Nakagawa: Waziri wa Japan aliyetia aibu taifa lake kwa ulevi


Zakaria Malangalila's picture

Na Zakaria Malangalila - Imechapwa 06 October 2009

Printer-friendly version
Shoichi Nakagawa

UKWELI wa ujumbe unaosema, 'Fuata ninayosema siyo ninayotenda" hudhihirika mara kwa mara, na kwa mara nyingine umejionyesha katika suala la aliyekuwa waziri wa fedha wa zamani wa Japan, Shoichi Nakagawa aliyekutwa amekufa chumbani mwake mjini Tokyo Jumapili iliyopita.

Nakagawa, alijiuzulu wadhifa wake Februari 17 mwaka huu siku chache baada ya tukio la kuonekana amelewa chakari katika mkutano na waandishi wa habari huko Rome Italia.

Alikuwa mchapa kazi mahiri katika serikali iliyopita ya chama cha Liberal Democratic Party (LDP) kilichoondolewa madarakani 30 Agosti katika uchaguzi mwaka huu baada ya takriban miaka 50 ya kutawala.

Aidha katika uchaguzi huo, Nakagawa alipoteza kiti chake cha ubunge na taarifa za kipolisi zinasema uchunguzi unaendelea iwapo alijiua mwenyewe kutokana na masaibu ya kisiasa yaliyomfika, au ni kifo cha kawaida tu.

Hata hivyo, mwaka 1983 baba yake, Ichiro Nakagawa, alikutwa amekufa katika chumba cha hoteli moja jijini Tokyo na uchunguzi ulionyesha kuwa alijiua.

Kifo cha Nakagawa ni pigo kubwa katika chama chake cha LDP kwani alikuwa ni mmoja wa vigogo katika chama hicho na alikuwa anategemewa sana kukifufua chama hicho baada ya kupoteza uongozi wa nchi.

Aidha viongozi wa chama hicho walikuwa wanatarajia kwamba kama LDP ingeshinda hapo baadaye angeweza hata kumrithi waziri wake mkuu, Taro Aso ambaye ndiyo aliyemteua Septemba 2008 kuwa waziri wa fedha baada ya kuwa ameshika wizara mbali mbali huko nyuma.

Baada ya kushika wizara ya fedha Nakagawa alianza kufanikiwa kufufua uchumi wa Japan ambao ulikuwa umedidimia kwa asilimia 3 baada ya uzalishaji viwandani kuporomoka kwa kasi katika miaka mitano iliyotangulia huku Wajapani wengi wakiachishwa kazi.

Aidha Nakagawa aliunga mkono juhudi za pamoja za Marekani na nchi za Ulaya za kudhibiti mtikisiko wa kifedha duniani.

Hata hivyo, wachunguzi wa mambo ya kisiasa nchini Japan wanasema kwamba pamoja na hali iliyokuwa ikiukabili utawala wa LDP hasa katika kusimamia kwake mtikisiko wa kifedha duniani, matatizo binafsi ya Nakagawa hayakuhesabiwa kama yalikuwa sababu ya kuanguka kwa chama hicho katika uchaguzi.

Matokeo ya uchaguzi yangelibakia pale pale – yaani kushindwa kwa LDP.

Waziri wa fedha wa sasa, Hirohisa Fujii, amesema kuwa Nakagawa aliimudu vyema kazi yake katika wizara ya fedha.

Wawili hao – Nakagawa na Fujii – walikuwa katika chama kimoja cha LDP hadi mwaka 1993 ambapo Fujii alikihama chama hicho na kujiunga na chama cha Democratic Party of Japan (DPJ) ambacho ndicho kinachotawala sasa.

Mara kwa mara alikuwa anawatahadharisha Wajapani kuhusu kuibuka kwa ukuaji wa nchi jirani ya China, kiuchumi na kijeshi, na hasa kijeshi kwamba inahatarisha usalama wa Japan.

Lakini matatizo yake ya ulevi ndiyo yalimuangusha. Katika mkutano na waandishi wa habari mjini Rome Italia Februari 14 mwaka huu, baada ya mkutano wa mawaziri wa fedha wa kundi la nchi za G7, Nakagawa alionekana kalewa chakari, kutokana na jinsi alivyokuwa akiyatamka maneno.

Hakuishia hapo. Baada ya mkutano huo na waandishi wa habari, alisababisha mtafaruku mwingine pale alipokuwa akizuru jumba la makumbusho ya mambo ya kale huko Vatican City ambapo aligusa vitu vya ukumbusho vilivyokuwa ndani ya makasha ya viyoo na kusababisha king’ora kikubwa kulia na watu kukimbia ovyo huku maafisa wa usalama na walinzi wa makumbusho wakitoa silaha tayari kwa lolote.

Mara tu baada ya kutangazwa kwa matukio hayo ya aibu chama cha upinzani nchini Japan (DPJ wakati huo) kilimtaka ajiuzulu mara moja. Inaelezwa kwamba kuna watu walimuona akibugia glasi za mvinyo (wine) katika mgahawa mmoja kabla ya kukutana na waandishi wa habari.

Mkanda wa matukio hayo ulioonyeshwa katika mitandao ya televisheni nchini Japan uliwastua wengi na huenda ndiyo uliongeza kasi ya kuporomoka kwa umaarufu wa chama cha LDP chini ya waziri mkuu Taro Aso.

Hata baada ya wito wa upinzania wa kumtaka ajiuzulu, Nakagawa hakujiuzulu mara moja. Waziri Mkuu Taro Aso alionekana kumuunga mkono na akamtaka aendelee na wadhifa wake wa uwaziri wa fedha.

Lakini baada ya kelele nyingi za kumtaka ag’atuke, hatimaye alikubali kujiuzulu kwa shingo upande, 17 Februari, siku nne baada ya tukio hilo la aibu kutokea.

Katika taarifa yake ya kwa vyombo vya habari na taifa, Nakagawa alikana kuwa alikuwa amelewa, bali alisema alikuwa amekunywa dawa ya kifua na alikuwa mchovu kutokana na safari ya ndege ya masaa marefu.

Mwanasiasa mmoja wa LDP, Suishi Mikiiro alisema kuwa Nakagawa alikuwa amelitia taifa la Japan aibu kubwa mbele ya mataifa duniani.

Wengine, akiwemo waziri mkuu wa zamani wa Japan, Yoshiro Mori alikiambia kituo kimoja cha televisheni cha Japan katika mahojiano kwamba aliwahi kuzungumza na Nakagawa huko nyuma kuhusiana na unywaji wake wa pombe wa kupita kiasi, na limuonya kuhusu tabia hiyo.

Ulevi halikuwa suala pekee lililokuwa linamweka Nakagawa katika mizozo. Aliwahi pia kuzusha zogo kubwa nchini mwake kuhusu masuala ya wanawake.

Mapema mwaka 2007, katika mahojiano na gazeti la Daily Telegraph la Uingereza alisema kuwa wanawake wana sehemu yao wanayostahili kuwepo.

Aliongeza, “Ni vyema wakajionyesha kama wanawake, kwani kwa upande wao wana uwezo fulani ambao lazima wautumie kikamilifu – kama vile ushoni, kupika, kupanga maua sehemu za kupumzikia na maeneo mengine kwa ajili ya kufurahisha wanaume.

Siyo suala la mazuri na mabaya, kwani ni lazima tukubali hali halisi – kwamba kuna tofauti kubwa kati ya wanaume na wanawake,” alisema.

Kauli yake ilifanya vikundi vya wanaharakti vya wanawake vilimjia juu na kumtaka afute kauli hiyo na aombe radhi, kitu ambacho alikifanya baada ya muda mrefu wa malumbano.

0
No votes yet