Nani anashauri rais wetu?


Jonathan Liech's picture

Na Jonathan Liech - Imechapwa 30 December 2009

Printer-friendly version

MAAMUZI mengi yaliyofanywa na Rais Jakaya Kikwete yanaibua maswali kuhusu iwapo ana washauri wa maana au ni yeye ndiye asiyetaka kufuata ushauri.

Ukizingatia namna mtandao uliomwingiza madarakani ulivyoparaganyika; na namna baadhi ya viongozi wastaafu wa serikali za awamu zilizopita (ambao wangeweza kuwa washauri wake wazuri) wanavyomzungumzia, unashindwa kupata jibu sahihi la maswali haya.

Kwa wanaomfahamu Kikwete, katika mazungumzo yasiyo rasmi wamekuwa wakinieleza kwamba yeye ni mtu anayetamani kukirejesha chama katika misingi yake ya asili – ile ya kutetea wanyonge.

Ilitarajiwa alipopata uenyekiti wa chama chake, angetumia fursa hiyo kukinyoosha chama. Hakufanya hivyo.

Angalia uamuzi wake wa kumteua Yusuph Makamba, kuwa katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Katika chama kinachojengwa katika misingi na kunachaomini katika utawala bora, Makamba hawezi kuwa mtendaji wake.

Kikwete hakuhitaji mtu mwenye uwezo mkubwa wa kuzungumza jukwaani ili kuvutia watu kujiunga na chama. Yeye mwenyewe ndiye turufu ya CCM.

Angeweza kumteua yeyote miongoni mwa makada wanaoheshimika na kukifahamu vema chama, ili amsaidie kuweka mambo sawa.

Huyo ndiye angerejesha misingi ya chama taratibu, ngazi kwa ngazi na angemuweka rais Kikwete katika sura halisi ya CCM ya asili.

Lakini hatua ya kumuweka Makamba kuwa mtendaji mkuu wa chama chake, kumezidi kudhoofisha chama na Kikwete mwenyewe.

Nafasi ya ukatibu mkuu katika chama kama CCM ni cheo kikubwa sana. Nchini Urusi, mara baada ya kifo cha baba wa taifa hilo, Vladmir Lenin, aliyemrithi alikuwa ni Katibu Mkuu wa chama cha Kikomunisti, Josef Stalin.

Hata nchini China, Jiang Zemin alipoachia ngazi kama rais wa nchi hiyo, aliyerithi nafasi yake alikuwa ni Hu Jintao, ambaye alitokea kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti.

Nchini Uganda, kama Rais Yoweri Museveni, ataondoka madarakani leo kwa hiari (sijui kama hilo litatokea), atakayemrithi anajulikana kuwa ni Stephen Amama Mbabazi, katibu mkuu wa chama tawala cha NRM.

Sasa nani anaweza kupendekeza Makamba kuwa raia wa nchi baada ya Kikwete kuondoka? Hata Makamba mwenyewe pamoja na kwamba kila mwanasiasa anatamani kupanda ngazi, lakini hana ndoto za kushika nafasi hyo.

Hapa mtu unajiuliza, nani alimshauri Kikwete kufanya uteuzi kama huu?

Hali kama hii ya kuhoji washauri unaweza pia kuiona kwenye uteuzi wa Sofia Mnyambi Simba kuwa waziri wa wizara nyeti ya Utawala Bora iliyo chini ya Ofisi ya Rais.

Taarifa zote za usalama wa nchi hii zinapita katika ofisi hii. Na kwa yale tuliyoyasikia akiyazungumza mama huyu Dodoma wakati wa vikao vya wabunge wa CCM na Kamati ya rais mstaafu Alli Hassani Miwnyi, unaweza kujiuliza kama siri za nchi hii ziko salama.

Kwa rais mwenye washauri makini, hii ni nafasi ambayo yeyote ambaye angepewa, alipaswa kuwa mtu ambaye umakini na ufahamu wake wa mambo hautiliwi shaka.

Hata uteuzi wa Lawrance Masha kuwa waziri wa mambo ya ndani katika serikali yake ni jambo la kushtua kwa wengi.

Wakati akifanya uteuzi huo, tayari jina la Masha lilikuwa limeanza kutajwa katika vyombo vya habari kuhusiana na ushiriki wake katika kashfa ya nyingi za kifisadi ikiwamo ukwapuaji uliofanywa na kampuni ya Deep Green Finance Limited.

Kama rais Kikwete alikuwa na dhamira ya dhati ya kushughulikia kesi za ufisadi, angepaswa kujua (au walau washauri wake wangemwambia) kwamba huenda serikali ingekuja kuchunguza kashfa hiyo.

Sasa baadhi ya vyombo vya ulinzi na usalama viko chini ya wizara ya Masha. Kama upelelezi ukianza, ni lazima Masha awe akifahamishwa hatua kwa hatua. Je, rais hakulina hili kwamba Masha hawezi kujichunguza mwenyewe?

Mtakumbuka pia kuhusu namna Kikwete alivyomteua Anatoly Choya kuwa mkuu wa wilaya wakati bado akikabiliwa na kesi ya rushwa mahakamani.

Ukiacha yote hayo, kuna hili la majuzi. Rais amekwenda mkoani Arusha kufungua hoteli ambayo ufunguzi wake umefanyika kwa mbwembwe.

Siku moja baadaye, watendaji kutoka Wakala wa Barabara (TANROADS) wamekwenda kubomoa ukuta huo kwa madai kwamba ujenzi ulikiuka sheria za barabarani.

Je, rais hakupewa taarifa na viongozi wa serikali wa Arusha kwamba kuna uwezekano wa TANROADS kufanya vitu vyao mara baada ya uzinduzi?

Hao washauri wa mambo ya ulinzi na usalama wanataka kusema kuwa hawakuwa na taarifa hii? Au watu wenyewe ndiyo hao wa dizaini ya Mama Simba?

Halafu, hivi huu utaratibu wa rais wa nchi kwenda kufungua hoteli umeanza lini? Kazi ya Makamu wa rais au waziri wa maliasili na utalii ni nini?

Au ndio tuseme rais mwenyewe anapenda kufungua hoteli na hata kama washauri wake watamwambia vinginevyo atawakaidi?

Mimi ni mkristo na katika kitabu kitakatifu cha Biblia, kuna hadithi moja kuhusu jamaa aliyeitwa Ahithofeli.

Huyu mtu anaelezwa kwamba alikuwa na maarifa mengi na alikuwa mshauri bota katika nchi yote ya Israel katika enzi ya Mfalme Daudi.

Baadaye akafarakana na Daudi na akawa mshauri wa miongoni mwa watoto wa mfalme huyo aliyefahamika kwa jina la Absalom, ambaye alitaka kumpindua baba yake.

Sasa siku moja Ahithofeli akatoa ushauri mzuri sana kwa Absalom lakini kijana huyo akaukataa. Na kama mwana huyo wa Mfalme angefuata ushauri huo, huenda angetwaa ufalme mara ile. Lakini kwa sababu Mungu alitaka Daudi aendelee na ufalme, Absalom akakataa ushauri wa jamaa.

Unajua nini kilichotokea? Ahithofeli alikwenda nyumbani kwake, akaaga kila mtu na akajitundika mtini (akajinyonga). Kule kukataliwa kwa ushauri wake kulimuuma sana.

Sisemi kwamba watu wote ambao ushauri wao unakataliwa na rais wakajinyonge, la hasha. Ninachosema ni kwamba kuna jambo ambalo mshauri anaweza kufanya kumwonyesha mshauriwa kwamba hajafurahishwa na hilo.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: