Mzanzibari atafutika ifutikapo dunia


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 07 December 2011

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

MBUNGE wa Uzini, Muhammed Seif Khatib anasema kulingana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, hakuna mtu anayeitwa “Mzanzibari.”

Katiba aliyoinukuu ilitokana na kuunganishwa kwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, People’s Republic of Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika, Republic of Tanganyika, tarehe 26 Aprili 1964.

Khatib, msomi na mtaalamu wa lugha ya Kiswahili, mtunzi wa tungo na vitabu, ni mbunge wa jimbo la nyumbani kwetu, katika Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja.

Anajulikana sana Zanzibar alivyo na mapenzi makubwa na muungano kiasi cha mara nyingi kujikuta akisakamwa kwa kauli zake za kuwaudhi Wazanzibari.

Alipotoa kauli yake hii ya “Hakuna Mzanzibari” alikuwa amemsikia kijana wa Zanzibar, Daudi Ismail Khamis, mtendaji wake mwandamizi wa zamani katika kampuni yake ya Zanzibar Media Corporation (ZMC) inayoendesha kituo cha redio cha Zenj FM, na gazeti la kila wiki la Nipe Habari, akisema wakati wa kujitambulisha, “Mimi ni Mzanzibari kwanza halafu Mtanzania.”

Ilikuwa ni kwenye mdahalo wa wazi kupitia Star TV, Daudi, kijana aliyejaribu bila mafanikio kugombea ubunge jimbo la Wawi, Chake Chake, Pemba, kwa tiketi ya CCM mwaka jana, akitaka kumshinda gwiji Hamad Rashid Mohamed, wa Chama cha Wananchi (CUF), alipouliza “hivi nini hasa hofu ya Watanganyika kwa Zanzibar katika muungano.”

Ninavyoyaona mambo kuhusu muungano, ninaamini Daudi amewakilisha mawazo ya vijana wengi wa Unguja na Pemba ambao ingawa walizaliwa muungano ukiwa umeshakuja, tangu hapo wamekuwa wakisikia wakubwa zao wakiulalamikia.

Kauli kama hiyo ambayo pia husikika kwa Wazanzibari waliozaliwa miaka mingi kabla ya muungano, niliisikia wakati tukijiandaa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, kwa Mohammed Ghassany, ambaye kama Daudi, naye ni mwandishi kijana.

Ghassany alisema miaka 30 ya maisha yake amejikuta ndani ya wigo wa mapambano dhidi ya udhalimu uliotokana na muungano wa serikali mbili anaosema uliopora mamlaka ya Zanzibar kinyume na matakwa ya Wazanzibari.

Ghassany ambaye sasa yuko nchini Ujerumani akifanya kazi na Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Ujerumani (Deutsch Welle), mjini Colon, alisema historia yake imejengwa katika harakati zinazolenga kuipatia nchi mama yake, Zanzibar, uhuru wa kweli uliofilisiwa na muungano.

Waziri huyu wa zamani wa masuala ya Muungano, Khatib, sidhani kama amesahau. Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, ambayo inatambuliwa na Katiba ya Muungano, yupo Mzanzibari.

Katiba hiyo, ya kwanza tangu pale katiba ya uhuru (Zanzibar ilipata uhuru 10 Desemba 1963) ilipofutwa na serikali iliyoingizwa kwa mapinduzi 12 Januari 1964, inamweleza Mzanzibari ni nani. Ina maana katiba hiyo imeweka msingi wa kuwepo Mzanzibari.

Ukifungua ukurasa wa kwanza wa Katiba ya Zanzibar, Sura ya Kwanza inayoeleza “Zanzibar na Watu,” utasoma kwenye fungu la Sehemu ya Pili, kitu kiitwacho “Mzanzibari” – Ibara ya 6.

Katika ukurasa wa 3 wa Katiba, kifungu cha kwanza cha Ibara hiyo, kinasema: “Kutakuwa na Mzanzibari ambaye upatikanaji wake, upoteaji wake na urudishwaji wake atakuwa kama alivyoainishwa katika sheria iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi.” Sheria hii ni Sheria Na. 2 ya mwaka 2002.

Ukiyatafakari haya, unaona dhahiri utata mkubwa unaokabili muungano ambao siku hizi unajadiliwa kwa nguvu na hoja nyingi na pande zote mbili, Bara na Zanzibar, tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma ambako ilionekana kama ni uhaini kufanya hivyo.

Hata useme vipi, vijana wa Zanzibar wanajijua kuwa wao ni Wazanzibari zaidi kuliko Watanzania. Ndivyo walivyolelewa kujua na ndivyo walivyokulia. Wanajua nchi yao iliunganishwa na Tanganyika na kuja Muungano, lakini wanajua pia muungano huo uligubikwa na usiri mkubwa.

Wanajua kuwa wakati wa maandalizi ya muungano wenyewe, Wolfghang Dourado, aliyekuwa mwanasheria mkuu wa serikali wakati huo, hakushirikishwa.

Dourado, pengine kwa makusudi ya kuendeleza usiri wa jambo hilo na kulizuia dhidi ya kukwama, alipewa likizo ya muda na mzee Karume.

Badala yake, mzee Karume alimwajiri Profesa Nabudere (amefariki dunia hivi karibuni), mwanasheria maarufu kutoka Uganda, ili ampe ushauri wa kile kilichokuwa kinafanyika. Profesa huyo aliyekuwa gwiji wa fani ya sheria ya katiba, baada ya kuulizwa anaonaje kuhusu mipango ya muungano, alimshauri mzee Karume kwa kumwambia:

“Usikubali chochote unachoambiwa na Mwalimu Nyerere bila ya kwanza kuwauliza mawaziri wako pamoja na viongozi wengine katika serikali yako.”

Mapema mwaka huu, Profesa Nabudere alitoa ushuhuda huo kwenye mkutano wa kujadili ripoti ya utafiti wa matatizo ya Muungano wa Tanzania, uliofanyika jijini Dar es Salaam. Utafiti huo ulifanywa na taasisi ya Kituo cha Katiba cha Afrika Mashariki.

Hata katibu mkuu wa kwanza wa baraza la mapinduzi (BLM), Salum Rashid Ahmed, aliyekuwa katibu wa baraza la mawaziri, alifichwa. Profesa Nabudere alikutana na Salum Rashid na Dourado.

Sasa Wazanzibari wanaamini kwamba ni stahili yao kuitwa hivyo. Mzanzibari yupo, atakuwepo leo na kesho. Atafutika ifutikapo dunia.

Na kwa kuwa wanasisitiza hilo kipindi hiki cha hekaheka za mabadiliko ya katiba ya Jamhuri ya Muungano, ni dhahiri wataendelea kuamini hilo na kulihimiza wakati wa kutoa maoni yao utakapofika.

Wanaamini muungano ulilenga kuimeng’enya mamlaka ya Zanzibar au kufuta historia ya nchi yao maana hata Mzee Karume hakulenga hapo kama ilivyothibitishwa na kauli zake mbalimbali.

Alipigia kelele mamlaka ya Zanzibar kulindwa, na akawa anakejeli kwa kusema “Muungano ni kama koti likikuzidi unalivua.” Kumbe mzee Karume aliahidi “kulivua koti” katika siku za mbele.

Mambo mengi yamefikisha Zanzibar hapo. Wakati ni mojawapo. Kwamba wakati wazee wakiunganisha jamhuri yao, si huu uliopo. Sasa hawataki usiri bali kila jambo lijadiliwe na ukweli ubainishwe.

Sasa wanataka muungano wenye maslahi ya kweli kwao siyo ya hisia. Wanataka muungano wa haki siyo wa uonevu ambao kila siku wanashuhudia wananchi wakilalamika na wanaamini kwa viongozi waliopo, hakuna ufumbuzi tena.

Ni kweli viongozi wa Tanzania, hasa wanaopewa dhamana ya kuongoza serikali, wamewageuka wananchi. Wamekuwa wazito kupindukia mpaka, na labda, si wakweli wa nafsi zao katika kuheshimu mawazo ya wananchi wanaowaongoza.

Haya yote ndiyo yamechochea muungano kuchukiwa na wananchi. Wanauchukulia kama dude lisilofaa.

Wanataka muungano kwa fikra zao siyo kwa fikra za waliouasisi. Wanataka muungano unaokwenda na wakati wa leo; unaotambua na kuzingatia matakwa na matumaini yao. Hakuna kulazimishwa eti waamini ulivyo sasa. Hapana.

Wanataka kuondokana na muungano uliotumika zaidi kisiasa na kusahau ujenzi wa uchumi unaonufaisha nchi mbili zilizoungana.

Na hizo ndio changamoto mbele ya mchakato wa mabadiliko ya katiba.

0
No votes yet