Nani anafikiri kwa niaba ya Rais?


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 27 October 2010

Printer-friendly version

HILI linaweza kuwa swali gumu kupata majibu haraka lakini nitauliza, nani anafikiri kwa niaba ya Rais?

Kinachonisukuma kuuliza swali hii ni kutokana na ukweli kwamba wapangaji mipango inayotekelezwa na serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) chini ya Jakaya Kikwete si mawaziri katika serikali hii ya awamu ya nne wala washauri wake ila watu walioko nje ya mfumo wa utawala.

Watu hao, ambao kwa sababu za kisiasa hubezwa sana na kuambiwa wahuni au Kikwete mwenyewe anawaita majuha, ndio wanaopanga mipango ya maendeleo na serikali inajifaragua na kutekeleza siku chache baadaye--wapinzani.

Kikwete amepita kila kona, ametoa ahadi 100 kubwa na ndogo, za makundi na watu binafsi, lakini zote si lolote si chochote kwa ahadi za kupewa elimu na afya bure zilizotolewa na Prof. Ibrahim Lipumba wa Chama cha Wananchi (CUF) na Dk. Willibrod Slaa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Hawa jamaa hawako katika mfumo wa utawala.

Baada ya kuona mambo magumu Kikwete amekaa, amewaza akaona heri aibe sera hiyo ya wapinzani wake, CHADEMA na CUF, kisha akamtumia Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Prof. Jumanne Maghembe aropoke:
“Serikali inafanya mabadiliko makubwa katika sekta ya elimu nchini, ikiwa ni pamoja na wanafunzi wote wanaomaliza darasa la saba kuendelea na masomo ya kidato cha kwanza hadi cha nne bila kuchujwa”.

Hizi ndiyo ghiliba za CCM. Katika kipindi chote cha kampeni, wapambe wake na JK mwenyewe wamekuwa wakisema elimu bure haiwezekani na vyombo vyao vya habari vikamzodoa Dk. Slaa.

Yako wapi? Wiki hii, CCM imelamba matapishi yake ikidai; “Msingi wa Ilani ya CCM ya mwaka 2010 ni kuwa kuanzia mwaka 2012 elimu ya msingi itakuwa kuanzia chekechea hadi kidato cha nne,” anadanganya Prof. Maghembe.

Sera hiyo ni ya CHADEMA/ CUF ambayo wagombea wa urais, Dk. Slaa na Prof. Lipumba wamekuwa wakiinadi katika kila kona ya nchi hii kwamba ukomo wa elimu ya msingi na ya lazima ni kidato cha nne, badala ya darasa la saba.

Mbali ya kunadi sera hiyo, Prof. Lipumba na Dk. Slaa wanasema wakishika madaraka watatoa elimu bure hadi ngazi ya elimu ya juu.

Maana ya elimu bure kama wanavyosema Dk. Slaa na Prof. Lipumba ni kwamba serikali yao ndiyo itachukua dhamana ya kutafuta fedha za kusomesha wanafunzi wote bure bila kujali anatoka familia tajiri au maskini.

Msingi wa mpango huu ni kuondoa upendeleo na matabaka katika jamii yanayokuzwa na CCM.

Sasa kama wapinzani CUF na CHADEMA ndio wanakaa, wanabungua bongo, wanafikiria mambo mazuri kwa maendeleo ya nchi, Kikwete na CCM yake wa nini?

CCM inaongozwa na watu ambao wamezirai hivyo huhitaji kuzinduliwa kwa ‘shoti’ ya umeme na safari hii umeme kwao ni Dk. Slaa au Prof. Lipumba.

Prof. Lipumba na Dk. Slaa wanapofika kusema jambo huwa wamefanya utafiti wao wenyewe au kwa kutumia tafiti za serikali na mashirika ya kimataifa.

Wana uwezo wa kufanya tafiti kwa sababu walipata shahada hizo kwa kufanya tafiti si kupewa kama hisani wala kujiita kama walivyo mawaziri kibao katika serikali ya awamu ya nne. Wanajipa vyeo kama wasanii Dk. Remmy, Dk. John, Prof. Jay.

Hawa wote hawawezi kufanya mambo kama wasomi waliohitimu shahada za udaktari wa falsafa kwa vile ni wasanii waliojiita hivyo kujipa umaarufu wasiostahili.

Vipi waziri wa serikali ajiite Dk wakati hajasomea? Kama hajasomea, anawezaje kufanya mambo kama mtu aliyesomea? Wakikusanyika hawa kupanga maendeleo ya Watanzania watakwama kwa sababu hawana uwezo ndiyo maana wanasubiri Prof wa kweli Lipumba na Daktari wa kweli Slaa waumize vichwa ndipo wao wanukuu.

Kumbuka wakati CCM wakinadi sera ya kuchangia elimu na huduma ya afya katika kampeni za mwaka 2000 , CUF/ CHADEMA walisema watatoa elimu bure.

Wananchi waliwaona waongo CCM kuwa wa maana na wakapuuza wakweli CUF/ CHADEMA. Wote mashahidi CCM walilegea wakashindwa wakaanzisha elimu bure kwa shule za msingi mwaka 2001.

Wananchi wakae chini wapime kama kuna ulazima wa kumrejesha tena Kikwete na CCM madarakani.

Kikwete ameshindwa mambo ya kimsingi ya uongozi na utawala bora. Alipoingia madarakani aliweka sawa mambo kwa kusema urais hausomewi na wala hakuna anayesomea uwaziri.

Kwenye kampeni hizi, amebadilika anasema chagueni wazoefu. Wamesomea chuo kipi? Wagombea ubunge zaidi ya 65 wapya wamepata wapi uzoefu? Maana isije ikawa analenga wapinzani akasahau wa kwake.

Bado nauliza, nani anafikiri kwa niaba ya Rais? Kikwete alitetea ukubwa wa Baraza la Mawaziri akisema utitiri wa mawaziri ulilenga kurahisisha utendaji kazi, akasahau kwa kufanya hivyo anaongeza matumizi ya serikali.

Miaka miwili baadaye, baada ya wazee kumhurumia na kumwambia awaache, ndipo kwa shida sana akabakiza mawaziri 47 kutoka 61.

Dk. Harrison Mwakyembe alipendekeza kitu katika Ripoti ya Uchunguzi wa Richmond, kwamba biashara na siasa vitenganishwe. JK alitutusa wazo hilo akasema atafanyia kazi. Hadi leo kaputi.

Katika kipindi cha miaka mitano aliomba apewe orodha ya mafisadi, akakabidhiwa; aliomba orodha ya wauza ‘unga’ yaani dawa za kulevya, akapewa; na aliomba pia orodha ya majambazi, akafikishiwa.

Katika kampeni hizi hazungumzii majambazi maana hata wanajeshi wanashiriki; hazungumzii wauza unga, walarushwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wala mchwa katika halmashauri—mafisadi wamemzingira kama chatu—kwisha kazi.

Usahaulifu: Agosti mwanzoni Kikwete alitembelea eneo la Kimara na akasema maji ya uhakika Dar es Salaam itakuwa mwaka 2013. Mungu wangu Jumatano akiwa Mwembeyanga akasahau akaahidi upya akisema maji ya uhakika Dar kuanzia mwakani. Huyu wa nini tena ikulu?

0
No votes yet