Namhurumia rais wangu Kikwete


Nyaronyo Kicheere's picture

Na Nyaronyo Kicheere - Imechapwa 30 November 2011

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

WIKI iliyopita ilikuwa mbaya sana kwa rais wangu, Jakaya Mrisho Kikwete, kwa namna alivyoumbuliwa mkutanoni na rafiki yake, Luteni wa Jeshi Mstaafu, Edward Ngoyai Lowassa, ambaye tumeambiwa mara nyingi kuwa hawakukutana barabarani.

Katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama cha Mapinduzi (CCM) uliofanyika Dodoma , Lowassa alipewa dakika saba tu kusema jambo naye akazitumia vilivyo, kwa kifupi na kwa ufasaha.

Nimeambiwa na wale waliokuwapo Dodoma , ndugu zangu wa Mwananchi, kama walivyoripoti katika gazeti lao, kwamba Lowassa alisema:

“Mwenyekiti, kwanza napongeza uamuzi huu wa kurejesha jambo hili katika taratibu za kawaida, lakini napenda kufahamu kwa miezi saba nimetukanwa nikiitwa fisadi, watu wamezunguka nchi nzima kwa fedha za chama wakinitukana, hivi hatukujua kwamba kuna kamati hizo za maadili?

“Mwenyekiti, utakumbuka kwamba mimi nilishaamua kuvunja mkataba wa Richmond mapema, lakini baada ya kukupigia simu ukiwa katika safari ya nje ya nchi ulisema tusubiri (soma ulikataa) kwani ulikuwa umepata ushauri wa makatibu wakuu wa wizara. Sasa leo hii ninahukumiwa na kuitwa fisadi, kwa nini?

“Nilijiuzulu kuwajibika kwa ajili ya kulinda serikali yangu na kwa heshima ya chama changu, sasa kwa nini leo nahukumiwa kwa jambo hili, tena natukanwa na wana CCM wenzangu na siyo wapinzani, nchi nzima, kwamba mimi eti fisadi.

“Mwenyekiti, nikukumbushe mwaka 1997 kule Zanzibar , kina Mzee Daudi Mwakawago walikuja na mafaili yakiwa na tuhuma dhidi ya mtizamo hasi wa jamii dhidi yako. Kwa hiyo, wakati ule kama si busara za akina Mzee (Benjamin) Mkapa leo hii usingekuwa hapo ulipo.”

Toba, hayawi hayawi huwa! Hauchi hauchi hucha! Haya ni maneno ya wahenga kuelezea jambo lolote linalosemwa semwa sana kwamba iko siku jambo hilo litakuja kutokea hadharani. Yamesemwa mengi kuwa Lowassa hayuko peke yake, na wngine wakisema kuna mapatano baina yao . Kweli sasa tumeyasikia from the horse’s mouth. Wajaluo wanasema ‘kasema minyewe’!!

Mwananchi wanasema alipomaliza tu kuongea Lowassa, aliinuka Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, na kukata mzizi wa fitina. Yeye alisema:

“Mwenyekiti, huyu bwana (Lowassa) amesema kwamba amechafuliwa kwa miezi saba, sasa kama leo tunasema kwamba tunarudi kwenye utaratibu wa kamati za maadili, hao waliomchafua watafanywaje?”

Cha kushangaza, au cha kusikitisha kwa upande wa Kikwete ni kwamba wakati wote, kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi, Lowassa na Sumaye wakizungumza, mtu mmoja mnene mfupi mwenye kipara aitwaye Mkapa alikuwa akifurahia na kushangilia! Yaani anashabikia mtu kupewa vipande vyake.

Magazeti mengine yalielezea hali hii kuwa “Lowassa amkaanga Kikwete.” Hayo ni ya wiki iliyopita ambapo Kikwete aliumbuka pale ilipodhihirika dhahiri shahiri kuwa Lowassa hakuwa peke yake katika Richmond iliyopewa jina wakati ule la Richmonduli.

Kabla haya ya Richmond na haya ya John Chiligati na Nape Nnauye kuzunguka nchi nzima wakimtukana Lowassa hayakwisha yamezuka mengine ya Bunge kuipa kibali kamati ndogo ya Bunge ya Maliasili na Utalii kufanya uchunguzi kuhusu utoroshaji wa wanyamapori kwenda nje ya nchi.

Miongoni mwa hadidu za rejea za kamati hii ni kuchunguza uhalali wa twiga kukamatwa wakiwa hai kisha kusafirishwa kwenda nje ya nchi na uadilifu wa watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii wanaofanya kazi katika sekta ndogo ya wanyamapori.

Hapa ndipo ninapojiuliza kuwa, je hili la utoroshaji wa wanyamapori litamponya rais wetu? Nasema haya kwa sababu nimesikia kuwa miongoni mwa watoroshaji wanyama wetu ni wageni wenye vibali vya watu wakubwa sana nchini.

Mie najiuliza kuwa watumishi wa sekta ndogo ya wanyapori watahimili vishindo vya kamati ndogo ya Bunge wakatae kutaja wakubwa wanaotoa vibali vya kukamata wanyama hai? Watakubali kweli kupata lawama kama aliyoipata Lowassa kwa niaba ya marafiki zake, serikali na chama tawala?

Kwa wale waliowahi kuwa maaskari jeshini kama mimi, watakuwa wanafahamu yafutayo: Kwanza kwamba kuna kitu kinaitwa SITREP jeshini, polisi, magereza na hata usalama wa taifa wakati ule tulipokuwa na usalama wa taifa (mimi nakubaliana na CHADEMA kuwa sasa tunao usalama wa CCM na siyo usalama wa taifa).

Pili kwamba SITREP ni kifupi cha Situation Report. Kinachotokea ni kwamba asubuhi sana au alfajiri kila kituo cha polisi hutoa taarifa ya matukio kituoni kwa Kamanda wa Polisi wa Wilaya (OCD), hii hufuatiwa na kila OCD kutoa taarifa ya hali ilivyo wilayani kwake kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC).

Kwa maana hii, mpaka saa mbili asubuhi au saa tatu hivi, kila RPC nchini anakuwa na taarifa ya hali ya usalama mkoani kwake, naye huituma kwa IGP. Kwa mantiki hii IGP anakuwa na taarifa ya hali ya usalama katika mikoa yote na kuifikisha ikulu kabla ya saa nne asubuhi.

Kwa upande wa Magereza hali na mlolongo ni huo huo ambapo kila gereza hutoa taarifa wilayani na wilaya kutoa taarifa mkoani kabla ya kila mkoa kutoa taarifa makao makuu ya magereza kwa kamishna wa magereza kabla ya saa nne ripoti inapofikishwa kunakohusika.

Jeshini nako mambo ni hayo hayo. Kila detach hutoa taarifa kikosini hali ikoje asubuhi ile. Kila kikosi hutoa taarifa kwa brigedi na kila brigedi hutoa taarifa kwa kamandi na kila kamandi hutoa taarifa kwa Mkuu wa Majeshi (CDF) ambaye naye huifikisha taarifa hiyo kunakohusika.

Hali ni hiyo hiyo kwa idara za usalama; ile ya taifa na ile ya Jeshi. Wakati taarifa za usalama wa taifa hufika kwa Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, ile ya jeshi hufika kwa Mkuu wa Usalama Jeshini (CMI) ambao huzifikisha taarifa hizo kunakohusika.

Kwa maana hii, inapofika saa fulani iliyokubaliwa, Mkuu wa Nchi, huwa na taarifa zote nchini na wakubwa wengine wote huwa wanafahamu kuna matukio gani makubwa nchini. Ndipo hapo sasa ninapouliza:

Iliwezekanaje ndege kuuubwa ya Jeshi la Falme za Nchi za Kiarabu kuingia nchini, kutua KIA na kubeba twiga bila wakubwa hawa kufahamu?

Kwanza ndege ya kijeshi kutoka nje ya nchi, yaweza kuingia nchini bila IGP kujua, bila CMI kujua, bila CDF kujua, bila Waziri wa Mambo ya Ndani kujua, bila Waziri wa Mambo ya nje kujua na bila Rais kujua? Mimi siamini na kamati ya Shah itavumbua mengi, tusubiri.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: