Mzee Ndejembi, kila zama na mji wake


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 07 April 2009

Printer-friendly version
Tafakuri

TUNAJUA kwamba ya kale ni dhahabu, na kwa maana hiyo hiyo uzee ni dawa. Yote haya yakipimwa na kulinganishwa na mkutano na waandishi wa habari ulioitishwa na wenyeviti wastaafu wa CCM wa mikoa minne, akili inaanza kucheza, kwa wingi wa maswali yasiyojibiwa.

Pancras Ndejembi (Dodoma); Hemed Mkali (Dar es Salaam); Jumanne Mangara (Pwani) na Tasil Mgoda (Iringa) walijitosa kueleza msimamo wao na pengine ushawishi kwa wanachama wenzao juu ya kutaka Rais Jakaya Kikwete, agombee kipindi cha pili cha urais.

Sina ugomvi na msimamo wao. Ni haki yao kumfikiria yeyote kuwa mgombea urais kwani mwisho wa yote kura ndizo huamua. Wana haki kumuunga mkono Kikwete.

Ni utamaduni wa CCM – si sheria – kupenda kila rais anayetokana nao apewe fursa ya kuwania vipindi viwili. Hawavunji sheria yoyote katika mapenzi yao hayo.

Pamoja na kutambua haki hiyo, wazee hawa wamekwaza wananchi pale waliposema – kama alivyonukuliwa msemaji wao, Mzee Ndejembi, akisema:

“Kila mwanachama wa CCM anakula kiapo cha kupambana na rushwa. Sote tunaichukia rushwa kwa kiwango sawa na kazi ya kupambana na rushwa si ya kikundi cha watu fulani ndani ya chama ila kila mwanachama.”

Wazee hao walisema jingine linaloelekea kutia doa kubwa juhudi za taifa za kupambana na ufisadi: “Vilevile katika kipindi hiki tunachoelekea uchaguzi mkuu, tusitumie neno mafisadi kutisha au kuzuia wanaotaka kugombea nafasi tunazozishikilia.”

Kauli hizi mbili zikiwekwa kwanye mizani moja ni dhahiri zitawaonesha wazee hawa hawana nia ya kupambana na rushwa.

Waliyonayo ni nia iliyojificha nyuma ya pazia kuhusu kupinga ufisadi nchini. Kwanza wanataka wananchi waamini kila mwana-CCM ni askari wa kupambana na rushwa; lakini wakati huohuo wanataka walarushwa wavumiliwe, wasitajwe, wasisakamwe!

Msimamo huu naona ni wa hatari sana. Hebu tujikumbushe hadi sasa nani anatuhumiwa kwa rushwa na ufisadi nchini.

Tuanze na kesi za wizi wa fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) iliyopo Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Wanaotuhumiwa ni watu wenye mafungamano – iwe ya moja kwa moja au vinginevyo – na CCM. Kati ya walioko mahakamani, ni Rajabu Maranda, Mweka Hazina wa CCM Mkoa wa Kigoma.

Lakini katika EPA hiyo ipo kampuni ya Kagoda Agriculture Limited iliyochota Sh. 40 bilioni. Ni kampuni imekuwa mfano wa jinni; wamiliki wake wanaogopwa kama ukoma. Hawatajwi hadharani na inaaminika mwenyewe ni kada wa CCM na swahiba wa viongozi wa juu.

Nani inamhusu kashfa ya Richmond? Wazee hawa wanajua kwa yakini Edward Lowassa, alifukuzwa uwaziri mkuu kutokana nayo. Wanajua mawaziri wawili waliotumikia Wizara ya Nishati na Madini, Nazir Karamagi (Mbunge wa Bukoba Vijijini CCM) na Dk. Ibrahim Msabaha (Kibaha Vijijini CCM) nao walijiuzulu.

Twende kashfa ya mlungula katika ununuzi wa rada. Amehusishwa Andrew Chenge, Mbunge wa Bariadi Magharibi CCM aliyepata kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa miaka 10 mfululizo.

Kuna kashfa ya mkataba wa ukaguzi wa thamani ya madini yanayochimbwa nchini uliofanywa na kampuni ya Alex Stewart. Wanaokabili mashitaka mahakamani ya matumizi mabaya ya madaraka ni Basil Mramba, Mbunge wa Rombo CCM aliyekuwa waziri mzoefu na Daniel Yona, aliyewahi kuwa mbunge wa Same na Waziri wa Fedha. Wote ni makada wa CCM.

Silumbani na wazee Ndejembi, Mangara, Mkali na Mgoda, isipokuwa waseme kweli kama vigogo wote ambao ni sehemu ya ufisadi mkubwa unaofanywa chini ya kivuli cha CCM kama na wao ni wanachama wa CCM waliokula kiapo cha kupinga rushwa? Je, wanapiga vita rushwa au wanaipalilia?

Naomba nizidi kuwaomba radhi wazee wangu hawa na kuwataka wawe wakweli ndani ya nafasi zao, hivi chanzo cha rushwa nchini ni nini hasa? Je, si viongozi walioko madarakani wanaotumia madaraka yao vibaya kupindisha sheria, kanuni na taratibu?

Hivi Benjamin Mkapa alikuwa nani hasa kwa kipindi cha miaka 10 – Desemba 1995 hadi Desemba 2005? Kumbukumbu zinaonyesha alikuwa Rais wa Tanzania awamu ya tatu. Mwaka 1997 alivikwa uenyekiti wa CCM.

Je, huyu si anatuhumiwa kwa mengi yakihusu matumizi mabaya ya ofisi? Si amekuwa bubu Dar es Salaam ila hujibu vijiji kusiko waandishi watambuzi wa tuhuma zake?

Ni kashfa ipi utataja nchini petu isiguse CCM kama chama au wanachama wake mmoja mmoja? Ipi? Nani kafikisha nchi kwenye umasikini wa kujitakia kwa sababu ya kuzembea matumizi ya raslimali za taifa? Nani? Si ni CCM na viongozi wake kuanzia kwenye uwindaji wa kitalii, uchimbaji madini, ubinafsishaji mashirika ya umma na uzibuaji bomba la maji machafu?

Kuna kila dalili akina mzee Ndejembi walitaka tu kutumia jina la Rais Kikwete ili kuwasilisha kampeni yao ya kutetea mafisadi. Najua kauli hii si nzuri kwao, ila bora kusema ili umma utambue na kuepuka kutumbukia kwenye mtego mbaya wa kubariki mafisadi.

Kupambana na mafisadi kuna njia nyingi; moja ni kukamata watuhumiwa na kuwafikisha mahakamani kama wazee wetu wanavyotaka, lakini njia nyingine ni ya kuwazomea wasikie aibu. Kwa lugha ya watu tunasema “name and shame.” Hizi ni mbinu katika vita, hakuna moja inayotibu maradhi yote.

Kwa mfano, katika jamii kama yetu, ambayo wezi walikuwa wanapongezwa na kuonekana majasiri kwa kuiba mali ya umma, ili kuleta mabadiliko, ni lazima mbinu ya “kutaja jina ili kuaibisha” itumike sawasawa maana ndiyo njia pekee ya kubadili mwelekeo wa mambo, kuvunja utamaduni mbaya wa kusifu matajiri wezi wa mali ya umma na kukejeli watumishi wa umma masikini lakini waadilifu.

Na rushwa na kila aina ya uovu ulioumiza nchi vimetokea wakati akina mzee Ndejembi, Mangara, Mkali na Mgoda wakiwapo. Historia ingewatambua iwapo wangehoji, lakini pia sasa inawatambua kuwa hawakuhoji. Aibu kwao ni huku kujitokeza leo na kubabaisha. Tatizo wamesahau kwamba kila zama na mji wake.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: