Nani amelonga taifa hili?


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 19 May 2010

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki
Rais mstaafu, Benjamin Mkapa

MWAKA mmoja uliopita, Tanzania ilikuwa nchi ya tatu barani Afrika kwa kuzalisha kiasi kikubwa cha dhahabu.

Mbele yake, zilikuwapo nchi mbili tu; Afrika Kusini na Ghana ambazo zilikuwa zimeanza uchimbaji mkubwa wa dhahabu miaka 100 iliyopita.

Maana ya takwimu hizo ni kwamba katika eneo zima la Afrika Mashariki, Tanzania ndiyo kinara pekee wa kuzalisha dhahabu na madini mengine.

Hata hivyo, wiki iliyopita serikali ya Uganda imetangaza kujenga kiwanda cha kusafisha dhahabu na madini mengine kwa thamani ya zaidi kidogo ya Sh. 2 bilioni.

Nchi hiyo ambayo haipo hata katika orodha ya nchi 20 zinazozalisha dhahabu kwa wingi katika bara la Afrika, imefanikiwa kujenga kiwanda hicho, wakati utawala wetu umeshindwa kufanya hivyo.

Na serikali ya Uganda imetangaza hadharani kwamba soko kubwa la kiwanda hicho litakuwa ni nchi za Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Hii ni kwa sababu wanajua hawana dhahabu (walau kwa sasa).

Kiwango cha fedha kilichotumika kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda hicho ni kidogo mno. Ni kidogo kiasi kwamba nina amini hata mfanyabiashara maarufu nchini, Said Salim Bakhressa anaweza kujenga kiwanda hicho.

Sembuse serikali? Serikali ambayo mmoja wa watumishi wake amewahi kukiri kumiliki zaidi kidogo ya Sh. 1 bilioni kutoka katika miongoni mwa akaunti zake?

Kwa maoni yangu, hii ni aibu ya mwaka kwa serikali yetu. Ninafahamu kwamba kiwanda cha Mwananchi Gold kilijengwa kwa madhumuni haya, lakini sasa ni kama kimefilisika.

Nchi kama Uganda haina sababu yoyote ya kuwa mshindani wa Tanzania katika uchumi kwa namna yoyote ile.

Tanzania ina ardhi kubwa yenye rutuba kuliko Uganda. Tanzania ina idadi kubwa ya watu kuliko Uganda. Tanzania ina bahari na maziwa mengi kuliko Uganda. Kubwa zaidi Tanzania imefaidi amani kuliko Uganda.

Na hili si jambo la kujisifia kwa baadhi ya watu lakini Waganda tuliwatwanga kwenye vita mwaka 1979. Kwa namna yoyote ile, hii ni nchi ambayo tulitakiwa kuwa mbele yake kwa kila kitu.

Lakini inaonekana wako mbele yetu tayari. Wanafanya mambo ambayo Tanzania ilitakiwa kuwa imeyafanya miaka kumi iliyopita wakati tulipoanza kuzalisha dhahabu kwa wingi.

Cha kusikitisha si katika eneo hilo pekee ambapo Waganda wanaonekana kuanza kuwa juu yetu. Hata kwenye sekta ya nishati wanaonekana wana akili kutuzidi.

Serikali ya Rais Yoweri Museveni, iliamua kupeleka wanafunzi wa kiganda nje ya nchi hiyo kwa ajili ya mafunzo maalumu kuhusu sekta ya mafuta na nishati.

Museveni aliamua hivyo baada ya kupata taarifa za kuwapo kwa uwezekano wa kuanza kuchimbwa kwa mafuta katika nchi hiyo.

Alitaka Waganda washiriki katika utafutaji na uchimbaji wa mafuta. Wajue nini hufanyika wakati wa utafutaji na uchimbaji. Alitaka wananchi wake wawepo katika kila hatua.

Dhumuni lingine kubwa la mafunzo hayo kwa Waganda lilikuwa ni kuwafanya wajue nchi zilizofanikiwa katika sekta hiyo zilifanya yapi mazuri na zile zilizoshiba migogoro zilifanya yapi mabaya.

Kama unanifuatilia vizuri, utaona lengo la kiongozi huyo lilikuwa ni kuhakikisha nchi yake haifanyi makosa yaliyofanywa na nchi nyingine. Anataka nchi yake ifaidike.

Njoo Tanzania ujionee tofauti. Tuliingia kwenye uchimbaji mkubwa wa madini mwishoni mwa miaka ya 1990 bila ya kujiandaa.

Tukawaacha wazungu waje kutafuta na kuchimba madini. Watuambie wao wamepata nini na watalipa kodi kiasi gani. Na sisi kazi yetu ikawa kusema hewala.

Hebu fikiria, yaani mtu anakuja kwako anajifungia mwenyewe kutafuta mali na halafu unamuacha yeye akuambie amepata nini? Hivi tuna akili kweli?

Tukawapa fursa wawekezaji kuleta wafanyakazi kutoka kwao kwa vile hapa kwetu hapakuwa na kada ya wafanyakazi wenye elimu na upeo katika mambo ya madini.

Mara baada ya migodi kuja na uchimbaji kuanza, ndipo serikali ikaamua kuweka mkazo vyuoni kutoa wahitimu katika mambo ya madini.

Cha kusikitisha ni kwamba, kwa mujibu wa takwimu za mwaka huu, Tanzania sasa ni ya nne kwa uzalishaji wa dhahabu barani Afrika. Nchi ya Mali sasa imechukua nafasi ya tatu na kutupiga kikumbo.

Kwa tafsiri nyingine, dhahabu ya Tanzania imeanza kupungua. Miaka kumi ijayo wakati tutakapokuwa na wasomi wa kutosha, watakwenda kuona mashimo tu kama ilivyo kwa eneo la Buhemba mkoani Mara.

Kwa taarifa ya msomaji wa makala hii, utafutaji na uchimbaji wa madini ya Uranium hapa Tanzania ulianza hata kabla serikali haijatengeneza sera ya uchimbaji huo.

Maana yake ni kwamba makampuni ya wawekezaji yaliyokuja kwa ajili ya kazi hiyo yaliachwa sawa na mbuzi aliyekata kamba na kuzurura alivyotaka.

Wangeweza kusema hawajagundua kama kuna madini wakati yapo. Wangeweza kusema madini yapo lakini hawajaanza kuvuna kumbe wakivuna. Wangeweza kusema lolote walilolitaka, na sisi tungebaki kusema hewala.

Ninaumia sana moyoni mwangu kuona viongozi wa nchi yetu wakifanya mambo kama waliyofanya akina Chifu Mangungo. Wakifanya hivi wakati baadhi yao walikwenda shule katika nchi za wazungu na kupata alama za juu.

Na tafiti zimeonyesha kwamba hakuna tofauti yoyote ya kiakili kati ya wazungu na sisi. Tunafikiri sawa. Inakuaje tunaongozwa na viongozi ambao hawajali kabisa mustakabali wa taifa letu?

Kulikuwa na sababu gani ya kuruhusu uchimbaji mkubwa wa madini wakati nchi haina wataalamu wazalendo wa kutosha?

Tulikuwa na shida gani ambayo ilitufanya tuharakishe kuchimba madini ambayo sasa imekwisha? Mbona wananchi wetu wamekuwa masikini zaidi, hususani wale wanaoishi katika maeneno ya migodi kuliko ilivyokuwa kabla wawekezaji hawajaja?

Kuna faida gani ya kuwashinda Waganda katika vita ya silaha halafu watushinde katika vita ya uchumi? Jamani, hata Uganda? Hii ni fedheha kwa nchi yetu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: