Nani anasema Sitta kashushwa?


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 01 December 2010

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

MOJA ya mijadala mikubwa inayoendelea nchini kwa sasa katika vyombo vya habari ni kuhusu aliyekuwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta kuteuliwa kuwa Waziri wa Afrika Mashariki.

Baadhi wanajenga hoja kwamba ameshushwa hadhi, na wengine wanasema hajashushwa. Hakuna jibu moja; huu ni mjadala na ili kujua nafasi yake, tutazame nini kinafanyika nchi jirani za Uganda na Kenya.

Nchini Uganda, iwapo litatokea jambo lolote, Yoweri Museveni na kusababisha ashindwe kuendelea na wadhifa wake wa urais, majina ya matatu yanatajwa kuwa na uwezo wa kushika wadhifa huo.

Majina hayo ni ya Katibu mkuu wa chama tawala cha National Resistance Movement (NRM), Amama Mbabazi, Balozi wa Uganda Umoja wa Mataifa, Ruhakana Rugunda na Naibu Waziri Mkuu, Eriya Kategaya.

Kati ya wote hao, Kategaya ana sifa ya ziada kuliko hao wawili. Yeye ni rafiki wa karibu wa Museveni tangu enzi ya utoto kwani walisoma wote katika Shule ya Msingi Ntare.

Museveni na Kategaya pia walisoma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) katika miaka ya 1960 ambacho kilikuwa kikisifika kama chuo cha kimapinduzi.

Wote pia walikuwa pamoja katika vita ya msituni iliyomwingiza Museveni madarakani. Hata hivyo, Kategaya alikuwa akifanya zaidi shughuli za nje ya msituni kuliko kushika bunduki.

Tofauti na Museveni, Kategaya ni msomi wa ukweli, mtaratibu, muungwana na mwenye uwezo mkubwa wa kujenga hoja pasipo kutumia nguvu kama rafikiye huyo.

Kategaya ndiye pia Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Uganda. Yeye, pengine kuliko mtu mwingine yeyote aliye hai, anafahamu kuwa ni ndoto ya Museveni, siku moja kuwa Rais wa Afrika Mashariki.

Na kwa mujibu wa mtiririko wa kuelekea kwenye Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki, huenda hilo likafanyika kwenye awamu hii ya pili ya utawala wa Rais Jakaya Kikwete.

Ndiyo maana, mimi ni miongoni mwa wanaoamini kwamba rais Kikwete alifanya uamuzi wa maana kumteua Samuel Sitta, kuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Katika hatua iliyofikiwa sasa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), baada ya kupitishwa kwa vipengele vya Ushuru wa Forodha wa Pamoja na Soko la Pamoja, huu ni wakati ambao EAC inaelekea katika jambo nyeti na gumu kidogo.

Ndiyo maana Museveni akampa nafasi hiyo Kategaya, mjenzi wa hoja na anayeifahamu EAC ya zamani iliyovunjika mwaka 1977 na hii ya sasa.
Ndiyo maana Rais Mwai Kibaki wa Kenya amemteua Profesa Hellen Sambili, msomi wa kiwango cha juu kushika wizara hiyo katika mabadiliko yaliyofanyika mwaka mmoja uliopita.

Tanzania inahitaji mtu ambaye ana ufahamu mkubwa wa EAC ya zamani na ya sasa. Anayejua kwa undani wapi Tanzania ilikosea katika jumuiya ya kwanza na kwa vipi kasoro hizo zizuiwe zisirejewe.

Na mtu huyo anapaswa kuwa anafahamu mambo hayo kwa vile aliyapitia na alikuwa sehemu ya maamuzi na si mtu aliyesoma mambo hayo kwenye vitabu na madaftari.

Sitta alikuwapo wakati EAC ikivunjika. Ni msomi na mjenzi mzuri wa hoja. Na hataogopa kujenga hoja mbele ya mawaziri wenzake wa EAC.

Kuna wanaoamini kwamba Sitta ameshushwa hadhi yake kwa kukubali kuvuliwa uspika na kupewa uwaziri. Ukitazama kwa jicho la tatu, unaweza kuona kwamba pengine Watanzania watafaidika zaidi na nafasi ya sasa ya Sitta kuliko ile ya uspika.

Wakati Shirikisho la Afrika Mashariki litakapoanza (kama kweli tutafika huko) mengi ya maamuzi magumu ya nchi wanachama yatafikiwa katika Bunge la Afrika Mashariki na mabunge ya kitaifa yatapungua nguvu.

Kwa hiyo, huenda uspika wa Sitta katika bunge hili usingekuwa na maana tena miaka minne hadi mitano kutoka sasa.

Nafasi ya uwaziri wa Afrika Mashariki katika kipindi hiki haimstahili mtu mgeni au mchanga katika nafasi hiyo au katika uwaziri.

Muda tu ndiyo utakaotuambia iwapo Kikwete alikosea au aliamua kumshusha cheo Sitta kwa kumpa nafasi ambayo baadhi ya wachambuzi na vyombo vya habari wamedai ni ya kumpoza.

Mwisho wa siku, Watanzania wangetakiwa kuangalia zaidi mustakabali wa nchi yao kuliko kuangalia kama Sitta amepanda au ameshushwa cheo.

Jambo la kwanza ambalo Sitta amezungumza tayari ni umuhimu wa kuongezwa kwa bajeti ya wizara hiyo kwenye eneo la elimu kwa umma.

Kwamba umma wa Watanzania utafaidika zaidi na EAC, katika hali yake ya sasa na pengine katika shirikisho, iwapo utakuwa na elimu ya kutosha kuhusu jambo hilo.

Kutoa elimu ya umma kwa Watanzania kuhusu EAC, jambo ambalo litamgusa kila mmoja katika suala la ajira, ardhi na uchumi, si kushushwa cheo au hadhi.
Katika kipindi chake cha uspika bungeni, Sitta atakumbukwa kwa mambo makubwa mawili.

Kwanza ni uamuzi wake wa kumsimamisha ubunge mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.

La pili ni namna alivyokuwa akishughulika na kundi la watuhumiwa wa ufisadi. Aliendesha mapambano makali ambayo kimsingi waliofaidika zaidi ni makundi mawili; CCM kwenye suala la Zitto na wapambanaji wa ufisadi kwenye vita yake ya pili.

Lakini kwenye EAC, Sitta atakuwa akitetea maslahi ya Watanzania wote. Kama atatetea maslahi ya Watanzania katika namna ileile aliyoshughulika na watuhumiwa wa ufisadi, Tanzania itafaidika na jumuiya hiyo.

Wakati watu wanapoendelea na mjadala wa iwapo Sitta ameshushwa au amepandishwa cheo, swali kubwa la kujiuliza liwe; lipi la muhimu zaidi kati ya kuwa na cheo kikubwa au jukumu kubwa.

Swali linatakiwa liwe iwapo ni muhimu kwa mtu mmoja kuwa na cheo fulani kikubwa kihadhi au kupewa hadhi ambayo inaweza kuamua mustakabali wan chi katika kipindi cha miaka mingi ijayo.

Nionavyo, Sitta ameongezewa majukumu ambayo yanaendana na haiba na uzoefu wake katika siasa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: