Nani ametuma Tendwa kusemea ikulu?


Benson Msemwa's picture

Na Benson Msemwa - Imechapwa 26 May 2010

Printer-friendly version
Mtazamo

JOHN Tendwa ni Msajili wa Vyama vya Siasa, lakini anajitumikisha kama msemaji wa ikulu ya Rais Jakaya Kikwete.

Wiki iliyopita Tendwa alijipa jukumu la kuwaambia waandishi wa habari kuwa aliyosema rais yalikuwa “utani” na akawataka waandishi kutangaza kuwa Watanzania “wajifunze kuvumilia utani.”

Vyombo vya habari vilimnukuu Rais Kikwete wiki iliyopita akisema kuwa matumizi ya “takrima” katika uchaguzi hayakwepeki.

Alikuwa amemaliza kuongea na viongozi wa madhehebu ya dini jijini Dar es Salaam walikokuwa wakielezwa sheria ya kudhibiti rushwa katika uchaguzi.

Vyombo vya habari vilipoamka na kauli ya rais na kufuatiza maoni ya wananchi wakilalamika na kumshangaa rais kwa kupingana na maamuzi ya mahakama iliyofuta sheria kuhusu takrima, ndipo Tendwa aliona wasemaji wa ikulu hawatoshi na hawafai.

Tendwa alijitosa kumtetea rais akisema kwa kauli hiyo, rais alikuwa akitania na kwamba wananchi wajifunze kuvumilia utani. Ni lini rais anafanya utani na lini anakuwa dhati?

Tendwa anataka kuwasadikisha wananchi kuwa rais aliwakusanya viongozi wa dini, kutoka kote nchini, ili awatanie?

Isije ikawa Tendwa anafanya utani kuhusu anachoita utani wa rais juu ya masuala makubwa ya nchi. Siyo rahisi kuamini anayosema Tendwa lakini kuna kila sababu ya kujenga mashaka.

Je, kauli za rais kuhusu maisha bora kwa kila Mtanzania ni utani? Kesi za EPA zilizopo mahakamani ni utani? Mbiu zote kuhusu “Kilimo Kwanza” ni utani; Kamati ya Madini ya Bomani ni utani na kauli kwamba wafanyakazi watakaogoma watafukuzwa kazi, wote ni utani?

Tendwa ana maana gani juu ya kauli za rais? Kwa nini anataka kumharibia rais? Kwa kauli ya Tendwa, tamko la rais kuwa serikali haiwezi kulipa kima cha chini cha Sh. 315,000 kwa mwezi, ni utani.

Hivyo kampeni ya “Malaria haikubaliki” ni utani; ahadi ya kushughulikia kero ya usafiri kwa wanafunzi Dar es Salaam ni utani; ujenzi wa shule za kata ni utani;
kusimamia sheria ya gharama za uchaguzi ni utani; na kushughulikia kero za Muungano ni utani.

Tendwa anatulazimisha tuamini kuwa hata kauli ya Rais kutetea kiti chake katika uchaguzi mkuu ujao ni utani; ilani ya chama chake ya uchaguzi ni utani na kauli za ufumbuzi wa mgogoro wa kisiasa Zanzibar ni utani.

Tendwa ana uzoefu gani wa Rais Kikwete kusema hili wakati anasema lile; kwamba anachosema sicho kwa kuwa ni utani mtupu? Lakini amesema. Ikulu haijakanusha wala kumkemea.

Yawezekana kwamba kamati ya Mzee Ali Hassan Mwinyi kutafuta chanzo cha migogoro ya ndani ya CCM ni utani? Ahadi ya kupunguza matumizi, hasa ununuzi wa magari ya kifahari na upunguzaji semina elekezi za aina ya Ngurudoto; vyote ni utani mtupu?

Kama hivyo ndivyo, na Tendwa alitaka wananchi waamini hivyo na kujifunza kuzoea utani, basi kushindwa kwa serikali kutoa mikopo kwa uwiano sawa kwa wanafunzi wote wa elimu ya juu ndio utani babukubwa.

Kwa hiyo inawezekana nami nikachukuliwa kuwa ninatania kwa kuandika yote haya? Kwamba nichukue kinga ileile na kwamba mnizoee?

Tendwa amekwaza wananchi. Rais angemshushua kwa kutamka wazi kwamba hakuwa anatania. Lakini atakubali kufanya hivyo? Je, kama alikuwa anatania kweli?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: