 1964, ingali vichwani mwa watu.

Kwa hivyo, Mwinchande, kada mzuri wa CCM, anaongoza tume inayotakiwa kufuata sheria na taratibu. Lakini hii ni tume ambayo inaendeleza watendaji wa kiutawala waliopo tangu 1995. Nasema Mwinchande, kada mzuri wa CCM, anaongoza tume ambayo rekodi yake ya utendaji ni mbaya.

Tangu uchaguzi wa 1995 wakati Mwenyekiti alipokuwa Zuberi Juma Mzee, msomi wa stashahada (diploma) ya sheria ya Chuo cha Mzumbe, hadi uchaguzi uliopita, tume ilikumbwa na tuhuma na shutuma nyingi za utendaji mbovu na uliojaa udanganyifu na upendeleo kwa Chama cha Mapinduzi.

Lazima niseme, Tume hii haijatenda kosa lolote kwa mtazamo wa CCM, chama ambacho kiongozi wake mwandamizi mwaka 1995, alikataa matokeo ya uchaguzi wa rais, wakati tukisubiri yatangazwe na Mwenyekiti Zuberi, lakini yalipotangazwa tu yakionyesha kuwa wameshinda, aliyakubali, na haraka akatimikia ofisini Kisiwandui ambako alipofuatwa, alijitetea; “hata angekuwa nani angebadilika.”

Duru za kiusalama wakati ule wa kusubiriwa matokeo ya urais, zilisema matokeo halisi yaliyokusanywa kwenye vituo vya uchaguzi yalionyesha CCM imeshindwa. Haya ndiyo matokeo yaliyotangazwa na kituo cha televisheni cha Dar es Salaam (DTV) ambayo yalikuja kukanushwa na Tume na serikali na hatimaye kituo hicho kuadhibiwa.

Dk. Salmin Amour Juma, mgombea wa CCM, alipoulizwa kuhusu matokeo hayo, alisema “ushindi ni ushindi tu hata ukiwa wa goli moja.” Alitoa kauli hiyo kwenye nyumba ya Bosnia, Maisara, alipoulizwa anachukuliaje ushindi mwembamba aliopata. Alipata asilimia 50.2 ya kura dhidi ya 49.8 za Maalim Seif Shariff Hamad wa CUF.

Majibu ya Mwinchande kuhusu shinikizo za CUF kutaka daftari la wapiga kura litolewe hadharani mapema, yanakuja ndani ya simanzi zilizowajaa wananchi wa Magogoni, ambao wengi wamenyimwa fursa ya kuandikishwa kwa sababu mbalimbali ikiwemo ya kutokuwa na kitambulisho cha Mzanzibari, ambacho kisheria, sasa ni shurti la mtu kuandikishwa.

Kitambulisho hiki kilipingwa na vyama vya upinzani kilipotangazwa mwaka 2005 kuwa kitatolewa kwa kila Mzanzibari. Walitoa madai kwamba kinaletwa kwa malengo ya kuvuruga uchaguzi wa 2005. Serikali ilitetea kwa nguvu na kuwahakikishia wananchi kuwa haina malengo ya kukihusisha na uchaguzi na kwamba ni haki ya kila mwananchi. Sheria ya kutoa kitambulisho inasema Mzanzibari asiyekuwa na kitambulisho hiki, anatenda kosa na anaweza kushitakiwa mahakamani.

Lakini wakati vyama vya upinzani vilipohimiza wananchi wapate kitambulisho, utoaji wake ulikuwa wa mazonge mengi hata watu kulazimika kuhonga watendaji wa serikali ndipo wakapata kuandikishwa. Mamia ya watu walijeruhiwa katika harakati za kusajiliwa ili kupata kitambulisho.

Tume chini ya Mwinchande karibu itaanza kutoa shahada mpya badala ya zile zilizotolewa kwa uchaguzi uliopita. Wakati huohuo, Idara ya Usajili na Vitambulisho vya Mzanzibari nayo itabadilisha kitambulisho ilichotoa wakati ule kwani muda wake unamalizika Julai mwaka ujao. Uhusiano wa mambo haya yaliyoambiwa hayaoani kwa namna yoyote, ndiyo mada yangu wiki ijayo. Inshaallah.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: