Nani anatunza usalama wa rais Kikwete?


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 16 June 2010

Printer-friendly version
Gumzo
Rais Jakaya Kikwete

ETI kituo cha mafuta ambako magari ya msafara wa Rais Jakaya Kikwete yaliwekwa mafuta na kushindwa kuwaka, ni cha mmiliki “anayeaminika.”

Hakika kila mtu angependa iwe hivyo ili kuondoa madai kuwa hata marafiki wa rais wanataka kumtisha na hata kumfanya “chakachuwa.”

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Nishati na Maji (EWURA, “chakachuwa” ni mafuta ya dizeli yaliyochanganywa na mafuta ya taa au mafuta ya petroli yaliyochanganywa na
mafuta ya taa.

Kuna madai kuwa ni mafuta ya aina hiyo waliyoweka kwenye magari yaliyokuwa yaingie kwenye msafara wa rais na kusababisha magari hayo kushindwa kuwaka.

Safari hii, bila shaka “chakachuwa” ililenga “kumchakachuwa” rais. Vyovyote itakavyotafsiriwa, mafuta yasiyowaka vizuri lazima yalete usumbufu kwa gari na abiria – gari litazimika mara kwa mara au litashindwa kuwaka.

Siyo lazima gari lililojazwa chakachuwa lishindwe kuwakia pale lilipowekwa mafuta. Matatizo yaweza kuja baadaye; labda baada ya kusafiri kilometa kadhaa.

Hii ni tofauti na ilivyokuwa mjini Moshi, wiki mbili zilizopita, kwenye kituo cha mafuta – Rafiki Petrol Station, kilichopo Barabara ya Taifa.

Hapa magari hayakuwaka baada ya kujazwa “mkorogo.”

Ripoti zilisema hivi: Magari matano yaliyokuwa katika msafara wa rais mkoani Kilimanjaro yalishindwa kuwaka kutokana na kuwekwa mafuta ya dizeli yaliyochanganywa na mafuta ya taa.

Wataalam wa mambo ya ulinzi na usalama; wale magwiji wa ulinzi waliofunzwa kujenga mashaka kwa kila kitu, wangeweza kuuliza, “Ingekuwaje iwapo magari haya yangekwama tukiwa na rais, tena usiku na gizani?”

Swali hilo haliwezi kuonekana la maana leo kwa kuwa magari hayakuwaka, lakini hayakuwa msafarani na haikuwa usiku.

Waliofunzwa kutilia mashaka kila tendo wangekwenda mbali na kuuliza, “Kama hali hiyo ingekuwa ni mpango maalum, kungetokea nini na sisi tungekabili vipi mazingira hayo?”

Labda swali jingine lingekuwa hili hapa: “Wangapi wamedhurika wakiwa nyumbani kwao au kwa marafiki au hata wapenzi wao?” Kwa hiyo lolote laweza kutendeka.

Hoja hapa ni ulinzi wa mkuu wa nchi; na ulinzi huu siyo wa Kikwete tu kwa kuwa ndiye alikuwa awe na magari hayo msafarani, bali yeyote atakayekuwapo.

Kuna hoja nyingi katika funikafunika ya kilichotokea. Kuna wanaosema lile la mafuta ya chakachuwa linaweza kutokea kwa yeyote yule na siyo lazima magari ya msafara wa rais.

Ndivyo walivyosema pia wakati gari la rais lilipopata “matatizo” naye akalazimika kulihama na kuingia jingine; huku ikaripotiwa baadaye kuwa lilikuwa lichomoke tairi.

Mara hii Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Salva Rweyemamu amelieleza tukio la Moshi kwa kauli kwamba “Rais yuko katika mikono ya watu makini, salama na wazalendo wanaoifahamu kazi yao.”

Salva amesema, kituo ambacho magari ya rais yalikwenda kujaza mafuta, “…ni miongoni mwa vituo vilivyoteuliwa kufanya kazi hiyo kwa muda mrefu; uamuzi wa kujaza mafuta magari ya rais katika kituo hicho haukuwa wa kushtukiza ama (au) kubahatisha.”

Kituo hiki cha mafuta kinachoaminiwa na ikulu ndicho Desemba 2008 Mamlaka ya Usimamizi wa Nishati na Maji (EWURA) ilifungia kuuza mafuta baada kuthibitika kilikuwa kinachanganya mafuta yake na “vitu vingine.”

Kwa mujibu wa taratibu za utendaji kazi wa EWURA, kituo ambacho hupatikana na kosa la kuweka vitu vingine katika mafuta, hutozwa faini ya Sh. 3 milioni na hulazimishwa kuboresha mafuta yake kwa kuyarudisha katika hali yake ya kawaida.

Bila shaka, hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa mmiliki wa kituo hiki – kutozwa faini na kulazimishwa kurejesha mafuta katika hali yake ya kawaida.

Mbali na kituo hiki, mmiliki huyo anamiliki kituo kingine cha Rafiki Petrol Station ambacho nacho tayari kimefungiwa kwa kosa la “kuchakachua mafuta.”

Kituo hiki kipya, kilifungiwa mwishoni mwa mwezi uliopita. Taarifa zinasema kipo jirani na kituo kilichojaza mafuta magari ya rais.

Katika mazingira hayo, nani anaweza kutetea uamuzi wa ikulu kutumia kituo ambacho tayari kimepatikana na hatia?

Nani anaweza kukubaliana na madai ya mkurugenzi wa ikulu kwamba uamuzi wa serikali kutumia kituo hicho, ulikuwa sahihi? Hakuna awezaye.

Siyo sahihi kutetea uamuzi wa serikali wa kutumia kituo ambacho tayari kimepoteza hadhi ya kufanya kazi kiliyoomba.

Siyo rahisi pia kutetea watendaji wabovu – wawe wa ikulu na usalama wa taifa au wengine ambao wameshindwa kazi ya kusimamia ulinzi wa rais na rasilimali za nchi.

Hata kauli ya Salva kuwa “Usalama mkuu wa nchi uko katika mikono ya watu makini, salama na wazalendo wanaoifahamu kazi yao,” yaweza kuwa ya kujenga matumaini tu kwani msemaji huyo asingesema jingine tofauti.

Bali wanaofuatilia wanaweza kupumua wanapopata kauli nyingine katika taarifa ileile ya Salva kwamba misafara ya aina hiyo, mara zote huwa na mipango mbadala ya usafiri “…yenye kiwango cha juu cha usalama.”

Mikasa iliyopata misafara ya rais Dar es Salaam na Moshi, ikujumlishwa kwenye taarifa kuwa rais ana ratiba ndefu, ngumu na ya kuchosha, kama ilivyoelezwa Oktoba mwaka jana, basi ni wazi kuwa wasaidizi wa rais hawamsaidii na hawastahili kutetewa.

Ni wasaidizi haohao waliomdanganya rais na kumchomekea vipengele ambavyo havikupitishwa na bunge katika Sheria ya Gharama za Uchaguzi na kumwacha aisaini kwa mbwembwe.

Hawastahili kulindwa kwa kuitwa makini.

Kinachoumiza ni kwamba, katika hili, aliyefanya makosa anafahamika na ametajwa mara nyingi – Philip Marmo – lakini hajachukuliwa hatua.

Kuna msululu wa wasaidizi wa rais wasiostahili kutetewa na yeyote kwa tuhuma wanazobeba au wanazobebeshwa.

Chukua mfano wa Januari Makamba, mmoja wa wasaidizi wa Katibu wa Kikwete.

Huyu anatuhumiwa “kuendesha kampeni chafu” na kwa kutaja jina la rais katika kutafuta ubunge wa Bumbuli, mkoani Tanga.

Hatua hii haiwezi kumfanya Kikwete kuwa salama kisiasa, kwa kuwa mbunge wa sasa wa jimbo hilo, William Shelukindo anaweza kufikiri kuwa rais ndiye kinara wa kumng’oa katika kiti chake kwa kumtumia Januari.

Aidha, hatua ya Januari ya kuanza mbio za kuwania jimbo hilo, huku akiwa bado mtumishi wa ikulu; huku serikali ikizuia watumishi wengine kufanya hivyo – hasa wanaogombea upinzani, kunaufanya uwanja wa ushindani kutokuwa linganifu.

Mwingine ni katibu wa rais, Prosper Mbena anayetuhumiwa kuanza kampeni za kuwania ubunge Morogoro Kusini.

Pamoja na kwamba Mbena amekanusha tuhuma za kutumia jina la Kikwete kujinadi, lakini hatua yake ya kubaki ikulu, kunamfanya mbunge wa jimbo hilo Hamza Mwenegoha na wanachama wengine wa CCM, kuona kuwa Mbena ana baraka za rais.

Katika mazingira haya, ufa miongoni mwa wabunge wa chama cha Kikwete na watendaji serikalini utazidi kuongezeka. Hii ni hatari kisiasa.

Msaidizi mwingine ni Yusuph Makamba, Katibu Mkuu wa CCM. Anatuhumiwa kubeba baadhi ya wagombea watarajiwa akiwamo mwanawe, Januari Makamba. Wote hawa hawastahili kutetewa; hawamsaidii rais wao.

Hata katika bajeti inayoendelea kujadiliwa bungeni, imedhihirika kuwa Kikwete hayuko salama. Watendaji wake wameshindwa hata kutambua vipaumbele vya serikali.

Mifano iko mingi. Kwanza, serikali imetenga Sh. 200 bilioni kugharamia mradi wa vitambulisho vya taifa, lakini ikatenga kiduchu kwa ajili ya kujenga upya au kuboresha shirika lake la reli (TRC).

Pili, serikali makini haiwezi kuingiza mradi wa vitambulisho vya taifa kama kipaumbele chake, lakini papohapo ikitenga Sh. 6 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Nzega Tabora.

Serikali iliyojaa watendaji makini lazima wangejiuliza: Kipi kinastahili kupewa kipaumbele kati ya mradi wa vitambulisho vya taifa na ujenzi wa barabara?

Ni kweli, vitambulisho ni muhimu, lakini tokea nchi hii ipate uhuru, hakuna ambaye amekufa njaa kwa kukosa vitambulisho.

Hakuna aliyekosa kitambulisho na hivyo kushindwa kusafiri, kusoma au kupata matibabu.

Hata ukisikiliza kauli za mawaziri wa zamani wa serikali, waliokuwa pamoja na Kikwete wakati wa utawala wa Benjamin Mkapa, Basil Mramba na Charles Keenja, utabaini kuwa Kikwete anakabiliwa na mtihani mgumu.

Ni Mramba aliyenukuriwa akisema serikali haina mikakati thabiti ya kupambana na umasikini; jambo ambalo linaonyesha kuwa kuna safari ndefu ya kufikiwa maendeleo ya kweli.

Anafika mbali zaidi. Anasema, yote haya yanatokana na serikali kutokuwa na mipango ya kuwakomboa wananchi wake katika nyanja za elimu.

Hii ni kauli ya mbunge wa CCM ambaye hajatangaza kuhamia upinzani.

Kama Mramba anasema safari bado iko ndefu, Kikwete atawezaje kuwambia Watanzania kuwa serikali yake inakaribia kumaliza matatizo yaliyopo?

Kama Mramba anasema serikali imeishiwa mipango na ubunifu, Rais Kikwete atawezaje kusema serikali na chama chake vina mipango ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu wa kuleta maendeleo?

Mramba amekuwa msaidizi wa Rais Kikwete. Kauli kama zake na matendo kama ya wote waliotajwa, vina nafasi gani katika kulinda usalama wa rais?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: