Mwisho mbaya wa Mkapa waja


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 29 April 2008

Printer-friendly version
Rais  Mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa

NIKIRI kwamba mimi si mtaalamu wa nyota na kwa maana hiyo nitakayoyajadili hapa, si suala la unajimu. Naangalia mambo halisi yanayotokea nchini petu.

Nazungumzia hatima ya Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa. Najadili hatima ya kiongozi huyu kwa sababu ya mwelekeo mpya wa kisiasa ulioibuka Tanzania kuanzia Agosti mwaka jana.

Hakuna ubishi kuwa, tangu wabunge wa upinzani waonyeshe ujasiri kwa kusema kisichozoeleka kusemwa awali, kama vile kutaja majina ya viongozi mafisadi hadharani kupitia orodha ya mafisadi iliyosomwa kwenye mkutano wa hadhara uwanja wa Mwembe Yanga, Dar es Salaam. Ni orodha ya waliotuhumiwa kufisidi nchi.

Baada ya kufichuka kwa wizi wa mabilioni kutoka akaunti ya madeni ya nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Tanzania imeona mabadiliko makubwa katika mijadala ya kisiasa na hata hatua zinazochukuliwa juu ya mambo yaliyotendeka.

Kikubwa ni kuvunjika kwa baraza la mawaziri, lakini kabla, mawaziri wenyewe wakiwa wamejionea au kuonja chuki ya wananchi kwa kuzomewa kwenye mikutano ya hadhara. Chuki hii ilitokana na wananchi kufunguliwa macho na wabunge wa upinzani wakielezwa jinsi nchi yao inavyotafunwa.

Kwa hasira ya kusalitiwa, wananchi wakaanza kuamka na kuamua kujitokeza hadharani nao kujadili masuala haya na hatimaye kulaani wahusika na kuibana serikali ichukuwe hatua.

Wenye madaraka yao wakajua mwekeleo wa kisiasa si mzuri. Ingawa CCM wanadai wapinzani waliifitinisha serikali kwa wananchi, wanasahau kilichotokea ni kuzindua wananchi waone hujuma inayofanywa na viongozi dhidi ya nchi yao. Matokeo yake ni taharuki na hukumu ya umma.

Mtiririko wa matukio haya umekuwa sinema iliyoanza, kila hatua ikitazamiwa kama mhusika mkuu atawajibika ili wajue mwisho wa sinema umefika. Baada ya kuwajibika aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, na waliokuwa mawaziri, Nazir Karamagi na Dk. Ibrahim Msabaha, watu walidhani mchezo huenda umeishia hapo.

Waliona kwa wakubwa watatu kutwikwa mzigo wa Richmond habari imekwisha. Haikuchukua muda wameshuhudia Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge, naye anawajibika kwa kutwikwa mzigo wa rada. Kila kukicha umma unajiuliza anayefuatia.

Mwanga unakuja kwa mbali. Tena kwa bahati nzuri umefunuliwa na CCM wenyewe, tofauti na mazoea, wabunge wake wameamka pengine kwa kutambua kuwa unafiki hautalipa wala kuwavusha.

Wamekunjua makucha wanataka kuwapiku Zitto Kabwe na Dk. Willbrod Slaa wa Chadema. Akina Aloyce Kimaro (Vunjo), Godfrey Zambi (Mbozi Mashariki) na Chrisant Mzindakaya, wameibuka wote wa CCM, wanataka kusafisha nyumba yao. Tunaona hatua yao inavyopanua wigo wa picha na washiriki wa ufisadi.

Kwa kauli ya Kimaro bungeni, kwa mara ya kwanza Mkapa anatajwa. Anatajwa kwa machafu ya utawala wake, anatajwa kula njama na kujimilikisha mali ya umma, anatajwa kama kiongozi asiye makini.

Utawala wake unasutwa na kunyooshewa kidole kuhusu mgodi wa Kiwira, uuzaji wa nyumba za serikali, usafi wa Ofisi Kuu, IKULU. CCM wanamsonda kidole yule waliyeaminishwa 1995 kuwa ni kiongozi msafi (Mr. Clean).

Sasa utabiri wangu unanisukuma nianze kuamini katika sinema hii kubwa inayoendelea, hakuna mwisho hadi mhusika mkuu aanguke au aangushwe. Suala la EPA, Meremeta, Deep Green Financial Limited, Tangold, Kiwira, uuzaji wa ATC, ununuzi wa ndege ya rais, wa rada, uuzaji wa TTCL, na mengineyo, yanamkaa Mkapa kooni.

Mambo haya yanazidi kumnyima pumzi na kadri siku zinavyokwenda, anabainika kuwa kiongozi aliyeikosea Ikulu. Anazidi kuthibitika kuwa ukali wake wa kupuuza wananchi na waandishi wa habari na hata mara kadhaa kuwakejeli na kuwatukana, haikuwa bure. Alikuwa na lake jambo!

"Niwatishe hawa ili kombe langu liweze kufunikwa vizuri wanaharamu wasijue kilicho ndani," ndivyo ulivyokuwa mwelekeo wake wa kiuongozi.

Ah, wapi? Ya Mungu mengi. Wabunge wa chama chake aliowageuza wanasesere (1995-2005), wameamka na wanasimama hadharani wakimtaja kwa jina "amekiuka maadili ya uongozi."

Kwamba ule ukali na tambo zake kwamba alikuwa mtu wa uwazi na ukweli haikuwa lolote isipokuwa kutishia nyau ili kujenga kukubalika mbele ya wananchi huku akificha maovu.

Ni kwa mwelekeo huu, watu wanabashiri mwisho wa Mkapa si mwema, kwamba historia ya Tanzania itageuka na kwa mara ya kwanza tutakuwa kama Zambia au Malawi! Tutapata Frederick Chiluba wetu au Bakili Muluzi kwa kushitaki rais mstaafu. Kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, CCM kwa kulazimishwa na nyakati, wanaelekezwa kutambua kuwa kulindana kwenye ofisi za umma, hakulipi.

Kitendo cha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuahidi "serikali inachunguza" suala la Mkapa na aliyekuwa Waziri wake wa Nishati na Madini, Daniel Yona, kujimilikisha mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira kwa bei ya kutupa na kinyume na utaratibu wa tenda, ni ishara kuwa sasa hata Rais Jakaya Kikwete aliyepata kuwaasa Watanzania wamwache Mkapa apumzike na asibughudhiwe kwa kutakiwa kujibu tuhuma nyingi alizoelekezewa akiwa rais, amebadili msimamo katika kumlinda.

Mkutano wa 11 wa Bunge umemalizika mjini Dodoma na kwa hakika umetoa taswira mpya kuhusu siasa za Tanzania. Inawezekana hili ni pambazuko jipya kisiasa nchini, inawezekana pia wale wahusika wakuu wa sinema za ufisadi waliodhaniwa hawagusiki wanaelekea kukalia kaa la moto.

Katika mwelekeo kama huu inakuwa vigumu kutambua namna Mkapa atakavyojinasua katika mawaa yake ya nyuma. Inakuwa ni vigumu kuendelea kuamini kwamba kimya chake kitamuokoa dhidi ya anayotajwa nayo.

Kama serikali ya Rais Kikwete imeamua kutii shinikizo la nyakati na sasa inawajibika kutekeleza yale yanayotakiwa na umma, ikiwa ni pamoja na kuadabisha mafisadi bila ya kujali umaarufu wa mtu kwa jamii, ni suala linalostahili kuungwa mkono.

Lakini kama inajaribu kuonyesha usanii, mwaka 2010 si mbali, akina Kabwe, Slaa na umma kwa ujumla wanaona. Akina Freeman Mbowe na Profesa Ibrahim Lipumba wanaona. Hukumu ya umma itakuwa juu ya Kikwete.

Mwaka jana, baada ya sakata la Buzwagi na EPA kwa kiwango cha chini kabisa serikali ilishuhudia uasi wa umma. Hata ilipokuja Richmond, ilikuwa imeshalainika, ikaacha mambo yaende yanakojielekeza. Ni hivi ndio maana nabashiri mwisho mbaya wa Mkapa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: