Nani ameibua mgomo wa mabasi Moshi?


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 18 July 2012

Printer-friendly version
Uchambuzi
Stendi ya mabasi Moshi

ALUU Segamba, katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Moshi Mjini, amekana kile ambacho wengi wameita hujuma kwa wananchi wanaotumia usafiri wa mabasi katika manispaa ya Moshi.

Aliliambia gazeti hili juzi Jumatatu, kuwa hahusiki katika kuandaa na kusimamia mgomo wa wenye mabasi jijini humo.

Segamba alikuwa akijibu tuhuma zilizohusishwa na barua moja iliyoonyesha kuwa inatoka ofisini kwake na imesainiwa na yeye, ikielekeza jinsi ya kufanya mgomo wa wenye mabasi ya abiria manispaa ya Moshi.

Mgomo huo umeelezwa kuwa wa kupinga ongezeko la ushuru wa mabasi madogo ya abiria kutoka Sh. 1,000 hadi 1,500 lililotangazwa na halmashauri ya manispaa inayoongozwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Barua ambayo Segamba anakana inaonyesha kuandikwa tarehe 8 Julai. Ina kichwa cha habari: Mgomo wa Usafirishaji abiria kuanzia tarehe 9/7/2012.

Barua inakumbusha juu ya kikao kinachodaiwa kufanyika tarehe 7 Julai katika ofisi za CCM wilaya “ikiwa mwendelezo wa kupinga ushuru wa mabasi madogo kutoka Sh. 1,000 hadi Sh. 1,500.”

Kwa mujibu wa mwandishi wa barua hiyo, Kumb. Na. CCM/MOS/VOL 102/FOLIO 230/2011,kuna maeneo manne muhimu kama ifuatavyo:

Kwanza, kwamba kuanzia siku ya Jumatatu tarehe 9/07/2012 kusimamisha shughuli zote za usafirishaji wa abiria hadi halmashauri watakapokoma kupanga ushuru kama wanavyotaka wenyewe.

Pili, kwamba chama kitatumia safu yake ya upambanaji kuandaa kikundi cha vijana wa Green Guard ili kuhakikisha kinafanya fujo zenye lengo la kuishinikza halmashauri irejee maamuzi yake.

Tatu, kwamba chama kitahakikisha wote watakaoshiriki katika mgomo watalindwa dhidi ya mkono wa sheria. Hakuna hata mmoja atakayekamatwa na kushitakiwa katika operesheni yetu hii, hata kama atakuwa amesababisha maafa, na

Nne, kwamba ili kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa ufanisi, chama kitatoa fedha taslimu Sh. 30,000 kwa kila mshiriki. Barua hii imesaini na Alu Sigamba, Katibu (W).

Lakini katibu wa wilaya alipopigiwa simu na gazeti hili juu ya suala hilo, alijibu kwa sauti ya upole kuwa kinachoitwa barua ya CCM ni feki.

Alipoanza kusomewa barua hiyo, alijibu haraka, “Nimeona barua hiyo. Ni feki. Si barua yetu. Haijaandikwa na CCM Wilaya ya Moshi.”

Alisema nembo ya CCM iliyotumika “imechakachuliwa kwa kuwa haifanani na nembo ambazo chama hicho kinatumia na imetofautiana na barua ambazo wilaya hiyo huandika.”

Alisema hata namba ya kumbukumbu ya barua hiyo ni ndefu ikilinganishwa na kumbukumbu za barua zao wilayani. Alisema kibaya zaidi ni kwamba hata jina la aliyesaini barua siyo lake.

Alisema aliyesaini barua ni Alu Sigamba wakati yeye ni Aluu Ismail Segamba.

Barua hiyo inanakiliwa kwa mkuu wa mkoa, usalama wa taifa na Mhe. Nape Nnauye. Lakini Segamba amekana utaratibu wa chama chake kupeleka nakala za mawasiliano yao kwa wakuu wa wilaya au mkoa, au usalama wa taifa.

Hata hivyo, alipoongea na gazeti hili Jumatano jioni, Segamba alikiri kuwa mgomo ulikuwa unaendelea.

Alipoulizwa kuwa mgomo huo ulikuwa unahusisha ubebaji bendera za CCM, alisema haraka kuwa anaona kuna bendera za CHADEMA pia.

Kugomewa ushuru mpya wa mabasi, maana yake ni kudhoofisha CHADEMA inayoongoza manispaa ya Moshi Mjini. Lakini wachunguzi wa siasa za Moshi na Arusha wanasema, kinachofanyika kilitabiriwa zamani.

Wanasema CCM inataka kuhujumu uongozi wa CHADEMA na kudai kuwa kama CCM wanataka ushuru upungue, mbona hawajateremsha bei za bidhaa mbalimbali katika bajeti inayoendelea kujadiliwa.

Hata hivyo, kuna hoja zinazohitaji majibu katika jambo hili. Kwa mfano, waraka umedai kuwepo makundi ya kigaidi dhidi ya “wapinzani wa serikali.”

Katika hili CCM inalazimika kutoka mbele na kulitolea majibu muwafaka. Ikilinyamazia inaweza kueleweka hivyohivyo.

Kuna suala la matatizo ya usafiri. Mengi ya haya yamesababishwa na sera mbovu za umilikishaji wa kila sekta ya umma kwa watu binafsi iliyoasisiwa na kusimamiwa na CCM na serikali yake.

Lakini hata maeneo mengine yaliyotajwa kupelekewa waraka ambao katibu anakana, hayana budi kijitokeza na kutoa maelezo; vinginevyo wananchi hawatayaelewa.

Kuna wanaouliza je, barua hii haiwezi kuandikwa na CHADEMA ili kuchafua CCM? Lakini kuna wenye magari ambao ni wanachama wa vyama vyote na wamo kwenye mgomo. Wananufaikaje na mgomo huu au wanafaidikaje na kiwango cha chini cha ushuru?

Lakini pia kuna mambo ambayo hayapaswi kupuuzwa. Kwamba kuna vikosi vya kudhibiti wapinzani, hata kama siyo Moshi, hilo limesikika sehemu kubwa nchini na hata Zanzibar ambapo wana-CCM wanajigamba kwa kuwa na kikosi cha Janja Weed.

Kikosi hiki kimekuwa kikitishia shughuli za Chama cha Wananchi (CUF).

Kuna wanaouliza pia je, CCM hawawezi kuandika barua hiyo na kukosea majina na namba za kumbukumbu kwa makusudi “lakini ujumbe ukawa umefika, potelea mbali?”

Panahitajika umakini katika kuchambua mazingira haya, hasa panapokuwa na ushindani mkubwa wa vyama viwili; huku kile kilichoko ikulu kikiwa na nyenzo kuu za kuzima na, au kuzimua.

0
No votes yet