Nani anamuenzi Mwalimu Nyerere?


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 01 November 2009

Printer-friendly version

LEO ni miaka 10 tangu mwasisi wa taifa hili, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere afariki dunia. Alifariki 14 Oktoba 1999 katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas, nchini Uingereza.

Ni miaka 14 tokea aondoke madarakani. Mwalimu Nyerere aling’atuka urais, Oktoba 1985.

Miaka miwili baadaye (mwaka 1987), aling’atuka uongozi wa chama alichokiasisi – Chama Cha Mapinduzi (CCM).

CCM ni mtoto wa TANU – Tanganyika African National Union na ASP – Afro-Shirazi Party – vyama vilivyopigania uhuru wa Tanganyika na Zanzibar.

Ilikuwa mwaka 1995 Nyerere alipoanza kukemea viongozi aliowakabidhi madaraka na ambao walikuwa wameanza kuvuruga maadili ya uongozi.

Hii ilikuwa wakati taifa limo katika mchakato wa kumpata rais wa tatu wa Tanzania. Ilikuwa tayari katika kipindi cha mfumo wa vyama vingi.

Kwanza, alishambulia wana CCM waliokuwa wakipigana vikumbo kutaka urais. Alihoji, “Kuna biashara gani ikulu, mbona ni mahali pagumu?”

Nyerere aliamini kuwa uongozi wa nchi ni jambo zito; ni sawa na mtu kubeba gunia la mawe.

Lakini tujiulize, mpaka sasa ni mangapi mazuri yametekelezwa ambayo Mwalimu aliamini na kusimamia.

Mwalimu alikuwa na sera za elimu zilizolenga kuwapa wananchi elimu kwa bei nafuu au bila malipo ya nyongeza kwa kodi za wazazi wao.

Kwa kuanzisha chuo kikuu, Mwalimu alilenga wananchi kupata elimu hapahapa nchini. Lakini leo, baadhi ya viongozi wanapeleka watoto wao kusomea nchi za nje.

Hii ina maana kwamba raslimali za taifa zinahamishiwa nje; lakini pia viongozi wanaacha kushughulikia vyuo vya ndani kwa kuwa watoto wao hawasomi katika vyuo hivyo.

Maana yake ni kwamba, elimu inayotolewa nchini, imekusudiwa zaidi kwa watoto wa masikini. Tatizo limekuwa kubwa zaidi mwaka 2006 pale serikali ilipoleta sera ya mikopo kwa wanaotaka kusoma vyuo vikuu.

Utoaji wa mikopo badala ya kuleta neema umeleta matatizo mengi na sehemu kubwa ya walengwa hawanufaiki.

Keki ya taifa inaliwa na wachache.

Unyonyaji wa maliasili ya taifa unafanyika kupitia mikataba inayoandaliwa kwa ushirikiano na watumishi wa serikali ambao walitegemewa kuwa ndio walinzi wa maliasili hiyo.

Katika sekta ya afya, hali ni mbaya zaidi. Huduma zinazotolewa kwenye zahanati na hospitali za serikali, hazikidhi mahitaji ya mgonjwa.

Lakini wakati hali ikiwa hivyo, viongozi wa serikali hukimbilia kutibiwa nje; wakati mwingine hata kwa magonjwa yanayotibika kwa dawa zilizoko nchini.

Gharama za safari na tiba za viongozi wetu zingetumika kuboresha hospitali zetu, zingesaidia idadi kubwa ya wananchi wasiokuwa na uwezo wa kwenda nje kutibiwa.

Leo wapo wanaomkumbuka Nyerere kwa kuamini kuwa angekuwepo hayo yasingetokea. Wapo wanaosema kwa utovu wa maadili ulivyo kwa viongozi serikalini, kumkumbuka Nyerere ni kiini macho.

Mwalimu hakupenda makuu wakati wa uongozi wake. Wapo wanaosema kwamba alibisha hata pale aliposhauriwa na daktari wake kwamba inampasa apelekwe Uingereza kufanyiwa uchunguzi wa kina wa afya yake.

Bado Mwalimu aliamini kuwa haumwi katika kiwango cha kulazimisha kufanyiwa uchunguzi nje ya nchi. Aliamini kwamba taifa masikini alilolijenga, halikuwa na uwezo wa kuhimili gharama kubwa za kumpatia tiba Uingereza.

Je, ni viongozi wangapi leo hii wenye moyo huo? Hawapo, ndio maana zipo rekodi za baadhi yao kukimbilia Ulaya hata kwa mafua.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: