Mzimu wa Ballali watesa BoT


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 03 March 2010

Printer-friendly version
Marehemu Dk. Daudi Balali

UTAWALA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), chini ya Dk. Daudi Balali ulikuwa na utaratibu wa kulipa mawakili wa kukodi wa makampuni tofauti lakini kwa kazi ileile, imegundulika.

Wakati benki hiyo ilikuwa na wakili wake wa kuitetea mahakamani, ilikodi pia mawakili wa makampuni mengine waliokuwa wakitoa ushauri wa kisheria tu katika kesi zilezile.

Hilo ndilo chimbuko la mgogoro unaoendelea kwa miaka miwili sasa kati ya BoT na kampuni ya uwakili ya Malegesi Law Chambers ya Dar es Salaam.

Hivi sasa ofisi ya Gavana, Benno Ndullu inadai kuwa malipo kwa Malegesi yalifanywa kinyume cha utaratibu.

Tayari BoT imefungua kesi ya madai Na. 49 ya mwaka jana, ikitaka kampuni ya Malegesi irejeshe fedha zote ilizolipwa kwa “ushauri” ikidai malipo hayakuwa halali.

Kwa mujibu wa nyaraka ambazo MwanaHALISI inazo, kampuni ya Malegesi ililipwa kwa ajili ya kutoa ushauri wa kisheria kwa BoT, wakati tayari ilikuwa na mkataba na wakili maalum wa benki hiyo, Nimrod Mkono wa Mkono and Company Advocates pia ya Dar es Salaam.

Huku Mkono akilipwa kwa kutetea benki mahakamani, Malegesi alikuwa akilipwa kwa “kutoa ushauri wa kisheria” kwa kesi zilezile za Vallambhia na Rajani Industries.

Vallambhia alikuwa anadai serikali kiasi cha dola 55 milioni (Sh. 71 bilioni) na kampuni ya Rajani Industries ilikuwa inadai dola19.8 milioni (Sh. 25.7 bilioni).

Malegesi aliyekuwa anadai dola 998,000 (Sh. 1.3 bilioni) kwa kazi yake hiyo, alilipwa kwa mikupuo miwili. Kwanza alilipwa dola 499,000 tarehe 10 Aprili 2007 na kiasi kama hicho kililipwa 29 Juni 2007.

Fedha zote zililipwa kupitia akaunti ya Malegesi Na. 011105010522 iliyopo benki ya NBC Limited, tawi la makao makuu, Dar es Salaam.

Mawasiliano ya benki yenye Kumb. Na.180040 ya 5 Machi 2007, yanaonyesha BoT iliamua kuomba ushauri kwa Malegesi kwa vile “inaingia gharama kubwa katika kesi hizo.”

“Kwa barua hii, BoT inaiagiza kampuni yako kutupa ushauri huru na wa kiweledi kuhusu namna benki inavyoweza kusonga mbele katika kesi hizo kubwa,” inasema sehemu ya barua ya BoT kwenda kwa Malegesi.

Barua ya BoT imesainiwa na B.N. Kimela na S.J Lalika wa ofisi ya Mwanasheria wa BoT.

Kimela ni miongoni mwa maofisa wa ngazi za juu wa BoT waliofikishwa mahakamani kwa tuhuma za ukwapuaji wa mabilioni ya shilingi katika akaunti ya madeni ya nje (EPA) ndani ya BoT.

BoT inalalamika kwamba kampuni ya Malegesi, ambayo pia imetajwa katika kashfa hiyo ya EPA, “iliingiza mkenge,” kwa kutozwa gharama kubwa kuliko stahiki.

“Makubaliano yaliyofikiwa kati ya BoT na kampuni ya Malegesi kuhusu utozaji wa gharama ya kutoa ushauri huo wa kisheria yalikuwa kinyume cha sheria na hivyo benki inahitaji kurejeshewa fedha zake,” inasema sehemu ya madai ya benki hiyo.

BoT pia inataka kulipwa riba ya kiasi hicho cha fedha (dola 998,000) katika kiwango cha kibiashara.

Nyaraka zinaonyesha kwamba BoT ndiyo iliyoifuata kampuni ya Malegesi kuiomba ushauri wa kisheria na kuitaka itaje gharama zake.

Kwa mujibu wa hati ya mahakama, kampuni ya Malegesi inapinga madai ya kuiingiza mkenge BoT kwa madai kuwa malipo hayo yalifanywa kwa mujibu wa sheria za nchi.

Kupitia kwa wakili wake, Richard Rweyongeza, Malegesi anadai kwamba malipo hayo yalikuwa sahihi kwa mujibu wa taratibu za malipo ya kazi za kisheria ya Rules for Advocates Remuneration and Taxation of Costs, GN 515 of 1991.

Pande hizi mbili ziko mahakamani kwa mwaka wa pili sasa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: