Najitoa mapema, sichagui CCM


Nkwazi Mhango's picture

Na Nkwazi Mhango - Imechapwa 25 August 2010

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli

MWAKA huu sitachagua mgombea urais, ubunge au udiwani kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM). Ninazo sababu:

Kwanza, serikali ya chama hiki imeshindwa kukabiliana na ufisadi nchini. Mpaka sasa, serikali imeshindwa kukanusha tuhuma kadhaa za matumizi mabaya ya madaraka, wizi na ufujaji wa mali ya umma.

Kwa mfano, serikali imeshindwa kuwajibisha wakwapuaji wa mabilioni ya shilingi kupitia kampuni ya Richmond Development Company, kutoka Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) na ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT); pamoja na ukwapuaji wa mabilioni ya shilingi unaofanywa na makampuni ya madini.

Ni juzi tu mwanasheria maarufu Mabere Marando alidai EPA ni mradi wa CCM ulioanzishwa kupatia pesa za kumwingiza madarakani Rais Jakaya Kikwete; ambaye si yeye wala chama chake wamekanusha tuhuma hizi.

Na hii si mara ya kwanza tuhuma hizi kutolewa. Hazijawahi kukanushwa. Tuhuma hizi ni nzito na hazisahauliki wala kufichika hata kuziacha zijifie.

Pili, matumizi mabaya ya fedha za umma. Rejea ziara zisizo na faida za rais na mkewe nje na kutoweka wazi majina ya wajumbe wanaoandamana nao.

Pia rejea ununuzi wa magari ya bei mbaya (mashangingi) ambapo inadaiwa serikali inamilki zaidi ya mashangingi 6,000 na kujilipa posho nyingi na kubwa kila siku.

Pia kuna hili la ujenzi wa nyumba za mabilioni za watendaji wa serikali. Rejea majumba ya wakuu wa BoT na TANESCO.

Tatu, matumizi mabaya ya raslimali za umma. Rejea ubinafsishaji wa kifisi, mgao usio wa lazima wa umeme na nchi kukaa kizani kwa mwaka mzima katika karne ya 21; huku wezi wachache wakichota mabilioni kwa kutumia Richmond na serikali ikikaa kimya.

Hapa hujagusa misamaha ya kodi yenye kila harufu ya rushwa.

Nne, viongozi wakuu wa serikali kutotaja mali zao kama wanavyotakiwa na sheria. Je, kama siyo wezi wanaogopa nini? Je, wanatoa picha gani kwa wananchi hasa kuhusiana na uwajibikaji wao? Je, wana mali kiasi gani?

Sababu ya tano ni uzembe: kuibiwa pesa nyingi kwenye wizara na taasisi za umma. Ni juzi tu tuliambiwa kuwa mwaka jana kiasi cha Sh. 1.7 bilioni zilikwapuliwa. Hebu piga picha kwa nchi yenye bajeti ya trilioni 11 na ushei!

Hii maana yake ni kwamba kilichoibiwa kwa mwaka mmoja ni sawa na moja ya tano (1/5) ya bajeti ya taifa ambayo hutegemea wafadhili kwa asilimia 40 ya bajeti yake.

Je, huu ni uzembe kiasi gani? Je, kwa miaka mitano ya utawala wa kisanii zimeibiwa trilioni mamia mangapi? Je, haya ndiyo maisha bora?

Sita, ni kutamalaki kwa rushwa. Rejea yaliyojiri hivi karibuni kwenye uchaguzi wa ndani wa kura za maoni CCM. Hawawezi kukwepa. Tena wamekamatwa na Taasisi yao ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Saba, masimango. CCM na viongozi wake wamekuwa wakitusimanga kuwa watatuletea maisha bora wakati, kimsingi wanaposema maisha bora kwa wote wanamaanisha wao, familia zao, marafiki zao na wawekezaji wa kweli na uongo.

Nane, kutotimiza ahadi nyingi. Mwenyekiti na mgombea wa CCM aliyechangiwa mabilioni alituahidi mambo mengi, hasa pepo. Kuna haja gani ya kumchagua kwa kutulipa jehanamu mahali alipoahidi pepo?

Yako wapi maisha bora kwa Watanzania ukiachia mbali watu wake wa karibu ambao hata wakiiba au kughushi vyeti hawaguswi? Tisa, ni uongo. Hakuna serikali yenye kusema uongo kama ya CCM.

Kila mtu anawahadaa wananchi kuwa ataweka maslahi ya nchi mbele wakati ukweli wanaweka maslahi ya chama na yao binafsi mahali pa maslahi ya taifa.

Na hii ndiyo siri ya mafisadi wa kila aina kutamalaki na kuneemeka chini ya CCM. Bahati nzuri Kikwete aliwahi kusema ana orodha ya majambazi, mafisadi, wala rushwa, wauza mihadarati na wengine wengi.

Amezifanyia nini hizi orodha? Tena ingekuwa afadhali kama angezisoma hadharani, angalau wakaumbuka. Amekaa nazo. Amelinda wahusika.

Kumi, ukosefu wa usalama. Rejea mauaji ya vibaka, vikongwe na watu wenye ulemavu wa ngozi wakati majambazi na mafisadi yakilindwa.

Kumi na moja, kupanua kwa serikali bila sababu. Rejea kuundwa mikoa mitatu na kugawanya baadhi ya wilaya kwa maslahi binafsi ya kisiasa kichama na makada wake.

Tunataka huduma bora si ukubwa wa serikali.

Kumi na mbili, kutosimamia uchumi wa nchi vizuri. Rejea kwa nchi yenye tamalaki ya madini kuwa maskini kuliko hata nchi zilizotoka kwenye majanga jana tena ndogo kama Burundi na Rwanda.

Je, pesa ya raslimali zetu inakwenda wapi na kumnufaisha nani iwapo watu wetu wanazidi kuwa maskini?

Kumi na tatu, utawala mbovu usio na mipango wala ubunifu. Rejea maisha magumu na ukosefu wa mbolea, pembejeo na masoko kwa wakulima na kejeli ya “kilimo kwanza” wakati ni uwekezaji ubinafsishaji na “ufisadi kwanza.”
Kumi na nne, kuua elimu.

Rejea kuwa na matundu mengi yaitwayo madarasa yasiyo na vifaa wala walimu. Sababu za kutochagua CCM ni nyingi.

Kumi na tano, rejea kauli za baadhi ya waliowahi kuwa viongozi wa CCM kwamba chama chao haina mwelekeo na kimetekwa na wafanyabiashara nyemelezi.

Haya yote hayakukanushwa.

Kumi na sita, ni hili la migongano na migawanyiko ndani ya chama na baina ya makundi ya kimaslahi au mitandao. Makundi haya yanakula muda na pesa nyingi za umma kwenye kumalizana badala ya kutatua matatizo ya wananchi yaliyofanya wahusika wachaguliwe.

Kumi na saba, sitaichagua CCM kutokana na kuua demokrasia. Rejea kutokuwapo kwa tume huru ya uchaguzi na kuwepo kwa msajili wa vyama anayetumika kuviminya na kuviua vyama vichanga badala ya kufikiria njia bora za kuweka upenyo kisheria kwa vyama kustawi nje ya masharti na kanuni zenye vibano.

Kumi na nane, kutumia walimu kama maajenti wa uchaguzi wa CCM kwa kanuni ya mapenzi wakati wa shida na karaha na uadui wakati wa neema.

Kumi na tisa, umaskini na maisha duni kwa umma na maisha bora kwa watawala. Rejea kulundikana kwa wagonjwa mahospitalini hadi wanne kulala kitanda kimoja; na wanafunzi miamoja katika darasa moja, huku kikundi cha watu wachache kikiogelea kwenye kila neema ambazo ni mateso ya umma.

Ishirini, uchakachuaji wa haki na hata mafuta. Hili mmeliona kwenye magari ya ikulu na uchaguzi wa CCM. Kila kitu kwa sasa ni kuchakachua!

Niichague CCM kwa lipi? Siichagui.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: