Mzigo wa Dowans tumeutua, wa IPTL lini?


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 08 July 2008

Printer-friendly version

TAARIFA kwamba Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limevunja mkataba wa kununua umeme wa dharura kwa kampuni ya Dowans (T) Ltd, kuanzia Agosti 1, mwaka huu, zinatia moyo. Angalau kilio cha wanachi na wawakilishi wao kwenye Bunge kimeanza kusikilizwa. Mkataba huo ulikuwa ukiligharimu taifa Sh. 152 milioni kwa siku.

Uamuzi wa kuvunja mkataba huo umetokana na ushauri wa kisheria wa kampuni ya kisheria ambayo haikutajwa. Mkataba wa awali kati ya Richmond Development Company LLC ulikiuka Sheria ya Manunuzi (Public Procurement Act No. 1 ya 2004) na pia uhamishaji wa mkataba huo kutoka Richmond kwenda Dowans Holdings SA, na kutoka kampuni hii kwenda Dowans (T) Ltd, haukuwa halali kwani ulikiuka msingi wa mkataba.

Inatia moyo kusikia pia kuwa hatimaye Serikali imekubali wale wote waliohusika na tatizo hilo washughulikiwe kwa mujibu wa Sheria. Lakini tunauliza: kwa nini Serikali imejijengea tabia mbaya ya kukalia maovu mpaka wananchi walalamike huku wakiendelea kuumia?

Udanganyifu wa Richmond/Dowans si pekee unaofanywa na kuumiza uchumi wa nchi. Aina ya mfumo na mbinu zilizotumika ni hizo zilizotumika katika uporaji wa fedha za Benki Kuu (EPA); ni mchezo mchafu mkongwe uliotumiwa katika mkataba wa kuuziana umeme kati ya kampuni ya kufua umeme ya Independent Power (T) Ltd (IPTL) na TANESCO miaka ya 1990. Chini ya mkataba huo, TANESCO inalipa Sh. 3.6 bilioni kwa mwezi. Umma umelalamika, wabunge na jumuiya ya kimataifa zimelaani ufisadi huo na Serikali inajua lakini haichukui hatua.

Julai 1994, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Waziri wa Mipango, Horace Kolimba (marehemu), alitembelea Malaysia na kuelezea tatizo la mgao wa umeme kwa serikali huko. Kwa mujibu wa mchumi Brian Cooksey, katika mada yake 'The Power and the Vainglory (Anatomy of a US$ 100 million Malaysian IPP in Tanzania), Kolimba alihakikishiwa Malaysia ilikuwa na uwezo wa kumaliza tatizo hilo na ikamuunganisha kukutana na wawekezaji ambao Agosti 2004 walialikwa kuja Tanzania. Walipata nafasi ya kukutana na maafisa wa Wizara ya Maji, Nishati na Madini.

Na mwezi huo huo, iliundwa kampuni ya ubia kati ya Shirika la 'Mechmar Corporation of Malaysia (lenye asilimia 70 ya hisa) na kampuni ya IPEM (asilimia 30) ya Riaz Bakri Somji (iliyokuwa maarufu kama kiunganishi kati ya Serikali ya Tanzania na makampuni ya kigeni) na kuundwa ubia uliojulikana kama 'Independent Power Tanzania Ltd (IPTL).

Ni wakati huo pia hati ya makubaliano (MOU) ilitiwa saini kwa IPTL kuiuzia TANESCO umeme wa dharura chini ya mradi wa 'Independent Power Project' (IPP) kama hatua ya dharura kusuburi maelewano kamili Novemba kati ya TANESCO na IPTL kupitia kampuni ya uhandisi ya KTA ya Malaysia, Firestone Private Capital Group ya Marekani na Long & Co.; and Clyde and Co ya Uingereza.

Mkataba wa kuuziana umeme (PPA) kati ya IPTL na TANESCO ulitiwa saini mwaka 1995 kwa kuanza na ujenzi na uendeshaji wa mtambo wa megawati 100 aina ya uliopo Tegeta, Dar es Salaam, kwa gharama ya dola 163.5 milioni; na mkataba mwingine wa ununuzi wa vifaa (EPC) wa dola 126.39 milioni. Chini ya mkataba huo, TANESCO inatakiwa kulipa IPTL Sh. 3.6 bilioni kila mwezi; bila ya kujali umeme umezalishwa au la.

Cooksey anasema Mwanasheria Mkuu wa Serikali alishiriki kikamilifu kupitia mkataba huo na kusema unafaa, kinyume na maoni ya wataalamu wa TANESCO, kampuni ya Acres (Canada) na Hunton & Williams ya Uingereza walioeleza wazi kuwa mradi unaoridhiwa licha ya kuwa uliongezwa thamani, ulikuwa haufai; pia uliipendelea na kuipa unafuu IPTL na haukutoa muda wa kukamilisha ujenzi. Na mbaya zaidi gharama ambazo TANESCO ilitakiwa kulipa zingejulikana baada ya mradi kukamilika katika muda usiotajwa.

Kati ya mwaka 1995 na 1996, bila ya kuiarifu TANESCO, IPTL ilijenga mtambo duni zaidi wenye bei ndogo, gharama kubwa za kuuendesha na maisha mafupi wa MSD na gharama za ujenzi zikaongezwa kwa zaidi ya asilimia 33. Februari 1998 ongezeko la gharama za ujenzi liliridhiwa na pande zote mbili, licha ya IPTL kushindwa kuthibitisha gharama halisi na (uhalali) wa malipo ya Sh. 6.4 bilioni kwa kampuni hewa ya Omni Technical Management and Price Consolidated Establishment.

TANESCO walijitahidi kuishawishi IPTL ipunguze gharama baada ya kubadili mtambo wa SSD kwenda wa MSD, hakukuwa na mabadiliko. Ndipo Novemba 1998 ikafunfua mgogoro kwa Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID) mjini London ambako TANESCO ilishindwa.

ICSID ilithibitisha kuongezwa gharama ovyo kwa mradi na uzalishaji wake lakini ilieleza kuwa mabadiliko hayo yaliridhiwa na TANESCO pamoja na serikali na kwa hivyo 2 Februari uamuzi ukaibana TANESCO kutekeleza mkataba.

Maafisa watatu wa Tanzania walitoa ushahidi kwa kiapo kwamba walipewa rushwa na afisa wa IPTL na wawili wakasema walikataa rushwa hiyo, lakini wa tatu alikiri kupokea. Kama maafisa wadogo hawa walikiri kuhongwa kuanzia dola 200,000 (Sh. 200 milioni), wakubwa walipata ngapi? Hapa ndipo mantiki ya mradi huo kuitwa wa kifisadi.

Tangu mwanzo mradi huu hakukubaliwa na umma pamoja na Jumuiya ya Kimataifa isipokuwa Serikali iliziba masikio kwa sababu wakubwa walijua maslahi yao ni mbele ya yale ya Watanzania. Umoja wa Ulaya ulisema bayana, 'inashangaza Serikali ya Tanzania kunyamazia ufisadi huu unaohusisha hata viongozi wa juu wa Chama na Serikali.'

Mwandishi wa Reuters, Mark Dodd, alisikitika kukosa nafasi ya kumhoji Rais Benjamin Mkapa afafanue sababu za wasaidizi wake - Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Waziri wa Nishati na Madini – kutia saini mkataba mbovu ulioelezewa na IMF kama, 'mzigo usiobebeka kwa uchumi wa Tanzania.' 'Watanzania (wasomi) ni wanyonyaji wakubwa wasioonea huruma Watanzania wenzao,' alisema Dodd.

Rais Mkapa alionya mapema: 'Serikali haiwezi kuruhusu watumiaji umeme na uchumi wa nchi hii kubebeshwa mzigo wa ada za umeme kwa njia hii.' Lakini, aliyekuwa Mbunge wa Dodoma mjini, Hashim Saggaf, alibashiri mapema kwa tabia ilivyojengeka ndani ya Chama na Serikali, mafisadi hawatachukuliwa hatua. 'Wale waliotia saini mkataba huu na kubebesha wananchi na uchumi wa taifa mzigo wasiostahili kubeba, si ajabu wataachwa hivi hivi wakaendelea kuchapa usingizi wao salama,' alisema.

Saggaf hakukosea, kwani zaidi ya miaka 10 sasa mafisadi wa IPTL wanaendelea kutanua salama kama vile wanavyotanua mafisadi wa EPA, TICTS, Kiwira Coal Mines, Meremeta, Tangold na kashfa nyinginezo. Wapi Watanzania wanapelekwa?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: