Nani ataokoa Kikwete?


Nkwazi Mhango's picture

Na Nkwazi Mhango - Imechapwa 04 November 2009

Printer-friendly version
Uchambuzi

UKIANGALIA jinsi mambo yanavyokwenda, utaona kama vile Rais Jakaya Kikwete hajali kutumbikiza serikali yake katika kashfa.

Angalia jinsi watendaji wa serikali wanavyotafuta kila njia kuokoa watuhumiwa wa ufisadi na kujiokoa wao wenyewe. Angalia jinsi ambavyo serikali ilivyobeba kampuni tata ya kufua umeme kati ya serikali na kampuni ya Richmond Development Company (LLC) ya Marekani.

Angalia jinsi serikali inavyoshindwa kushughulikia ufisadi uliofanywa na kampuni ya Kagoda Agriculture Limited, iliyochotewa na serikali na washirika wake mabilioni ya shilingi miezi miwili kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.

Hata pale wakili wa Mahakama Kuu, Byidinka Michael Sanze aliponukuliwa katika hati yake ya kiapo, kwamba Rostam ndiye aliyemtaka kushuhudia hati za mikataba ya Kagoda, Kikwete ameshindwa kuchukulia hatua madai hayo.

Kampuni ya Kagoda ilichota zaidi ya Sh. 40 bilioni katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Hii inaonyesha kwamba taifa hili limekumbwa na gonjwa hatari la wakubwa kuonea wadogo katika karibu kila mahali.

Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa nchini (TAKUKURU inasifika kwa kuwaandama wafanyakazi wa kada ya chini, hasa polisi, mahakimu wa mahakama za mwanzo, walimu, manesi na wengine.

Tuhuma hizo tayari zimefanya baadhi ya wanachi kuona kuwa taasisi yao hiyo nyeti, inatumiwa na wakubwa kulinda watuhumiwa na kutisha wale wanaothubutu kufichua maovu.

Na kwamba Takukuru kama ilivyotaasisi nyingine za umma, mkurugenzi wake anateuliwa na rais, na kwamba ni rais mwenye uwezo wa kumfuta kazi.

Acha hilo. Angalia hili la mgawo wa umeme. Rais haonekani kulishughulikia kikamilifu.  Amesahau kuwa “Maisha Bora kwa kila Mtanzania” hayawezi kupatikana kama nchi yote itakuwa gizani kila siku na kwa wakati mmoja.

Maisha bora yatapatikana iwapo taifa litakuwa na nishati hiyo muhimu kwa uchumi na maisha ya kila siku ya mwanadamu.

Ni aibu kwa mfano, nchi ndogo kama Uganda yenye raslimali na vyanzo vidogo vya maji kuuuzia umeme Tanzania.

Kama kuna nchi ilipaswa kuwa na mgao wa umeme kama kweli tatizo lingekuwa ni upungufu wa maji, basi ni Kenya. Lakini wakati tukiishi kama bundi kwenye giza wenzetu wa Kenya wanatucheka hadi kutukumbusha la kufanya kwa kutoa vibonzo vyenye manufaa kwetu.

Lakini achana na hilo. Angalia hili lililoibuka sasa ambapo baadhi ya mawaziri wa serikali ya Kikwete wanatuhumiwa kughushi vyeti vya taaluma.

Kisheria, kujitambulisha tofauti na ulivyo ni kosa la jinai. Hata kuwasilisha hati za kughushi kwa mamlaka yeyote ni kosa kisheria ukiachia mbali kujipatia marupurupu na mshahara kwa kazi ambayo huna ujuzi wala sifa nazo.

Hapa tutaambiwa ubunge si kazi ya kusomea. Je kuwadanganya wananchi, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na taifa kwa ujumla na kujipatia mshahara kutokana na sifa usizokuwa nazo si kosa?

Hili la kugushi vyeti lilianzia kwa mbunge wa Bushosa, Samwel Chitalilo (CCM). Chitalilo anatuhumiwa kughushi vyeti na kuwadanganya wapiga kura kama ilivyothibitishwa na Jeshi la Polisi.

Kinachokera ni Chitalilo kujifedhehesha kama mbunge, ukiachia mbali wapigakura wa Buchosa.

Tuhuma za Chitalilo ziliibuliwa na mshindani wake wa kisiasa ndani ya chama chake. Huyu ndiye aliyekusanya nyaraka na kuziwasilisha kwenye vyombo vya dola.

Hata hivyo, pamoja na ushahidi wote uliokusanywa, Chitalilo hajawahi kuonywa wala kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria. Badala yake, Rais Kikwete alisikika akiwa akiwa jimboni Bushosa akisema, “kelele za wapangaji haziwezi kumnyima usingizi mwenye nyumba.”

Hivyo, kutokana na uzito wa rais na mwenyekiti wa chama kesi iliishia hapo. Ajabu, umma wa Watanzania haukuchukua hatua kumshinikiza rais kuomba msamaha kwa kushiriki jinai ukiachia mbali kutochukua hatua kama mwenyekiti wa CCM – chama ambacho Chitalilo anatoka.

Tufike mahali tumkabili rais bila woga. Kashfa dhidi ya serikali yake na chama chake zimezidi. Rais amekaa kimya na anaonekana hataki kuchukua hatua.

Sasa mawaziri sita wanatuhumiwa kughushi vyeti na sifa hasa za shahada ya uzamivu ya falsafa (Ph.D), wakati hawajawahi kusomea shahada hizio. Lakini rais haonekani kuguswa na jambo hilo.

Je, taifa linaweza kupata maendeleo wakati linaongozwa na watu walioghushi au matapeli huku mamlaka za juu katika nchi zikiwa zimenyamaza bila sababu? Katika mazingira haya serikali itawezaje kutimiza ndoto ya kuwapa Watanzania “Maisha Bora?”

Tayari madai mapya yameibuka na rais haonekani kuyashunghulikia. Kwamba hatua ya mkurugenzi wa Takukuru, Edward Hoseah kutaka kuhoji wabunge kwa kile kinachodaiwa kuwa wanalipwa posho mbili kwa wakati mmoja, “kumelenga kuwanyamazisha wawakilishi hao wa wananchi.”

Kama alivyosema Spika wa Bunge la Jamhuri, Samwel Sitta, kama akili ikitumika vizuri, tukalinganisha hujuma na hasara zitokanazo na Richmond na EPA, wabunge kupokea posho mbili ni sawa na kulinganisha kichuguu na mlima.

Sasa swali la kujiuliza: Kwa nini rais ameamua kukaa kimya ilhali mwakani kuna uchaguzi? Je, anataka kusema kwamba kuendelea kunyamazia tuhuma hizi ndiyo njia sahihi kuliko kukemea au kuchukulia hatua wahusika.

Rais na serikali yake haoni kuwa hatua ya kukalia kimya tuhuma hizi kutatoa nafasi kwa viongozi wa vyama vya upinzani kuendeleza madai yao ya siku zote kuwa serikali hii ni mama wa ufisadi?

Tumeona jinsi serikali ilivyofikisha haraka mahakamani wanafunzi waliotuhumiwa kughushi vyeti. Tumeona jinsi wafanyakazi wa ngazi ya chini wa BoT walivyoburuzwa mahakamani kwa tuhuma kama hizo pia.

Lakini linapokuja suala kama hili kugusa wakubwa, tumeshuhudia vyombo vya dola na serikali kwa jumla ikishindwa kufumbua mdomo.

Ni lazima serikali itambue kuwa hii si nchi ya mabwege kama alivyosema Dk. Harrison Mwakeyembe, na isitoshe mambo yamebadilika sana.

Tuhitimishe kwa kushauri serikali kuweka nukta kwenye aibu inayosababishiwa na watendaji wake kwa bahati mbaya baada ya kumdanganya rais kuwa huku nje mambo yanakwenda vema.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: