Nani atafungiwa "hotelini?"


Stanislaus Kirobo's picture

Na Stanislaus Kirobo - Imechapwa 12 August 2008

Printer-friendly version

MAPEMA wiki iliyopita, magazeti mawili yaliandika habari za kufanyika ukarabati wa vyomba vya magereza katika gereza kuu la Ukonga, jijini Dar es Salaam.

Ilielezwa kuwa lengo ni kuweka mazingira ya kuwafungia vigogo wanaokabiliwa na makosa makubwa.

Watu makini wameanza kujiuliza; hivi serikali inaweza kufanya hili" Au inafanya geresha ili wananchi waiamini kwamba inashughulikia ufisadi wakati haina ubavu huo"
 
Kuna uwezekano kwamba taarifa za ukarabati wa selo zilivujishwa kwa makusudi kama mbinu za serikali.
 
Swali jingine ni hili. Je, kwa nini watuhumiwa vigogo watengewe selo maalum katika magereza" Kwa kigezo gani" Sheria au kanuni ipi? Hivi uzito wa wizi wa mali ya umma unapimwa kutokana na matabaka katika jamii"

Kwamba wezi wa kuku wanastahili kuwekwa mahali pagumu, lakini wezi wa mabilioni ya walipa kodi wawekwe mahali laini mithili ya hoteli.

Na kwa nini serikali ianze kutangaza "matayarisho" ya ujio gerezani wa "tabaka" hilo la wezi? Ina maana ndiyo inaanza sasa kuwashughulikia? Kwamba huko nyuma hakukuwa na vigogo wahalifu?
 
Wapo wasioamini kama "ukarabati" huo upo, mimi nikiwamo. Inajulikana kwamba masuala haya ya ufisadi yanawaandama watu wakubwa sana wa serikali na katika chama tawala.

Ni masuala mazito ambayo yakidhihirika yanaweza kudhalilisha serikali na hata baadhi ya marafiki wa karibu wa rais Kikwete.

Vilevile ni masuala ambayo ukweli wake ni bora ukabakia katika hisia tu mwa umma ? hasa ile hisia  inayozungumzwa sana na ambayo wengi wanaamini hakika ilikuwa hivyo.

Kwamba sehemu ya mabilioni yaliyoibwa Benki Kuu (BoT) kupitia Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) yalitumika katika kampeni za uchaguzi za mwaka 2005.

Kwamba kuna watu wengine walitumia mwanya huo kujichotea na kuichangia CCM.

Kutokana na jinsi fedha zinavyodaiwa kutumika katika kampeni za CCM, na kutokana na ukweli kwamba CCM hakiwezi kuthibitisha kwa njia yoyote ile kilipopata fedha kilizotawanya nchi nzima wakati huo, hilo nalo linabaki kitendawili.
 
Wale wenye ujasiri wa kiasili wamejaribu sana kusaidia kutuonyesha ukweli ulipo, ingawa hawa hupigwa vita kali kutoka kwa baadhi ya wahusika wa ufisadi na hasa kwa kupitia mawakala wao.

Tumeona baadhi ya magazeti yanavyoripoti habari za ufisadi kwa namna ya upotoshaji unaoonyesha usaliti mkubwa kwa taifa.

Kwa mfano, wiki iliyopita gazeti moja liliandika habari inayojaribu kuufanya umma uamini kuwa "EPA ni cha mtoto," ufisadi hasa umejikita katika chama cha upinzani cha CHADEMA.

Gazeti limejaribu kuonyesha jinsi ruzuku ya Sh. 60 milioni kinazopata chama hicho kila mwezi kutoka serikalini zinavyotumika vibaya.
 
Utalinganishaje Sh. 60 milioni, mali ya CHADEMA zilizotumiwa na CHADEMA yenyewe; na ufisadi wa Kagoda wa kukwapua zaidi ya Sh. 30 bilioni kutoka BoT?

Hakika CHADEMA wanatumia fedha zao; lakini Kagoda wamechukua fedha za umma, kwa udanganyifu na kwa kazi isiyofahamika.

Sasa kuna wasiwasi kwamba watu mashuhuri watakaoanza kukamatwa hawatakuwa wezi wa EPA, bali ni watu wengine kabisa wasiohusika " na hasa wale wanaoonekana "wapiga filimbi" wa ufisadi huo. Wananchi wanasubiri kuona maajabu.
   
Rais Kikwete ana wajibu mkubwa wa kuhakikisha haki inatendeka katika suala hili. Serikali yake isije kufunga wezi wa nyanya na kuacha wanaoua taifa kwa ufisadi usiomithilika.

0
No votes yet