Nani anampotosha Kikwete?


Kondo Tutindaga's picture

Na Kondo Tutindaga - Imechapwa 18 July 2012

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala

MGOMO wa madaktari unaendelea kwa sura tofauti. Kila siku unachukua sura mpya na msokoto wake unazidi kuwa mgumu, huku serikali ikionekana kutokuwa na nia ya dhati ya kutatua mgogoro huu.

Baada ya Rais Jakaya Kikwete kuhutubia taifa na kuweka msimamo “madaktari warudi kazini au waondoke,” yaelekea bongo za watawala zimefika ukomo wa kufikiri.

Ndiyo maana jitihada za viongozi wa dini na wanadiplomasia mbalimbali hazijaweza kuzaa matunda kwa sababu yaelekea rais hana njia nyingine huru ya kubaini kinachoendelea zaidi ya ushauri anaopewa na wasaidizi wake wa karibu.

Hii ndiyo sababisho la itikio la vyombo vya usalama kuhusu utekaji na uteswaji wa Dk. Steven Ulimboka kuudhi wengi. Dk. Ulimboka amenukuliwa akisema ametekwa na watu waliojitambulisha kwake mbele ya mashahidi kuwa ni polisi. Walivaa magwanda ya kijeshi na walikuwa na bunduki. Ni mchoko wa kufikiri kusema polisi ndiyo wachunguze sakata hili.

Mwishoni mwa wiki iliyopita tulisikia viongozi wa madhehebu ya kidini wakitoa wito kwa serikali kurudi kwenye meza ya mazungumzo na madaktari ili kukomesha mateso kwa raia wake.

Walitaka pia kuundwa kwa tume huru ya uchunguzi kuhusu yaliyompata Dk. Ulimboka. Mwisho walisema rais Kikwete amepotoshwa kuhusu suala hili. Hili la mwisho ndilo kiini cha mjadala wangu wa leo.

Hii si mara ya kwanza kusikika rais anapotoshwa. Upotoshwaji huu hudaiwa kufanywa na wasaidizi, washauri, marafiki, familia, mawaziri au hata wakuu wa vyombo vya usalama. Kwa hali hiyo, mara nyingi imesikika kuwa rais hana matatizo bali wasaidizi wanampotosha.

Hali hii ya rais kupotoshwa haijawahi kukanushwa na ikulu wala serikali nzima. Kwa hiyo, wananchi wana njia mbili tu za kushughulikia huu upotoshwaji anaofanyiwa rais wao.

Kwanza, ni kuamini kama serikali inavyotaka, kuwa si kweli kuwa rais anapotoshwa. Lakini inatia shaka kuishia hapa kwa sababu si rais wala ikulu imewahi kukanusha hadharani kuwa rais amepotoshwa katika jambo fulani. Wanaodai rais anapotoshwa, wanafanya hivyo hadharani, tena mbele ya rais.

Pili, ikiwa ni kweli rais anapotoshwa na kupotoka, basi si tatizo la wapotoshaji bali ni tatizo la mpotoshwaji. Ni kosa kumpotosha kiongozi wa nchi, lakini kosa zaidi na hatari kwa kiongozi wa nchi kukubali kupotoshwa au kujenga mazingira ya kupotoshwa.

Ikiwa tabia hii imeendelea kwa muda wa kutosha, inatosha watu kuamini kuwa tatizo tulilonalo mkononi mwetu ni zaidi ya washauri wanaopmtosha rais, ila sasa ni tatizo la uwezo, weledi, na uadilifu wa mpotoshwaji.

Kwa bahati njema, rais wetu amewahi kutamka hadharani kuwa, “Akili za kuambiwa, nawe changanya na zako.” Aliyasema haya mwaka 2010 alipohutubia wanaojiita wazee wa mkoa wa Dar es Salaam.

Alimkemea kiongozi wa mgomo, Nicolas Mgaya na kufikia hatua ya kuwaambia wafanyakazi kuwa yuko tayari hata kukosa kura zao katika uchaguzi uliokuwa unakaribia. Ushauri nasaha aliowapa wafanyakazi, hivi sasa anahitaji kuutumia.

Kwamba hizi akili za kuambiwa na washauri wake, awe anachanganya na zake kwa njia ya kupima madhara ya maamuzi yake. Hata katika sakata la mgomo wa wafanyakazi, ilikuja kubainika wakati huo huo kuwa rais alipotoshwa kimahesabu, hali iliyomfanya ataharuki na kutoa hotuba yenye tarakimu za uongo. Waliomshauri, walilenga kumkasirisha rais na walifanikiwa sana.

Wakati wa kuanzisha mchakato wa katiba mpya ulizuka mgogoro bungeni. Wengi waliona muswada wa sheria ile umeandaliwa vibaya. Wabunge wa CHADEMA wakatoka nje na kuacha wabunge wa CCM wakiwazomea.

Bunge likaendelea kwa mbwembwe na kuupitisha muswada mbovu kuwa sheria mbovu. Wabunge wa chama kilichopo ikulu badala ya kujadili muswaada wakaishia kuwajadili CHADEMA.

CHADEMA wakafanikiwa kukutana na rais na kueleza mashaka yao kuhusu sheria iliyopitishwa. Rais akashangaa kila kitu alichoambiwa hadi kufikia hatua ya kuhoji wasaidizi wake aliokuwa nao, kuwa kwa nini mmekataa mawazo haya mazuri ya CHADEMA?

Ikabainika rais alikuwa anapotoshwa na wasaidizi wake pamoja na makada wa chama chake kuhusiana na sheria ya uundwaji wa katiba mpya. Kwa tahadhari kubwa inayotokana na woga kwa chama chake, akayakubali maoni yao na kuahidi kuirudisha sheria ile bungeni ifanyiwe marekebisho kabla ya kuanza kutumika.

Woga ule aliouonyesha mbele ya wapinzani ikulu, ndicho kiini na silaha inayotumiwa na washauri wake kumdanganya katika masuala mengi tete yanayoikabili nchi kwa sasa.

Sheria ile iliporudishwa bungeni, kukawa na tishio la kuyakataa marekebisho yaliyokuwa yanapendekezwa. Joto la kisiasa likapanda na kushuka huko Dodoma. Rais akaenda Dodoma na kukutana na wabunge wa chama chake kwa kuwa alikuwa amepotoshwa na washauri wake kwamba hali ni mbaya.

Badala yake akawakuta wabunge wa CCM wakiwa tayari kuyakubali marekebisho ya sheria hiyo. Wakammiminia pongezi nyingi kwa kurudisha sheria ile na mambo yakaisha. Kwa wema na ubaya, rais wetu anapotoshwa.

Tumeshuhudia mabadiliko mengi ya baraza la mawaziri yanayotokana na rais ama kupotoshwa au kukubali kirahisi kupotoshwa na washauri. Katika sakata la Richmond, aliposhauriwa na hatimaye kukubali kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge, hakujua mkenge aliokuwa anauingia. Alipotoshwa akapotoka.

Baada ya uchunguzi, Edward Lowassa mwenyewe anasema alimshauri afike Dodoma usiku ili “kuzima” maasi ya wabunge wa CCM. Lakini washauri wakampotosha kuwa amshauri Lowassa aandike barua ya kujiuzuru lakini asiikubali.

Lowassa alipoondoka kurudi mjini, akashauriwa naye akakubali Lowassa kuondoka. Hii ilikuwa usiku wa manane na bila kumshirikisha Lowassa. Kikwete hakujua madhara ya jambo hilo. Alipotoshwa, akapotoka.

Serikali ikavunjika. Akalazimika kuiunda upya. Vita kali ya makundi ikahamia ndani ya baraza la mawaziri na kwenye chama. Hadi sasa, si Lowassa wala Kikwete aliye na furaha na maamuzi yale yaliyotokana na ushauri mbaya aliyopewa rais.

Wakati wa awamu ya pili ya Mzee Mwinyi, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliokoa jahazi pale alipoamua kuwashughulikia wapotoshaji wa rais. Walikuwa Horace Kolimba na John Samwel Malecela.

Lakini sasa hatuna Nyerere mwingine wa kushughulikia wapotoshaji wa rais. Kibaya zaidi, Kikwete siyo Mwinyi aliyekubali kuwa yeye ni kichuguu na Nyerere ni Mlima Kilimanjaro. Baadhi ya wasaidizi wake wanadai kuwa “haambiliki,” lakini papo hapo wanampotosha na kupotoka.

Viongozi wa dini wamesema juzi kuwa anapotoshwa. Madaktari baada ya hotuba ya rais walisema anapotoshwa. Yeye mwenyewe alikubali ikulu kuwa anapotoshwa na washauri kuhusu maoni ya wapinzani kuhusu katiba. Je, sasa tufanye nini na rais anayepotoshwa na kupotoka? Je, akipotoshwa katika masuala ya uhai wa nchi itakuwaje?

Mbona rais anapotoshwa kuwa hakuna mgomo wa madaktari, wakati ukweli mgomo bado upo na ndiyo kwanza umeanza? Je, tufanye nini hapa kwa kuwa migomo iko mingi na kila siku inazaliwa mpya?

Kwa mfano, kuna mgomo wa wana usalama, wanaoacha wahamiaji haramu waingizwe nchini wakiwa ndani ya makontena ya mizigo. Kuna mgomo wa washauri wa rais – wanaojua ukweli lakini wakaamua kugoma kumshauri rais vizuri na nchi inazidi kuzama katika lindi la wasiwasi.

Kuna mgomo wa wabunge wa CCM – wanaogoma kuwakilisha wananchi na kuamua kuwakilisha chama! Kuna mgomo wa serikali kukataa kurudi mezani kuongea na madaktari ili kuokoa maisha wa wagonjwa walioichagua CCM. Tufanye nini hapa?

0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: