Nani amelisha Chiligati milungi?


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 10 March 2010

Printer-friendly version
Tafakuri
Katibu wa Itikadi na Uendezi wa CCM, John Chiligati

WAINGEREZA walikuwa wa kwanza kuingia katika mapinduzi ya viwanda, lakini baada ya kuonja tamu ya viwanda wakabweteka; walikaa hapo hapo hawakutaka kuumiza tena vichwa zaidi. Kuendelea kukaa hivyo kulitokana na kiburi cha kudhani kwamba wamefika na kwa maana hiyo hakuna wa kuwafanya lolote.

Ukubwa na nguvu za taifa hili zilikuwa kubwa kiasi cha kuelezwa kwamba jua halikuzama kwenye dola ya Waingereza kwa sababu walikuwa wanatawala dunia, kuanzia jua likochomoza hadi linakozama na kuchomoza kwingine, kunzia mashariki hadi magharibi; kuanzia kusini hadi kaskazini.

Hata hivyo, Uingereza pamoja na kwamba hadi leo ingalia taifa lenye nguvu na linaloheshimika duniani, haijashililia nafasi yake ya kwanza.

Leo hii dunia kiuchumi inaongozwa na mataifa ya viwanda tajiri manane kwa maana ya Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan, Marekani, Canada, Rassia na Uingereza wenyewe.

Zile zama za jua kutokutua kwenye dola ya Uingereza kwa sasa hazipo tena, lakini kama haitoshi bado kuna mataifa mengine yanafukuzia hayo hapo juu, yaani Brazil, China, India, Mexico na Afrika Kusini.

Mataifa haya yanatajwa kuwa ni nchi zinazoendelea lakini hadhi yake ikionyesha wazi kwamba baada ya miaka michache ijayo, mfumo wa G8 ni lazima ubadilike.

Si nia ya uchambuzi huu kuelezea mifumo na nguvu za kiuchumi za mataifa tajiri, ila ni kuonyeha kwamba hakuna kitu ambacho ni cha kudumu katika mfumo wa maisha ya wanadamu.

Lakini inakuwa ni mbaya zaidi pale inapotokea kwamba mafaniko fulani yakifikiwa, basi watu kukaa na kubweteka na kudhani kwamba hali itakuwa hivyo miaka yote. Huko ni kujidanganya kwa hali ya juu.

Wiki iliyopita vyombo vya habari viliripoti utafiti uliofanywa nchini juu ya rushwa, na ikawekwa wazi kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinaongoza kwa ugonjwa huo hasa kwenye uchaguzi.

Kwa bahati nzuri ripoti ya utafiti huu ilitolewa siku chache tu baada ya rais Jakaya Kikwete binafsi kueleza jinsi rushwa inavyotumika kununua nafasi za uongozi.

Akifungua mkutano wa mwaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Mwanza, Rais Kikwete alitoa wito kwa Takukuru kudhibiti wote wanaonunua kura na wanaouza kura hasa kwenye ngazi ya kura za maoni. Rais alirudia kauli hiyo kwenye hotuba yake kwa taifa ya mwisho wa Februari.

Wakati Rais akieleza hali hii na kubainisha hofu yake kwamba uchaguzi wa kununua kura unaweza kumfikisha mwendawazimu ikulu, na kwa maana hiyo ni lazima juhudi za makusudi kuidhibiti hatari hiyo hasa katika uchaguzi wa mwaka huu zichukuliwe, Katibu wa Itikadi na Uendezi wa CCM, John Chiligati, anaonekana kuwa katika ulevi mkubwa kuhusu hali hiyo.

Chiligati wiki iliyopita aliulizwa maoni yake juu ya habari kwamba CCM ni baba wa rushwa katika uchaguzi; katika majibu yake ya kushangaza kabisa alisema rushwa katika uchaguzi si habari. Alifika mbali zaidi akisema kwamba ni vigumu kuondoa rushwa kwenye uchaguzi.

Chiligati kwa majibu yake anaonyesha wazi kama mtu asiyekuwa na hofu na ugonjwa huu. Hana hofu kwa sababu CCM ni chama tawala, kimejiimarisha kipo mdarakani na kinatawala. Kipo na kitaendelea kuwepo.

Changamoto ya rushwa kwake haimnyimi usingizi, hasumbukii matatizo hayo kwa sababu anajua kwamba rushwa ipo. Hiyo si habari ya kumsumbua kwa sababu angeambiwa kwamba rushwa itaingoa CCM madarakani labda angeshtuka kidogo, lakini hilo halipo. Chiligati wa watu kajibwetekea.

Ni kama ilivyokuwa Uingereza ambayo baada ya kufanya mapinduzi ya viwanda, hawakujishughulisha na changamoto mpya; kama ni kwa jinsi gani watabakia kuwa namba moja kwa viwanda duniani ili wasipitwe.

Hawakujali walibweteka na leo tunawaona wananusanusa nafasi ya saba duniani kwa maana ya nguvu za viwanda na uchumi kwa ujumla.

Chiligati anaweza kuwa katika ulevi unaotokana na ukubwa wa CCM, wingi wa wanachama, wingi wa wabunge, madiwani, wenyeviti wa mitaa na vitongozi, fungu kubwa la ruzuku na pengine hata kuwa chama tawala. Kwake anaona ni kama haki na wajibu wa CCM.

Hakosi usingizi kwa sababu ya habari kama za rushwa ndani ya chama hicho na kwa maana hiyo hawezi kukosa usingizi kwa sababu ya kero na shida za kweli za wananchi ambazo hazishughulikiwi kwa sababu ya watu kununua uongozi.

Chiligati anaamini kwamba jua halitui kwenye dola ya CCM.

Kwa kiongozi kama Chiligati alipaswa kusikitishwa kikwelikweli na taarifa za CCM kuongoza kwa rushwa, kwa sababu maana ya matokeo hayo kwake na kwa chama chake ni kwamba ni vigumu mno kuongoza kwa rushwa halafu ukawa na ubavu wa kuitokomeza.

Alichotuonyesha Chiligati ni kitu kimoja, kwamba CCM haishutushwi na rushwa, na kwamba ni sehemu ya utamaduni wake, ni jadi yake ni mfumo wake ndiyo njia ya kujipatia ushindi wa kishindo katika chaguzi zote.

Hata hivyo, kauli ya Chiligati ni faida kwa umma, kwamba muda CCM idumupo madarakani rushwa si kitu cha kuisumbua, itakuwepo na itaendelea kuwepo.

Chiligati anaamini CCM ipo kwa sababu ni haki yake kutawala, itaendelea kubakia madarakani kama vile Waingereza walivyoamini kwamba kwao hakuna machweo. Waliposhtuka walishangaa kujikuta wakipitwa na mataifa madogo kama Japan ambayo yalipata kukaliwa kwa mabavu kijeshi na Marekani na kuwa kwenye hofu ya kukaliwa na China wakati wote.

Kama jeuri ya Chiligati ya kutokutishwa na kiwango cha rushwa ndani ya CCM ni jeuri ya nguvu ya chama tawala, basi salamu zangu ni nyepesi tu kuwa ngoma ikivuma sana inakaribia ukingoni.

Nasikitika kusema kwamba inavyoonekana Chiligati ni mlevi wa madaraka. Amelewa nguvu za kutawala na sasa anaamini ni halali kwa kila kifanyikacho.

Anadhani jua halitazama kwenye himaya ya CCM, itaendelea kuwa chama tawala hata kama kimejitumbukiza kwenye tope zito. Pole Chiligati kwa ulevi wa madaraka.

0
No votes yet