Mwisho wa maswahiba CCM


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 06 July 2011

Printer-friendly version
Wazo Mbadala

IPO mifano mingi ya kuonyesha namna viongozi marafiki wasivyoweza kutawala pamoja. Watapingana hadharani, watakorofishana na mwisho, mmoja hutafuta mbinu za kumpoteza mwingine kisiasa.

Hali hii hutokea pale viongozi ‘washikaji’ wanapokuwa na mitazamo tofauti. Mwenye mamlaka kati yao husaka mbinu za kuwamaliza kisiasa marafiki nuksi.

Ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) sasa, Mapacha Watatu ni nuksi. Wanadaiwa kukishushia hadhi chama chao hicho kutokana na vitendo vyao vya kifisadi. Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nauye, amesafiri nchi nzima akitangaza kwamba CCM inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete imepania kuwapoteza kisiasa Mapacha Watatu ambao kwa miaka mingi ni ‘washikaji’ wakubwa wa rais.

Mapacha Watatu wakiafiki maamuzi ya chama, utakuwa mwanzo mzuri kwa CCM, lakini wakigoma kutoka, chama kitayumba na matokeo yake hiyo itadhoofisha serikali. Itakuwa ni kujinyonga kwa CCM.

Hayo yanasubiriwa mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) utakapokamilisha falsafa ya “CCM kujivua gamba” ndani ya siku 120 (Aprili 12-Agosti 12).

Ikitokea hivyo, hakitakuwa kitu kigeni. Hata Mwalimu Julius Nyerere alipishana kimtazamo na akawatuhumu kwa uhaini marafiki zake.

Wanaojulikana haraka ni Oscar Kambona, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, na Bibi Titi Mohamed, mmoja wanawake madhubuti ndani ya TANU.

Kambona, kama ilivyo kwa Mapacha Watatu katika serikali ya JK, alionekana ‘kirusi’ katika uongozi wa TANU na nchi changa na maskini, Tanganyika.

Alihitilafiana na Mwalimu Nyerere tangu mwaka 1962 akipinga Tanganyika kuwa nchi ya chama kimoja. Balozi Kasanga Tumbo ambaye alijiuzulu ubalozi na kurudi nchini kuanzisha chama kilichoitwa Peoples Democratic Party (PDP). Alitaka kupata jukwaa la kupinga mpango huo. Lakini, loo!, PDP ilipigwa marufuku muda mfupi tu na Tumbo akatupwa kizuizini.

Hii ndiyo ilikuwa hofu ya Kambona kwamba hakukuwa na uhakika wa kutoitumbukiza nchi katika udikteta wa chama kimoja cha TANU.

Januari 1964 Jeshi liliasi. Mwalimu Nyerere na Makamu wa Rais, Rashid Mfaume Kawawa, waliingia mafichoni. Kambona ndiye alifanya kazi kubwa ya kutuliza hasira za wanajeshi waliolenga kushinikiza nyongeza za mishahara yao na kutaka nafasi za maofisa wote wa Kiingereza zichukuliwe na wanajeshi wa Kiafrika.

Inadaiwa Kambona angeweza kutumia nafasi hiyo kumwondoa Mwalimu madarakani. Pamoja na juhudi hizo, aligomewa pia na ndipo, akiwa mafichoni, Mwalimu Nyerere aliomba msaada Uingereza, Nigeria na Algeria ambao walizima uasi ule.

Mpasuko wa wazi baina yao ulijitokeza mwaka 1967 Mwalimu alipoanzisha Azimio la Arusha. Kambona, bila ya shaka kwa kuhofia usalama wake, alitoroka akaenda uhamishoni nchini Uingereza.

Vita vya maneno vikaanza na Mwalimu. Juni 1968, Kambona akiwa ziarani Nigeria, kwa mara ya kwanza alimwita Mwalimu Nyerere kuwa dikteta na kuunga mkono harakati za jimbo la Biafra nchini Nigeria kujitenga.

Mwalimu Nyerere alijibu mapigo kwa kudai Kambona alikuwa anapanga kupindua serikali yake na kwamba mapinduzi yangefanyika mwaka 1969.

Binamu wa Kambona; John Lifa Chipaka na mdogo wake, Eliya Dunstan Chipaka, walikamatwa na kutiwa ndani kwa uhaini. Bibi Titi; Waziri wa Kazi, Michael Kamaliza, na wanajeshi wanne wakatiwa nguvuni pia.

Bibi Titi alihukumiwa kifungo cha maisha jela lakini alisamehewa mwaka 1972. Serikali ikabadili barabara ya Bibi Titi kuwa UWT lakini aliporejea CCM mwaka 1991, akarejeshewa ‘barabara yake.’

Mapacha Watatu hawajatoa kauli yoyote tangu NEC-CCM ilipotaka wajivue gamba, ila taarifa zinasema walipoitwa na kuhojiwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa, waligoma kujiuzulu.

Wachambuzi wa sakata hili wanahisi NEC, katika mkutano ujao, ‘ikimwaga ugali’, yawezekana Mapacha Watatu ‘watamwaga mboga.’ Hapo sasa, itakuwa hadithi ya “lipasuke tugawane mbao.”

Vita vya panzi furaha kwa kunguru. Uhasama mkubwa usiotarajiwa unaweza kuibuka na kuvutia kunguru (vyama vya siasa) kuwa katika furaha kwani wataokota mlo wa nguvu (kuwapa kadi) Mapacha Watatu. Itakuaje?

0658 383 979, jmwangul@yahoo.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: