Nani anamtuma Augustine Mrema?


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 07 April 2009

Printer-friendly version
Gumzo
AUGUSTINE Mrema, mwenyekiti wa chama cha cha Tanzania Labour (TLP)

AUGUSTINE Mrema, mwenyekiti wa chama cha cha Tanzania Labour (TLP) bado hajaacha tabia yake ya siku nyingi ya kushutumu na kutuhumu kila anayetofautiana naye.

Kuanzia ndani ya chama chake, hata nje ya chama, Mrema amekuwa anatuhumu kila mwenye mawazo na mtazano tofauti na yeye.

Tuhuma za sasa zimemgusa rafiki yake wa siku nyingi, mtetezi wake wa miaka yote na Katibu Mwenezi wa chama chake, Benedict Mutungirehi.

Mrema anasema Mutungirehi amekodiwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kumng’oa katika kiti chake. Kisa: Mutungirehi ametangaza kuwania uenyekiti wa TLP unaoshikiliwa na Mrema. Uchaguzi mkuu wa TLP unatarajiwa kufanyika 19 Aprili 2009.

Mutungirehi aliyepata kuwa mbunge wa Kyerwa, Karagwe, mkoani Kagera kutoka mwaka 2000 hadi 2005, anasema ameamua kugombea nafasi hiyo ili kufufua uhai wa chama hicho na kujenga matumaini mapya kwa wanachama na wafuasi wa TLP kutokana na kile anachoita, “Nyakati za Mrema kufikia ukomo.”

Lakini Mrema amemtaka Mutungirehi kuacha mara moja kumpinga. Anasema iwapo Mutungirehi ataendelea na dhamira yake ya kutaka uenyekiti wake, basi anaweza kutengua nafasi zake katika chama na kumfukuza uanachama.

Mrema anadaiwa kuchochoea uadui kati ya Mtungirehi na wanachama; kati ya Mutungirehi na viongozi na kati ya wanachama na wanachama. Anasema anawaomba “wanachama wa TLP kutomchagua kibaraka wa CHADEMA.”

Katika hili hakuna asiyeona kuwa matamshi hayo yatamwathiri vibaya Mutungilehi na wale wanaomuunga mkono katika mbio za kutafuta uongozi ndani ya chama hicho.

Hata hivyo, hii si mara ya kwanza kwa Mrema kushutumu na kutuhumu wenzake. Wala madai kwamba wale wanaompinga na kutofautina nao kisiasa wametumwa, hayakuanza leo.

Kwa zaidi ya miaka 14 sasa, Mrema amekuwa anaendesha siasa za aina hiyo. Amekuwa anatuhumu kila anayempinga. Amekuwa anahubiri: “Huyu ametumwa na mashushushu (Idara ya Usalama wa Taifa) kuja kunifiksi (kuniharibia) na, au majigambo kuwa yeye ni chuma cha pua.

Sasa swali moja muhimu la kujiuliza: Kama kila anayetofautina na Mrema ametumwa na CCM, CHADEMA, au usalama wa taifa. Je, yeye anapogombana na wenzake anakuwa ametumwa na nani?

Hivi hakuna uwezekano wa Mrema kutumwa na kutumika? Kwa nini wananchi waaminishwe kwamba ni wale wanaotofautina na Mrema tu ndio wanaotumwa, na wala si Mrema mwenyewe ndiye anatumika?

Kwa mfano, kabla ya Mrema kujiunga na NCCR-Mageuzi, alijiunga na TLP. Sasa ni nani aliyemtuma kuingia chama hicho? Je, alitumwa na utashi wake, CCM au mtu mwingine?

Hakudumu ndani ya chama hicho. Alijiunga na chama cha NCCR-Mageuzi ambacho kabla ya Mrema kuja kukivuruga kilikuwa kimesheheni viongozi na wanachama waliobobea na wanasiasa wanaoheshimika.

Sasa nani alimtuma Mrema kukimbia CCM, TLP na kujiunga na NCCR-Mageuzi? Alitumwa na CCM, au usalama wa taifa? Si kweli kwamba alitumwa kujiunga na NCCR- Mageuzi baada ya kuona kuwa TLP haikuwa tishio, ukilinganisha na NCCR ya wakati huo?

Katika kile kilichoitwa, “mtafaruku wa NCCR” ambapo Mabere Marando alisimama kutetea katiba na tishio la Mrema la kutaka kuvuruga upinzani, Mrema alisema “Marando ametumwa kunimaliza kisiasa.”

Lakini leo imefahamika na kila mwenye akili timamu, kuwa Marando na wenzake waliosimama kidete kumpinga Mrema walikuwa sahihi. Kwamba Mrema hakuwa na sifa za kuwa kiongozi katika chama kikubwa kama kile.

Mrema alipogombana na mbunge wa Viti Maalum na Mjumbe wa Kamati Kuu ya NCCR-Mageuzi wakati huo, Chiku Abwao, madai ya Mrema yalikuwa hayohayo. “Ametumwa kunimaliza. Anatumiwa na CCM kunidhoofisha.” Je, nani alimtuma Mrema kugombana na Abwao?

Hata alipogombana na Prince Bagenda, ambaye awali alikuwa mfuasi na mtetezi wake mkubwa, hasa wakati huo alipokuwa akigombana na Marando, Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mrema hakusita kulalamika. Alipokuwa ameona kuwa Bagenda hawezi kuvumilia mtu wa aina yake, akadai kuwa “Bagenda ametumwa.”

Hadi sasa hakuna ajuaye nani alimtuma Mrema kugombana na Bagenda.

Hata Harold Jafu, ambaye alikuwa anaishi nyumbani kwa Mrema, Masaki Dar es Salaam, “ndoa” yao ilipovunjika, alifukuzwa katika chama na Mrema kumtuhumu kuwa “ametumwa kunimaliza kisiasa.” Jafu alikuwa mfuasi wa karibu wa Mrema hadi kufikia kumfanya kuwa katibu mkuu wake.

Jafu aligombana na kila aliyekuwa anampinga Mrema ndani ya NCCR-Mageuzi. Kabla ya kujiunga na TLP, Jafu alikuwa mwenyekiti wa NCCR mkoa wa Dodoma. Je, ni nani alimtuma Mrema kugombana na Jafu?

Kazi ya kummaliza Jafu ilipokamilika, wembe wa Mrema ukamgeukia Mohammed Tao ambaye alitumika kumng’oa Jafu katika wadhifa wake. Wakati Jafu akiwa katibu mkuu, Tao alikuwa Naibu Katibu.

Haikuchukua muda, Mrema akamshughulikia Tao. Baada ya kazi aliyotumwa ya kummaliza Jafu kukamilika, Mrema akamfukuza Tao na kusema “ametumwa kunimaliza.” Haijulikani yeye alitumwa na nani kugombana na Tao.

Orodha ya waliokuwa watetezi wa Mrema na baadaye kugeuka maadui, ni ndefu. Kuna Msafiri Mtemelwa. Huyu aliwahi kupachikwa jina la “Black Mamba” kutokana na kuamua kumpigania Mrema kwa gharama yoyote ile ikiwa ni pamoja na kuongoza vikundi vya kufanya ghasia vya Mrema.

Kazi ya kumtumia ilipokamilika, Mtemelwa aliishia kutukanwa na Mrema kwa kuambiwa, “Ni mimi niliyekujenga kisiasa.” Haijulikani nani alimtuma Mrema kumjenga Mtemelwa kisiasa wala aliyemtuma kumchukia.

Maji yalipomfika shingoni, Mtemelwa alikimbilia Chama cha Wananchi (CUF). Huko hakudumu. Akaamua kujiunga na CHADEMA ambako yuko mpaka sasa.

Kuna Juma Kilimba (sasa mbunge wa Iramba Magharibi- CCM). Ni miongoni mwa walioitwa “vibaraka” wa Mrema waliotumika na kutupwa kama tishu.

Kuna Abbas Mtemvu (sasa mbunge wa Temeke). Katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) cha NCCR-Mageuzi, kilichofanyika mkoani Tanga, Mtevu alipigana hadharani kumtetea Mrema.

Lakini hatimaye aliambulia matusi. Haijulikani Mrema alitumwa na nani.

Yupo Mustapha Wandwi, Kamishina wa Polisi mstaafu. Huyu alivuliwa nguo hadharani na polisi walipokuwa wanaelekea ofisi za Umoja wa Matifa (UN) kumtetea Mrema kwamba anaadamwa na wapinzani.

Lakini mwisho wa siku aliambulia matusi, kejeli na dharau. Alimtuhumu kutumwa kummaliza kisiasa. Hadi sasa Mrema hajasema yeye alitumwa na nani kugombana na Wandwi.

Kuna Thomas Ngawaiya. Huyu alimwabudu Mrema. Alitoa nyumba yake kuwa ofisi ya TLP bila malipo yoyote. Hakuna alichopata zaidi ya tuhuma na shutuma. Alimkoromea. Akamkashifu. Hatimaye Ngawaiya akakimbilia CCM.

Leo Lekamwa ambaye alimkabidhi Mrema uongozi wa TLP, aliishia kutukanwa na kusakamwa kwa kumwambia, “Umetumwa Lekamwa. Huna jipya.”

Hata wale masheikh maarufu wa NCCR-Mageuzi walioondoka na Mrema kuingia TLP – kwa mfano Sheik Ali Iddi na Sheikh Mtopea – pamoja na kumpigania, waliishia kudhalilishwa na kutukanwa.

Mchango wa Sheikh Mtopea katika kampeni za ubunge wa Mrema katika jimbo la Temeke, hauwezi kusahaulika. Katika jua na mvua, alisimama kumnadi Mrema. Haikuwa kazi rahisi Mrema kushinda ubunge katika jimbo hilo tena katika uchaguzi mdogo.

Lakini hakuna alichoambulia Mtopea. Badala yake, Mrema alimwambia, “Sheikh gani wewe? Kama Usheikh ni kofia hata mimi ninayo.” Je, Mrema alitumwa na nani kuwafanyia haya waliokuwa wanachama, wafuati na viongozi wenzake?

Shiekh Ali Iddi kwa upande wake, mbali na kutoa mchango mkubwa kwa Mrema, alikuwa pia mgombea mwenza wake katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2000. Aligombana naye. Je, nani alimtuma Mrema kugombana na masheikh hawa?

Hata Dk. Masumbuko Lamwai aliyemtetea Mrema katika Bunge na ndani ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka, mwisho wa siku alilipwa alichostahili kutoka kwa Mrema: Keleji, kebehi na vijembe.

Mrema hakujali mchango wa Lamwai. Alimalizana naye kwa staili ya “shukurani ya punda ni mateke.” Alimtuhumu na kumshutumu kuwa “Lwamwai umetumwa kunimaliza.” Je, hapa napo Mrema alitumwa na nani?

Hata Makongoro Nyerere, aliyemtetea Mrema na kumuacha baba yake, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere hakupata shukurani kutoka kwa Mrema.

Mchango wa Makongoro katika kampeni za urais wa Mrema mwaka 1995 na ubunge jimboni Temeke, haukuwa haba. Lakini Makongoro kama ilivyo kwa wenzake wengine, aliishia kaumbiwa “…unanipinga kwa sababu mimi ni Mchagga.”

Steven Wasira, ambaye alikuwa mfuasi wa karibu wa Mrema, hakuna alichopata, isipokuwa matusi na kejeli. Shutuma na tuhuma alizombebesha ni pamoja nakusema, “Wasira unajifanya msomi. Hamna kitu. Umetumwa kunimaliza.” Je, nani alimtuma Mrema kugombana na hazina yake?

Hiyo ndiyo staili ya Mrema. Kulialia. Kutafuta kuonewa huruma. Leo anasema iwapo hatachachaguliwa tena kuongoza TLP, chama hicho kitafilisiwa.

Katika kitabu chake “ Hatma ya Mageuzi Tanzania ,” Ndimara Tegambwage anaandika, “Mrema anaumwa… Ana ugonjwa wa kisukari cha siasa…wa kupenda kusifiwa, kuonewa huruma…”

Mfano anaoutoa ni kwamba kama si yeye “kucheza tik tak, katika kesi aliyofungua Thomas Ngwaiya na kudai Sh. 30 milioni, jengo la TLP lililopo Magomeni Dar es Salaam lingekwisha kuuzwa.”

Nilipomuuliza Marando ambaye Mrema amekuwa akimtuhumu na kushutumu, hadi kuaminisha baadhi ya wananchi tuhuma za kuchonga, alijibu haraka, Mmuulize yeye. Bila shaka atakuwa na idadi kubwa ya wanaomtuma.”

Kuna taarifa kwamba kilichomsukuma Mrema kugombea tena uenyekiti wa chama chake, ni nyumba anayoishi iliyopo Sinza Dar es Salaam .

Nyumba hiyo ni mali ya TLP, na imesajiliwa kwa jina la Mwenyekiti wa chama hicho. Hii ina maana kwamba Mrema asipokuwa mwenyekiti atalazimika kuhama katika nyumba hiyo.

Na Mrema hana pengine pa kwenda jijini Dar es Salaam. Hiki ndicho chanzo na kichocheo cha kutuhumu wanaotaka kugombea uenyekiti kwa kusema “wametumwa,” kama alivyomwambia Mtungirehi

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: