Mwisho wa ubaya ni aibu


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 25 July 2012

Printer-friendly version
Wazo Mbadala

MUNGU anapotaka kuziumbua serikali zinazofanya udhalimu dhidi ya raia katika uso wa dunia, huzipiga kofi na kutibua mipango yao.

Kazi ya ukatili dhidi ya binadamu hufanywa na jeshi au polisi au walioajiriwa kutesa – Uhalifu wa Taifa. Mfano mzuri ni tukio la kutekwa Umaru Abdulrahaman Dikko, aliyekuwa Waziri wa Usafirishaji katika serikali ya Rais Shehu Umaru Shagari wa Nigeria.

Mwaka 1983, Jenerali Muhammad Buhari aliipindua serikali ya Shagari, akatangaza vita dhidi ya maofisa wa serikali iliyopinduliwa akiwemo Dikko aliyekimbilia Uingereza.

Serikali ya kijeshi ilituma majasusi Israel kuomba msaada wa Mossad, ambao inasadikiwa walimtuma ofisa mstaafu tu, kuchora ramani ya kumteka Dikko na kumrejesha hai Nigeria.

Mungu akatibua, watekaji wakafanya makosa. Kosa la kwanza lilifanyika wakati wa utekaji. Dikko alitekwa muda mfupi baada ya kuachana na mwandishi mmoja wa vitabu.

Katika majadiliano yao ulizuka ubishi, hivyo mwandishi alitoka kwenda nyumbani kuchukua kitabu cha kusaidia kuweka sawa mazungumzo yao. Aliporejea kuendelea na majadiliano, alikuta nyumba wazi; Dikko haonekani.

Mwandishi alisubiri sebuleni; alipoona mwenyeji wake hatokei aligonga chumbani akidhani huenda amelala. Baada ya kumkosa hata chooni, mwandishi alijiridhisha kuwa jambo ovu limetokea akaripoti tukio hilo polisi, nao wakaiarifu Interpol.

Wewe! Interpol walifanya kazi usiku kucha pamoja na kufuatilia mzigo kutoka ubalozi wa Nigeria. Maofisa wa Nigeria walipofika Uwanja wa Ndege wa Stansted na boksi kuuuubwa, wakaambiwa Interpol wanafuatilia mzigo huo.Walishusha boksi hilo na kulitelekeza.

Macho yakawa katika mzigo huo, na kwa vile ndege ilisubiri mzigo wa Nigeria, zaidi ya nusu saa, huku boksi lile halishughulikiwi licha ya magari ya maofisa ubalozi kuonekana uwanjani, Interpol wakazingira.

Ooh! Walipolifungua wakakuta Dikko amelazwa hajitambui huku daktari wa kumchoma sindano ya usingizi akiwa amekaa. Hivyo ndivyo lilivyoparaganyika jaribio la kumrejesha Dikko nchini Nigeria ili ajibu mashtaka dhidi yake.

Hata hapa Bongo, Mungu ameiumbua serikali. Mara ya kwanza ni polisi walipofanya mauaji kutekeleza amri kutoka mamlaka za juu mwaka 1996
Polisi wawili, Koplo Juma Mswa na Konstebo Mataba Matiku walimkimbiza hadi kumuua kinyama aliyekuwa Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Luteni Jenerali Imran Kombe.

Wakati polisi wanamkimbiza hadi kumuua, walisahau kwamba mkewe alikuwa anashuhudia kutoka mahali alipojificha. Huyo ndiye alitoa ushahidi kuwa mauaji yalifanywa kwa makusudi, na mahakama mwaka 1998 ikawahukumu kifo polisi hao.

Lakini wakati mjane na wananchi wakiamini kwamba haki imetendeka, Ikulu iliyotuhumiwa kuwatuma polisi kumuua Kombe, ikatoa ushahidi wa kuhusika kwake nje ya mahakama, ikawasamehe polisi wauaji, sasa wako huru.

Mara ya pili ni mwaka 2006, polisi walipowaua, kwa makusudi, vijana watatu wafanyabiashara wa Mahenge na dereva teksi mmoja jijini Dar es Salaam, walidai ni majambazi na eti ilikuwa katika tukio la kurushiana risasi.

Mungu akawapiga kofi polisi wale wakasahau kwamba wakati wanawateka vijana wale pale Sinza, ndugu yao alishuhudia na ndiye alisimulia mkasa mzima. Polisi waliohusika wakanaswa, lakini Mahakama ikawaachia.

Mwaka huu, maofisa wa Uhalifu wa Taifa wakitumia mbinu za Mossad wakamteka Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka. Mungu akawapiga kofi wakasahau uwepo wa watu katika Baa ya Kibona, akiwapo daktari mwenzake, Dk. Deo Michael.

Saa ya kuaibika imewadia, Dk. Ulimboka huyooooo anarudi!

0658 383 979
0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)