Nani anayekabidhiwa fedha ya Dowans?


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 22 December 2010

Printer-friendly version
Gumzo la Wiki
WAZIRI  Mkuu wa Jamhuri, Mizengo Pinda

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri, Mizengo Pinda amejitwisha zigo lisilobebeka. Litamuangusha. Ameahidi kulipa mabilioni ya shilingi kwa kampuni ya kufua umeme wa dharula, Dowans Holding Tanzania Limited.

Akizungumza na waandishi wa habari Ijumaa iliyopita, ikulu jijini Dar es Salaam, Pinda alinukuliwa akisema, “…Nchi hii inaendeshwa kwa utawala wa sheria. Tutakata rufaa, lakini tukishindwa, basi itabidi tulipe…”

Pinda, hata hivyo, amenukuliwa akisema, hukumu hiyo ni matokeo ya genge la watu wachache wanaofahamika; ambao wameamua kutafuna rasilimali za taifa bila huruma.

Tarehe 15 Novemba 2010, Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Biashara (ICC), iliagiza serikali kuilipa kampuni ya Dowans fidia ya Sh.185 bilioni kutokana na kile kilichoitwa, “Kukiuka masharti ya mkataba.”

Kampuni ya Dowans ilipata kazi hiyo baada ya kurithi mkataba wa kufua umeme kutoka kwa dada yake – Richmond Development Company (RDC), ambayo ilibainika baadaye kuwa haikuwa na hadhi, sifa wala uwezo wa kupewa kazi iliyoomba.

Sasa kabla ya Pinda kuagiza watendaji wa serikali kulipa mabilioni hayo ya shilingi na kugeuza taifa hili kuwa kichaka cha wajanja wachache kuvuna wasichopanda, kwanza ni lazima aeleze: Nani aliyefikisha serikali hapa ilipo katika sakata hili?

Pili, hicho ambacho waziri mkuu anaita, “genge la watu wanaofahamika,” ni akina nani? Nani anayewalinda serikalini na kwa maslahi yapi hadi yeye anashikwa na kigugumizi cha kusema, “Basi, tutalipa…?”

Tatu, kabla ya hundi ya malipo kuandikwa, waziri mkuu aeleze nani anayekabidhiwa fedha hizo?

Mpaka sasa, serikali haijataja mmiliki wa Dowans na wala haijataja mahali anakoishi?

Haya ni muhimu yajulikane mapema kwa sababu, aliyetajwa kuwa “mmiliki” wa Dowans Holding Tanzania Limited, Bregedia Jenerali Sulaiman Mohammed Yahya Al Adawi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) amekana, mara mbili, kumiliki kampuni hii.

Naye mfanyabiashara na mbunge wa Igunga, Rostam Aziz ambaye aliwahi kunukuliwa akisema, “Mimi nawafahamu Dowans, si Richmond,” hajataja hadharani mmiliki wa Dowans nchini.

Nako ndani ya Bunge, si serikali wala Kamati Teule ya Bunge iliyotaja mmiliki wa Dowans.

Badala yake, Kamati Teule iliyoongozwa na mbunge wa Kyera, Dk. Harrison Mwakyembe iliishia kusema, “Richmond ni mradi wa mkubwa…”

Hadi sasa huyo mkubwa hajulikani ni nani. Je, uhusiano wake na hicho ambacho waziri mkuu anaita “genge la watu linalofahamika,” ni upi?

Jingine ambalo Pinda anapaswa kulifahamu ni hili: Mwenye uwezo wa kulisema hili kwa ufasaha na akatosheleza majibu ya wananchi, ni Rais Jakaya Kikwete na aliyekuwa waziri wake mkuu, Edward Lowassa.

Kikwete ndiye aliyeongoza kikao cha Baraza la mawaziri kilichopitisha maamuzi ya kuipa kazi Richmond ambayo haikuwa na uwezo wa kufanya kazi iliyoomba.

Mara kadhaa, Kikwete amekiri kwamba alikuwa anafuatilia kwa karibu shughuli za Richmond. Kuna wakati alisema aliwahi kumuagiza waziri wake kutoilipa kampuni hiyo kwa vile tayari ilidhihirika kuwa ni kampuni ya kitapeli.

Kigugumizi cha rais kushindwa kuchukulia hatua watuhumiwa wakuu wa Richmond na dada yake Dowans, kunazidi kusisitiza kuwa “Richmond ni kampuni ya wakubwa.”

Kamati Teule ilipendekeza kwa mamlaka za juu za uteuzi kuwaondoa kazini Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru), Edward Hoseah, aliyekuwa mwanasheria mkuu wa serikali, Johnson Mwanyika na aliyekuwa katibu mkuu wizara ya nishati na madini, Athur Mwakapugi.

Bunge lilitaka pia hatua za kisheria zichukuliwe kwa wote ambao walionekana wazi kutenda jinai.

Ndani ya Bunge, Hoseah alituhumiwa kuibeba Richmond. Kamati Teule ilisema Hoseah aliaibisha serikali kwa kusema, “Mkataba ulikuwa halali na hakuna harufu ya rushwa ndani yake.”

Hadi sasa, Hoseah hajajiuzulu, wala rais Kikwete hajamfuta kazi. Badala yake rais alimteua kwenye kamati yake ya kufuatilia walioiba Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Johnson Mwanyika kama ilivyokuwa kwa Hoseah, naye alibaki katika nafasi yake hadi alipotimiza muda wake wa kustaafu. Naye aliingizwa kamati ya rais ya kufuatilia mafisadi waliokwapua mabilioni ya shilingi BoT.

Kosa la Mwanyika ni kushindwa kushauri serikali; kuzembea katika usimamizi wa mkataba; na kushindwa kuangalia maslahi ya umma katika mkataba.

Kimsingi uzembe wa Mwanyika, iwapo hakutenda hayo kwa maelekezo ya juu, ndiyo yaliosababisha serikali kulipa fedha hizo.

Naye Lowassa alitajwa kuwa ndiye aliyekuwa akiagiza, kushinikiza na ndiye aliyeibeba Richmond na kuifikisha hapo ilipofika.

Mathalani, baadhi ya nyaraka zinaonyesha aliyekuwa waziri wa Nishati na Madini, Dk. Ibrahim Msabaha, alibakia kama karani wa kutekeleza maagizo ya Lowassa.

Akitii kile alichoita maagizo ya Lowassa, 21 Juni 2006, Dk. Msabaha aliandikia Mwakapugi akisema, “…Andaa barua kwa mwenyekiti wa bodi ya Tanesco kumuagiza aingie mkataba na Richmond haraka iwezekanavyo. Nakuletea nakala ya kibali kutoka ofisi ya Mhe. Waziri Mkuu kwa kumbukumbu za wizara.”

Lakini kama haya ndiyo maagizo ya Dk. Msabaha kwa Mwakapugi, nani aliyeagiza Lowassa kuipa kazi Richmond? Maana kwa vyovyote vile, Lowassa hawezi kutenda haya peke yake.

Ni Msabaha anayedaiwa kuandika katika baadhi ya nyaraka kuwa “suala la kushughulikia mashine za umeme wa kukodi limekwisha kushughulikiwa na waziri mkuu Lowassa?”

Je, kwa nini Lowassa ajipe kazi hii wakati kazi ya kutafuta mashine hizo ilikuwa ya kitaalamu na Lowassa si mtaalamu wa masuala ya umeme?

Aidha, kama hayo ndiyo maagizo ya Lowassa kwa Dk. Msabaha, kwa nini waziri Msabaha aliyatekeleza wakati alijua wazi kuwa tayari kuna walakini wa uhalali na uwezo wa Richmond?

Mashaka ya uwezo wa Richmond kumudu kufanya kazi yanadokezwa na kauli ya Lowassa katika barua yake ya 21 Septemba 2006 kwenda kwa Dk. Msabaha.

Lowassa katika barua hiyo anasema, “…Yapo maneno mengi sana yanasemwa kuhusu uwezo wa Richmond kuagiza Gas Turbines... Inawezekana hivi vikawa ni vita vya kibiashara… Ni vizuri ukajiridhisha kwamba kampuni hii itaweza kutekeleza kazi hiyo…”

Kujitosa kwa Lowassa katika sakata la Richmond/Dowans halipo kwenye kuagiza Dk. Msabaha na Timu ya Majadilino ya Serikali (GNT) pekee.

Barua ya Msabaha ya 17 Juni 2006, siku sita kabla ya mkataba wa Richmond kusainiwa, inaonyesha alivyoelezwa jinsi majadiliano yalivyokwenda hatua kwa hatua kati ya GNT na Richmond na jinsi utekelezaji wa mkataba utakavyokuwa.

Lowassa alijulisha yote aliyoyatenda kwa rais Kikwete. Je, Kikwete alichukua hatua gani mpaka sasa wanataka kulipa “kikundi hiki kidogo cha watu” mabilioni ya shilingi?

Lakini kuna jingine: Baada ya serikali kujiridhisha kuwa Richmond haiwezi kutekeleza mkataba wake iliyofunga na Tanesco 23 Juni 2006, baadhi ya vigogo serikalini walishinikiza kampuni hiyo kuhuisha mkataba wake kwa Dowans.

Je, nani aliyemtuma Nazir Karamagi kufanya kazi hiyo na kwa faida ya nani wakati ambapo mkataba kati ya Tanesco na Richmond ulikuwa tayari umevunjika? Ni vema Pinda ataje aliyemtuma Karamagi.

Kwa inavyoonekana, Karamagi hakuwa peke yake. Je, alishirikiana na nani? Nani alimuagiza? Rais Kikwete, Lowassa au alitenda hayo kwa shinikizo la Rostam Aziz?

Jingine ambalo linahitaji ufafanuzi ni hili: Wakati Richmond inaomba kazi iliyopewa, haikuwa na fedha za kuendesha mradi. Huo ndiyo msingi wa kutaka serikali iidhamini kwa kufungua LC – dhamana.

Kamati Teule ya Bunge imethibitisha; Karamagi aliyesimamia uhamisho wa mkataba naye amekiri pia, kwamba Richmond haikuwa na  uwezo, ujuzi wala fedha za kufanya kazi iliyoomba.

Sasa kwa nini serikali inataka kulipa watu ambao hawakuwa na fedha?

Ni lazima Pinda afahamu kuwa huwezi kuitenganisha Richmond na Dowans. Hii ni kampuni inayomilikiwa na watu walewale, lakini walioamua kuzitambulisha kwa majina mawili tofauti.

Ushahidi wa hilo ni jinsi Richmond ilivyoruhusiwa kuhuishaji mkataba wake.

Hakuna mahali popote panapoonyesha Richmond iliwahi kutangaza tenda ya kutafuta mbia; badala yake yote yaliyofanyika yalitendeka kwa siri na yakishirikisha baadhi ya viongozi serikalini.

Kwa mfano, kwa nini Karamagi alihamisha mkataba wa Richmond kwenda Dowans, wakati tayari kampuni hiyo ilishindwa kazi; mvua tayari zilishaanza kunyesha na mabwawa kujaa?

Hoja kuu ambayo Pinda na wenzake wanasimamia katika kuhahalalisha malipo ya Dowans, ni “serikali hii inafuata misingi ya sheria.”

Lakini serikali inayofuata misingi ya sheria, haijalipa fidia wananchi wake hata baada ya kushinda kesi mahakamani.

Tokea mwaka 1986 wananchi wa kijiji cha Kitondoloni, wilayani Kisarawe mkoani Pwani, walihamishwa ili kupisha kilichoitwa “shughuli za jeshi.”

Kupitia waziri wa fedha wa wakati huo, Kighoma Malima, serikali ilikubali kuwalipa stahiki zao, lakini hadi leo hii ahadi ya serikali haijatekelezwa.

Hata baada ya hukumu ya Jaji Khamisi Msumi ya 18 Novemba 1996, iliyowapa haki yao ya kufidiwa, bado serikali haijawalipa Ally Mwang’omba na wenzake 143 katika kesi Na. 144 ya mwaka 1996.

Ni serikali hii, ambayo Pinda anasema inafuata utawala wa sheria iliyogoma kulipa wafanyakazi zaidi ya 40 wa lililokuwa Shirika la Bima la Taifa (NIC) waliosimamishwa kazi tokea mwaka 1998.

Kesi ya watumishi hawa ambayo hata baadhi ya wafanyakazi wa serikali waliipachika jina la “kesi ya kuchonga,” ilichukua miaka 11 na ilifutwa mapema mwaka huu kwa kile serikali ilichoita, “Hakuna tena sababu ya kuendelea na shauri” hilo.

Katika kipindi chote hicho, wafanyakazi hawa walikuwa wanalipwa nusu mshahara. Baadhi yao wamefariki. Lakini serikali imegoma kulipa hata vizuka.

Wapo ambao watoto wao wameshindwa kwenda shule kwa kuwa wazazi wao hawana tena kipato na Pinda na serikali yake imegoma kuwalipa. 

Orodha ya kesi ambazo zimeamuliwa mahakamani, lakini serikali haijalipa wanaostahili, ni nyingi na nzito hata kuliko Dowans.

Tokea mwaka 1989 serikali imeshindwa kumlipa mfanyabiashara Devram P. Valambhia. Hata pale iliposhindwa katika mahakama ya rufaa kwa zaidi ya mara 10 bado serikali iliendelea kugoma kulipa fedha hizo hadi akaaga dunia akiwa masikini na dhaifu.

Kama haya yalifanyika kwa Valambia, kwa nini serikali isiyafanye kwa Dowans? Au ni kweli kwamba Dowans ni ya vigogo ambao wanadai wameiweka serikali kiganjani?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: