Nani atafuata nyayo za Pinda?


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 04 February 2009

Printer-friendly version
Tafakuri

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Mizengo Pinda, amejiandikia historia kwa kufanya mambo mawili makubwa.

Kwanza, alisimama bungeni na kuomba radhi wananchi na taifa. Pili, alimwaga chozi mbele ya wabunge na mbele ya wananchi.

Radhi na chozi la waziri mkuu vilitokana na hoja ya mbunge wa Wawi, kisiwani Pemba, Hamad Rashid Mohammed (CUF). Hamad alitaka Pinda kutoa ufafanuzi juu ya kauli yake aliyoitoa wiki mbili zilizopita mkoani Tabora.

Akiwa Tabora, Pinda alitaka wananchi kutosubiri vyombo vya sheria kuchukua mkondo wake. Alitaka wananchi kuwasaka na kuwauwa wale alioita, “wauwaji wa albino.”

Akiongea kwa kunyenyekea, Pinda aliliambia Bunge kwamba hakutoa kauli hiyo kwa nia mbaya. Alisema alifanya hivyo kwa nia ya kukomesha mauaji ya albino yaliyotapakaa kila pembe ya nchi.

Alisema, "…Nilidhani kwa kufanya hivyo, kutasaidia kutisha wahusika na mauwaji yatapungua…Lakini nia yangu ilikuwa nzuri kabisa. Nilitaka mauaji yakome. Hivyo basi, kama nimekosa naomba sana mnisaheme," alisema Pinda huku akimwaga chozi.

Mengi yamesemwa na kuandikwa tangu Pinda aombe radhi Bungeni. Wapo waliompongeza na wapo waliombeza.

Baadhi ya wanaombeza wanasema, Pinda hakumwaga chozi kwa sababu ya huruma yake kwa albino bali alikuwa analilia uwaziri mkuu wake ili usimponyoke. Inawezekana.

Ukweli ni kwamba amri ya Pinda ilikuwa na utata. Kuwinda na kuadhibu wanaodaiwa kuua bila kuwafikisha katika chombo cha sheria, ni hatari. Wengi wangeuawa kwa visingizio ikiwa ni pamoja na albino wenyewe kwamba walikuwa wanaongoza wauaji.

Hata hivyo, jambo ambalo haliwezi kupingika hadi sasa, ni kwamba Pinda amekuwa kiongozi wa kwanza kutoka ngazi ya juu serikalini kuomba radhi Bunge na taifa na kumwaga chozi hadharani kujutia alichosema na kusisitiza alichodhamiria.

Lakini jambo la kuomba radhi si dogo. Linastahili kuigwa na viongozi wengine; kujutia ulichofanya au ulichosema. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kwa muda mrefu wananchi wameshuhudia taifa lao likitawaliwa na viongozi wababe, jeuri, wenye kibri na dharau ya kiwango kikubwa.

Baadhi yao walifikia kujitangaza kuwa miungu watu. Wengi wao wametoka katika utumishi wa umma na kujibandika utawala.

Mifano katika hili iko mingi. Ni aliyekuwa Waziri Mkuu Cleopa Msuya anayekumbukwa kwa kutoa kauli za kukatisha tamaa wananchi.

Wakati wananchi kutoka kila pembe ya nchi wakilia na kusaga meno; wakilalamikia kero mbalimbali zilizosababishwa na serikali ikiwamo kodi ya maendeleo, Msuya alitoa kauli za kebehi dhidi ya raia.

Hata pale ambapo wabunge walitaka kauli ya serikali kuhusiana na kero hizo, Msuya hakujali. Badala yake alisema, “Kila mtu atabeba mzigo wake.”

Matokeo yake, wananchi wakajenga chuki na mashaka dhidi ya serikali yao. Wengi wakaanza kujiuliza, “tunaelekea wapi? Mbona tuliowapa mamlaka wameanza kutugeuka?”

Mwingine ni rais mstaafu, Benjamin Mkapa. Huyu kauli zake bado zinakumbukwa na wengi. Akiwa mkoani Singida, Mkapa alitoa kauli za kejeli dhidi ya vyombo vya habari vinavyokosoa utendaji wa serikali yake.

Mkapa alisema, kabla ya vyombo hivyo vya habari kuchokonoa watendaji wa serikali yake, ni lazima kwanza wamiliki wake wataje walikopata fedha za kuanzishia vyombo hivyo.

Hakuishia hapo. Alikemea hata wananchi waliokuwa wanahoji uadilifu wa aliyekuwa waziri mkuu wake, Frederick Sumaye. Akiwa nchini Boswana, Mkapa alisema kwamba wanaomtuhumu Sumaye “wana wivu wa kijinga.”

Wala Mkapa hakutaka kujihangaisha kuchunguza kile kilichokuwa kinasemwa. Inawezekana tuhuma dhidi ya Sumaye zilikuwa na ukweli.

Inawezekana Mkapa alilijua hili. Hata hivyo, alipaswa kuwaachia wananchi wenyewe kupima ukweli wa kile kilichokuwa kikiandikwa.

Mwingine aliyejitokeza kwa kauli za kebehi na kejeli alikuwa Pius Msekwa; wakati huo akiwa spika wa bunge. Huyu alisema, “Watu waache wivu wa kike.”

Msekwa alikuwa akijitetea kwa kupewa nafasi ya uenyekiti wa bodi ya wakurugenzi katika kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom wakati akiwa bado Spika.

Wakati huo pia Katiba ilikuwa bado inatamka kuwa wakati rais na makamu wake hawapo, ni jaji mkuu au spika wa bunge anayekaimu urais.

Hoja mbili zilijengwa: Kama spika wa bunge anakuwa mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa kampuni binafsi; na hoja ya kampuni husika inaletwa bungeni, vipi spika atashughulikia hoja hiyo? 

Ilifafanuliwa kuwa bila shaka, spika au rais anayekuwa mwenyekiti wa bodi ya kampuni binafsi anaweza kutumia nafasi yake kupendelea kampuni yake na hivyo kulikuwa na mgongano wa maslahi. Msekwa hakujutia kuwa na mgongano wa maslahi. Aliishia kufanya kejeli.

Kuna Andrew Chenge. Akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Chenge alituhumiwa na wabunge kuingiza maneno katika sheria ya kuvunja Benki ya Taifa ya Biashara (NBC). Ilikuwa katika mchakato wa kubinafsisha NBC na kuunda National Microfinance Bank (NMB).

Katika moja ya vifungu, ofisi ya mwanasheria mkuu iliingiza kifungu kinachoitaja National Bureau kuwa mali ya NBC Limited, badala ya kubaki kitu kinachojitegemea.

Hoja ililetwa bungeni na mbunge Philip Magani. Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria, chini ya mbunge wa Muhambwe, Kibondo, mkoani Kigoma, Arcardo Ntagazwa, ilichunguza suala hilo na kuwasilisha ripoti yake bungeni.

Kamati ilisema ni kweli kwamba ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ilivunja sheria kwa kujipa jukumu la bunge. Serikali iliomba radhi.

Lakini Chenge alipopewa nafasi, hakuomba radhi bunge. Badala yake alikejeli kwa kusema, “Kiti cha mwanasheria mkuu wa serikali kimejaa.”

Orodha ya wasiojutia kauli au matendo yao ni ndefu. Lakini itoshe tu kusema kwamba Pinda amejitofautisha na wenzake. Inawezekana hatua yake ilitokana na kusoma alama za nyakati.

Pinda alijua asipochukua tahadhari na kushughulikia suala hilo kwa makini, wabunge wangeweza kumsulubu. Aliogopa yasije yakamkuta yaliyomfika Edward Lowassa, aliyekuwa waziri mkuu kabla yake.

Hata hivyo, Pinda amedhihirisha kuwa mtumishi anayejali anaowatumikia. Amevaa sura ya utumishi badala ya utawala. Katika siasa, hili si haba!

Je, msululu wa mawaziri wanaokabiliwa na mikingamo ya aina hiyo wako tayari kunyenyekea kwa umma kama Pinda?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: