Nani amewaachia wauaji wa Kombe?


Prof. Abdallah Saffari's picture

Na Prof. Abdallah ... - Imechapwa 19 October 2011

Printer-friendly version

UTAWALA wa Rais Jakaya Kikwete umekana na umekataa kuhusishwa na kuachiwa huru kwa askari wawili wa jeshi la polisi waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa, Koplo Juma Mswa na Konstebo Mataba Matiku.

Askari hao walihukumiwa kunyongwa na mahakama kuu ya Jamhuri mwaka 1998 baada ya kupatikana na hatia ya kumuua kwa makusudi, Luteni Jenerali Imran Kombe. Hukumu hiyo ilithibitishwa na Mahakama ya Rufaa ya Tanzania, takriban miaka 16 iliyopita.

Ushahidi uliotolewa katika kesi ile ulithibitisha kwamba askari hao walimpiga risasi nne kifuani Jenerali Kombe huku akiwa ameinua mikono juu kuonyesha kuridhia kukamatwa na askari hao.

Wao walidai eti walifikiri Jenerali Kombe ni jambazi sugu wa wizi wa magari!

Halafu ndipo inadaiwa walipunguziwa adhabu ya kifo, kwenda kifungo cha maisha na baadaye hadi kifungo cha miaka miaka miwili gerezani.

Ieleweke kwamba Jenerali Kombe hakuwa mtu mdogo kimadaraka nchini. Na kwa vile alikuwa amestaafu miaka michache tu nyuma, polisi hao lazima walikuwa wanamfahamu.

Alikuwa mmoja wa majemedari mashuhuri waliojizolea sifa kwa kuitetea nchi hii katika vita vya Kagera mwaka 1978. Alikuwa pamoja na Luteni Jenerali Silas Mayunga, Kanali Salim Hassan, Brigedia John Walden na wengineo.

Baada ya vita hivyo kumalizika, rais wa wakati huo, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alimteua Jenerali Kombe kuwa mkurugenzi mkuu wa usalama wa taifa nchini – moja ya asasi nyeti na muhimu kwenye uongozi wa nchi.  Alibaki na wadhifa huo mpaka alipostaafu.

Hivyo mazingira ya kuuawa kwake yalileta simanzi na tuhuma nyingi kwamba aliuawa kwa maagizo ya serikali iliyokuwa madarakani wakati huo ikiongozwa na Benjamin Mkapa. Kwa hiyo, taarifa ya kuachiwa huru kwa wauaji hawa imezusha upya hasira ya wapenda haki nchini na duniani kote.

Swali lililopo ni nani aliamuru wahalifu hawa wakubwa kuachiwa  huru na kwa nini?  Kwa vile Rais Kikwete amekana kutoa msamaha wa kuachiwa kwa wahalifu hawa, ni muhimu Rais mstaafu Mkapa atoe ufafanuzi kuhusu kadhia hii.

Angeweza kufanya mambo mawili. Kwanza, angeweza kukana kuhusika na kutoa msamaha huu. Kama ni hivyo, kuachiwa kwa askari hawa kulifanywa kinyume na katiba na sheria, hivyo wasakwe na warejeshwe gerezani kutumikia adhabu yao ya kunyongwa mpaka wafe.

Pili, angeweza kukiri kutoa msamaha kwa wahalifu kwa mamlaka aliyopewa kwa mujibu wa ibara ya  45 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kama ilivyorekebishwa mara kwa mara.

Sehemu ya ibara hiyo 45(1) inasema, “Bila ya kuathiri masharti mengineyo yaliyomo katika ibara hii, rais anaweza kutenda lolote kati ya mambo yafuatayo:

Kutoa msamaha kwa mtu yeyote aliyepatikana na hatia mbele ya Mahakama  kwa kosa lolote, na anaweza kutoa msamaha huo ama bila ya  masharti au kwa masharti, kwa mujibu wa sheria.”

Maneno kwa mujibu wa sheria yana maana kuwa msamaha wa rais sharti uwe na sababu za msingi kwa mazingira ya Tanzania kuepuka dalili za upendeleo au ubaguzi katika kutoa msamaha huo jambo ambalo ni kinyume na ibara ya 13 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

Ibara hiyo inasema, “Watu wote ni sawa mbele ya sheria, na wanayo haki bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria.”

Kwa kawaida wafungwa wote waliopatikana na hatia ya mauaji ya kukusudia ama hunyongwa au  adhabu yao  hiyo hupunguzwa na kutumikia kifungo cha maisha.  Magereza ya nchi hii yana wafungwa ambao wametumikia kifungo cha maisha kwa zaidi ya miaka arobaini na kuendelea.  Kwa kawaida hufia na kuzikwa gerezani.

Hata wale wanaotetea kuondolewa kwa adhabu ya kifo hawapingi adhabu ya kifungo cha maisha na  utekelezaji wake.  Maana kama kibaka anaweza kuuawa kwa ghadhabu za raia, au jambazi kutumikia kifungo cha maisha, inakuwaje waliyemuua mtu mashuhuri kama Jemadari Imran Kombe waachiwe huru baada ya kutumikia miaka kumi na sita tu ya kifungo chao?

Pamoja na upole wote wa Mwalimu Nyerere aliidhinisha kunyongwa kwa Abdallah Mwamwindi aliyemuua Dk. Wilbert Kleruu  aliyekuwa mkuu wa Mkoa wa Iringa.  Na baadaye Rais Ali Hassan Mwinyi aliidhinisha kunyongwa kwa kanali wa jeshi la wananchi aliyepatikana na hatia ya mauaji ya kutisha.

Kwa hiyo wapenda haki wanasubiri maelezo thabiti kuhusu mazingira ya msamaha huu. Vinginevyo wataona kuwa msamaha huu ni ithibati kuwa askari hawa, kweli walitumwa kumuua Jemadari Kombe na utawala uliokuwa madarakani wakati huo uliongozwa na Benjamin W. Mkapa.

Mwandishi wa makala hii, Prof. Abdallah J. Saffari, ni mwanasheria mashuhuri nchini, wakili wa mahakama kuu. Anapatikana kwa simu Na. 0754 262523.
0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)