Mzimu wa kitambulisho na malezi ya demokrasia


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 15 September 2009

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

WAKATI umethibitisha. Watu hawaandikishwi ili kuingizwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura (DKWK) la Zanzibar. Wengi wa wanaofika vituoni ni wasiokuwa na kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi.

Kitambulisho hicho kulingana na Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar ya mwaka 1985, ni sharti kwa Mzanzibari anayetaka kuandikishwa kama mpiga kura.

Utoaji wake umekuwa wa kibaguzi: wale wanaostahili hawasajiliwi na kupewa lakini wanaoaminika ni wafuasi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wanapelekewa nyumbani.

Utata mwingine ni taarifa kwamba wapo watu wasiostahili kupiga kura katika uchaguzi wa Zanzibar, unaosimamiwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), wamepatiwa kitambulisho hiki kirahisi kwa nia ya kusaidia CCM.

Yote haya yamekuwa yakikanushwa na serikali na idara yake inayosajili na kutoa kitambulisho hiki kwani wanasema watu 503,895 wamepatiwa kitambulisho Unguja na Pemba kufikia 15 Agosti 2009.

Kwenye vituo vya uandikishaji wapiga kura watu wengi wanafika, lakini idadi kubwa hawana kitambulisho na wanakosa kuandikishwa.

Wananchi wameamua kugomea hii. Sasa wanafika kwa wingi vituoni, lakini wanachofanya ni kuzuia wale wachache waliopewa kitambulisho wasiandikishwe; kwa kuamini wote ni wafuasi wa CCM.

Itakumbukwa kuwa takwimu za uchaguzi uliofanyika mara tatu tangu mwaka 1995, zimeonyesha CCM haijavuka asilimia 10 ya kura zote za kisiwani Pemba. Huku ni ngome isiyotetereka ya Chama cha Wananchi (CUF).

Mara kadhaa CCM wamejaribu kufuta utamaduni huu. Imeshindwa. Lakini haijaacha kupanga na kupangua ndipo mwaka 2003 ilipotangazwa mshindi katika majimbo kadhaa ilhali kura nyingi zilipigwa kwa waliopaswa kuwa wagombea wa CUF.

Huu ndio ule unaokumbukwa hadi leo kama uchaguzi ulioleta matokeo ya ajabu. Ilishuhudiwa wapiga kura wakitia kura zao kwa wagombea waliofutwa kugombea.

Hizi zikaitwa "kura za maruhani." Mgombea wa CCM alitangazwa mshindi kwa kura 400 za ndiyo kwa kuwa zaidi ya 7,000 zilipigwa pasipo mgombea. Bado walibaki CCM ndio washindi.

Uandikishaji wapiga kura unaendeshwa upya Zanzibar katika mfumo tofauti na inavyofanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Tume ya Zanzibar inabadilisha shahada za kupigia kura kwa kile walichosema "zilizopita zimeharibika kwani zilitengenezwa kwa viwango duni."

Walitangaza zamani kwamba wamepata vifaa vya kutengeneza shahada madhubuti zaidi kulingana na teknolojia ya kisasa. Ni lazima kila mpiga kura afike kituo cha uandikishaji. Akishathibitishwa, anapigwa picha na kuandikishwa, ndipo aingizwe kwenye daftari.

Watu wengi wanafika lakini kwa sababu hawana kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi wanakataliwa kuandikishwa. Wapo wale waliotimia umri wa kupiga kura ambao ni miaka 18 ambao hawakuwa wamefikia muda 2005.

Uandikishaji ulianza 6 Agosti lakini ulikwama baada ya wananchi kugomea walichoita "mbinu za kukandamiza haki zao." Waliamua kuzuia uandikishaji na watenmdaji wa Tume wakafungasha virago. Uandikishaji ukasimamishwa.

Baada ya siku 38, Tume imeanza tena uandikishaji. Na kama nilivyosema katika makala ya wiki iliyopita, uandikishaji umeanza kwa mazonge na safari hii ni makubwa zaidi.

Siku ya kwanza tu, Jumamosi, askari wengi wa polisi wameitwa ili kutuliza wananchi waliokasirika kwa kukataliwa haki yao ya kuandikishwa huku wakiona wasiostahili wanaandikishwa.

Wanajipanga na kuzuia wachache waliosaidiwa kupata kitambulisho na kufika vituoni ili kuandikishwa. Kwa hivyo, watu wachache wanaotaka kuandikishwa, hawafiki kwa waandikishaji wa Tume.

Kwenye vituo sasa ni mkabiliano wa wananchi na askari wa dola wakiwemo polisi. Tafakari uonapo raia wasio na silaha yoyote wanakabiliana na askari tena mbele ya Kamanda wa Mkoa (RPC).

Uandikishaji wapiga kura ni zoezi la kiraia linalostahili kutekelezwa kiraia. Hakuna sababu ya makundi ya askari kuwepo vituoni. Ni zoezi la amani na maelewano maana ni sehemu tu ya mlolongo mrefu wa utekelezaji wa haki ya kikatiba ya wananchi.

Mlolongo huo unahitaji kufuatwa kwa mujibu wa sheria na taratibu, lakini pia katika misingi ya haki na usawa. Mwenendo huu ndio stahiki hasa ili kupata uchaguzi huru, wa haki na ulio wazi. Kila mwenye haki anaingia, tena kwa hiari bila shinikizo kutoka kwa mtu au chombo chochote.

Ungetarajia pakiwa na nia njema ya kisiasa, zoezi hili liende bila matatizo. Sivyo. Serikali inasema tatizo ni wananchi kufanya vurugu. Ikaweka ulinzi mkubwa uliojumuisha maelfu ya askari wa vikosi mbalimbali.

Askari wanaokutwa vituoni, wamebeba silaha za moto na wengine wameshika marungu. Uwepo mkubwa wa askari umeshtua hata watazamaji wa kimataifa ambao tayari wapo kazini.

Hawa wamekaririwa na waandishi wa habari walioko Pemba wakisikitika kwa hali mbaya ya usalama waliyoiona vituoni na mitaani. Wameona magari ya deraya yaliyochukua askari wenye silaha na yakipepea bendera nyekundu na kuchomozea silaha zao kwa wananchi.

Lakini hayo yanatokea sasa Unguja katika Mkoa wa Kaskazini ambako uandikishaji pia umeanza 12 Septemba. Makundi ya watu wasiokuwa na kitambulisho hawapati fursa ya kuandikishwa.

Wanakasirika na kuzuia wengine kuandikishwa. Ni hali ya kushangaza kwa sababu hata mara moja viongozi wa CCM hawajalalamikia tatizo la utoaji wa kitambulisho kwa wananchi.

Kwao kila kitu kinakwenda vizuri? Inawezekana ndivyo. Wasingeacha kulalamika. Kidogo walilalamika kuwa Tume imesitisha uandikishaji kwa shinikizo za kisiasa za CUF.

Mkurugenzi wa Idara ya Usajili na Kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi, Mohamed Juma Ame, ametoa changamoto kwa Tume ya Uchaguzi kuwa hata ikifanyaje haitafikia kuandikisha wapiga kura kwa idadi ile waliyotoa vitambulisho ambayo ni 503,895.

Tume wanasema hawajali, kwani wanachokifanya ni kuandikisha watu wanaofika vituoni. Ila wanakiri hata idadi waliyokisia, hawataifikia kwa sababu ya vikwazo vingi.

Wametaja kwamba kitambulisho ni kimoja ya vikwazo. Walisema walipositisha uandikishaji walitoa fursa kwa serikali, vyama vya siasa, asasi za kiraia na wadau wengine kutafakari tatizo hilo na kulipatia ufumbuzi.

Wamerudi kuandikisha wakati tatizo hilo lingali bichi. Isitoshe, limezidi kuzorotesha haki. Sasa masheha wanapokutwa wanazongwa na wananchi watoe fomu za kuombea kitambulisho. Wanatimka.

Sharti la kitambulisho kwa mtu kuandikishwa, linakiuka Katiba ya Zanzibar inayotoa haki kwa kila Mzanzibari kuandikishwa akishathibitisha uhalali wake kwa cheti cha kuzaliwa, pasipoti na shahada ya kupiga kura ya uchaguzi uliopita.

Sasa wananchi wameanzisha harakati – na wanaungwa mkono vizuri na CUF – za kupinga kutumika kwa kitambulisho na kutaka ifuatwe katiba ambayo ndiyo sheria mama.

Kila ninavyotafakari napata picha kuwa uchaguzi wa Oktoba mwakani umeshapangwa. Hakika umepangwa katika namna ya kubakisha CCM madarakani.

Inajulikana fika kuwa mipango hiyo haitatimizwa kirahisi. Inasikitisha kuwa CCM na serikali hawako tayari kuona matakwa yao yanazimwa.

Tatizo zaidi ni kwamba watataka yatimie kwa gharama yoyote. Mabavu yanayotumika yanathibitisha dhamira ya watawala. Wakati mzimu wa kitambulisho unakula haki ya watu, mwingine anasema "ndivyo demokrasia inavyolelewa Tanzania."

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: