Nani anambeba Profesa Kapuya?


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 05 May 2010

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki
Profesa Juma Athumani Kapuya

Kuna watu wanazaliwa na bahati. Wengine wanakutana na bahati wakati fulani katika kipindi cha maisha yao. Wengine wanaitafuta na kupigana kwa ajili ya bahati - Malcolm X

WAKATI aliyekuwa Makamu wa Rais, Dk. Omar Ali Juma, alipofariki dunia mwaka 2002, magazeti ya Tanzania yalionyesha picha ya Profesa Juma Athumani Kapuya, akilia kwa uchungu kuomboleza msiba huo.

Kapuya alilia kwa uchungu katika namna ambayo sijawahi kuona kiongozi wa kitaifa akifanya hivyo hadharani. Ilibidi ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu, wakiwamo baadhi ya mawaziri wenzake, waende kumshika ili kumtuliza.

Mara ya mwisho kupata taarifa za kiongozi wa kitaifa kulia hadharani ilikuwa ni wakati wa msiba wa aliyekuwa Rais wa Ufaransa, Charles De Gaulle, katika miaka ya sabini, pale aliyekuwa mtawala wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jean Bedel Bokassa.

Alibubujikwa na machozi mbele ya jeneza la Gaulle uyo na kuishia kusema, “Baba….Baba… Baba.”

Baada ya kuona picha za Kapuya akilia, wakati ule ghafla sura ya Bokassa ikanijia kichwani (na hawafanani hata kidogo). Nikajiuliza: Kwa nini Profesa alie vile? Dk. Omar alikuwa nani kwake? Au ndiye Godfather wake?

Hii ni kwa sababu, kwa maoni yangu, Profesa Juma Athumani Kapuya, hastahili kuwa waziri wa wizara yoyote hapa nchini kwa sababu ya rekodi yake ya utendaji tangu apewe fursa.

Kwa mambo ambayo ameyafanya katika miaka ya nyuma, Kapuya hakukuwa na sababu ya kubaki naye serikalini.

Labda kama anayemteua pekee ndiye anayeujua uzuri wake.
Nikiwa mwanafunzi wa kidato cha nne mwaka 1998, Kapuya alikuwa waziri wa Elimu.

Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu, mitihani ya taifa ilivuja kiasi kwamba baadhi ya mitihani ilionekana ikiwa imebandikwa kwenye vituo vya daladala kabla haijafanyika.

Mtihani ule ule uliokutana nao kwenye kituo cha daladala kabla hujafika shuleni, ndiyo ule ule uliokuja kukutana nao kwenye chumba cha mtihani.

Hatimaye serikali ikaamua kuifuta mitihani hiyo. Hasara iliyopatikana wakati huo haijapata kuelezwa hata leo. Na tangu wakati huo, ‘ugonjwa’ wa kuvuja kwa mitihani umekuwa ‘donda ndugu’ kwa serikali.

Pamoja na kashfa hiyo kubwa kwa serikali, Kapuya akaendelea kudunda tu kama kawaida. Akaendelea kuwa waziri na akasema hatajiuzulu kwa vile eti “hahusiki.”

Katika nchi ambazo waziri anajua wajibu wake, na serikali inafahamu maana ya uwajibikaji, Kapuya alikuwa ama ajiuzulu au aliyemteua alipaswa kumtema katika baraza lake la mawaziri.

Hilo halikufanyika. Na matokeo ya yeye kutochukuliwa hatua yoyote ni kwamba tatizo la wizi wa mitihani limeendelea.

Kama aliyemteua Kapuya hakumchukulia hatua, yeye angekuwa na nguvu gani ya kuwachukulia hatua wa chini yake?

 Na nakumbuka ni katika kipindi hicho ndipo alipokuwa akifanya maamuzi ya ajabu ajabu kwenye masuala ya michezo. Nakumbuka zaidi tukio la kushusha au kupandisha daraja timu isiyostahili.

Kwa sababu ambazo ni serikali yetu pekee inazifahamu, Kapuya akaendelea tu kupeta na kuwa waziri.

Alipopelekwa kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, kama kawaida yake, Kapuya akafanya jambo ambalo lilizua mjadala katika vyombo vya habari.

Alitumia ndege ya jeshi kufanya ziara binafsi katika jimbo lake la uchaguzi. Kimsingi, kwa wadhifa wake, alikuwa anaruhusiwa kutumia ndege hiyo. Lakini tatizo akawa anatoa lifti kwa watu. Kiutaratibu, hili ni jambo ambalo watu hawakuwa wakilielewa.

Haya yalikuwa matumizi mabaya ya mali ya umma. Katika nchi za wenzetu, hili lingechunguzwa na kufanyiwa kazi. Na ingethibitika kwamba mheshimiwa alitoa lifti kushoto,kulia na katikati, ni lazima rungu lingemwangukia.

Lakini hiyo ni nchi nyingine, si Tanzania. Hapa kwetu, hilo likapita kama lilivyokuja. Juma Athumani Kapuya akaendelea kuwa waziri hadi aliyemteua alipoamua kumrejesha kwenye Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana.

Lengo la aliyemteua kumpeleka katika wizara hiyo nyeti silijui. Wizara hii ni nyeti kwa vile inagusa kundi lenye watu wengi hapa nchini.

Sensa zote zilizowahi kufanyika nchini zimethibitisha pasipo shaka kwamba nchi yetu ni ya vijana. Kwamba karibu robo tatu ya watanzania ni vijana. Kwa hiyo waziri wa wizara hii anashughulika na walau nusu ya watanzania.

Anatakiwa kutazama maendeleo ya kundi hilo kubwa la watu. Katika dunia ya sasa ambayo ina tatizo kubwa la anguko la uchumi. Ni wizara ambayo, kwa maoni yangu, inahitaji mtu makini kwelikweli.

Cha ajabu akapelekwa Kapuya ! Na kama kawaida yake, tayari kashaharibu na ninaweza kukuhakikishia kwamba ataendelea kuwa waziri katika serikali hii.

Kama Kapuya angekuwa aina ya waziri anayestahili kuongoza wizara hiyo, huu mgomo wa wafanyakazi uliopangwa kufanyika Mei 5 mwaka huu, usingefikia katika hatua ya sasa.

Yeye angekuwa amekutana na viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) kabla hawajafikia hatua waliyofikia sasa.

Angekuwa tayari amempa rais taarifa kuhusu matatizo ya wafanyakazi. Rais angepanga kukutana na wawakilishi wa TUCTA kuweka mambo sawa. Kama serikali ingeona ina uwezo wa kutatua tatizo hilo, ingelitatua mapema au ingewaeleza wafanyakazi ukweli kuhusu hali halisi.

Lakini Kapuya hana muda wa kufanya haya. Kwake yeye, ni afadhali aende Uwanja wa Taifa kwenda kukabidhi Kombe la Ubingwa wa Ligi Kuu kwa klabu kipenzi chake ya Simba !

Waziri wa Kazi anapata wapi muda wa kwenda kuangalia mpira na kukabidhi makombe wakati mgomo wa wafanyakazi ukiwa unanukia? Hivi, kama mgomo huu utafanyika, yeye atakwepa vipi lawama za kuhusika?

Halafu sikiliza taarifa zake kwa wana habari tangu mgomo wa wafanyakazi ulipotangazwa. Wakati wafanyakazi wa serikali kuu ndio hasa wanaodai kuumizwa na mishahara yao kiduchu, yeye anakwenda kuzungumzia mishahara ya watu wa sekta binafsi ambayo serikali haihusiki.

Mwalimu anahusika vipi na mshahara wa wachimbaji madini na  mahausigeli? Kwa nini alifanya mkutano kutangaza mishahara ya watu ambayo serikali si inayolipa? Inachekesha. Sana tu.

Kama mgomo wa wafanyakazi utafanyika, uchumi wa nchi yetu, ambao tayari uko taabani, utaathirika sana. Na najua hakuna anayejali katika serikali yetu.

Na Kapuya ataendelea kuwa waziri katika serikali hii. Kwanza, yeye si aliyegoma. Watakaogoma ndiyo wenye matatizo. Yeye ataendelea kupeta.

Sina hakika kama ni bahati pekee ndiyo inayombakisha Kapuya madarakani. Lakini kama ni bahati, basi pengine mwenzetu ana bahati ya kuzaliwa.

Vinginevyo nina imani kwamba yupo anayemlinda Kapuya ndani ya serikali yetu. Swali pekee ninalojiuliza kichwani ni kwamba; ni nani huyo Godfather wa Kapuya?

0
Your rating: None Average: 4 (2 votes)