Nani atasimamia nidhamu ndani ya CCM?


Nyaronyo Kicheere's picture

Na Nyaronyo Kicheere - Imechapwa 31 August 2011

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

BINTI yangu anayesoma darasa la sita, wiki iliyopita, alinishangaa nilipokuwa nazungumza na mtu aliyevaa shati la kijani. Akahoji kwa nini nilikubali urafiki na fisadi!

Nilipomuuliza alijuaje kwamba rafiki yangu ni fisadi alijibu, “Kwani hukuona shati lake? Shati lake ni la kijani lile, yule ni CCM.” Kauli ya binti huyu mwenye umri wa miaka 13 iliniacha hoi nisijue la kusema.

Nikabaki najiuliza, amepata wapi habari kuwa watu wenye mavazi ya kijani ni mafisadi? Ameambiwa na nani kuwa mafisadi ni wanachama na wapenzi wa CCM?

Nilijiuliza pia je, mtoto huyu anayesoma bweni katika shule hizi zinazoitwa ‘intaneshino’ ingawaje hazina ‘uintaneshino’ wowote kaambiwa na walimu wake shuleni kuwa mafisadi wote ni CCM na kwamba utambulisho wao ni mavazi ya kijani?

Je, inawezekana maneno yale ya kuhusisha rangi ya kijani, uanachama wa CCM na tabia ya ufisadi kayapata mitaani anapokuja nyumbani kwenye likizo hizo fupi za mwishoni mwa wiki wanazoita wao ‘visiting day’?

Au habari za uanachama na upenzi wa CCM kuhusishwa na ufisadi zimepatikana kwenye redio na runinga zinapotangaza maandamano ya CHADEMA huku polisi wakiua watu kwa madai kuwa wanatii amri ya wakubwa?

Sikupata majibu ya maswali haya, na bado naendelea kujiuliza kama watoto wetu wamepata wapi mawazo haya kwamba CCM ni chama cha mafisadi na watu wanaovaa au wanaopendelea kuvaa mavazi ya kijani kwanza ni CCM na pili ni mafisadi?

Kwamba sasa watoto wanaosoma na wasiosoma kuchukulia suala la ufisadi limebuniwa, limetekelezwa na linadumishwa na watu wanaopendelea mavazi ya kijani na ambao wote ama ni wananchama au ni wapenzi wa chama tawala, inapaswa kuwatia hofu watawala na wana CCM.

Kwamba sasa ufisadi, uhujumu, wizi na ubadhirifu wa mali ya umma ni matatizo yanayoletwa na watawala ambao wote wameteuliwa na watawala kwa kigezo kuwa ni wanachama wa CCM inapaswa kuwatia wasiwasi wana CCM.

Wakati ningali natafakari uanachama na ukereketwa wa CCM vimepataje sifa ya kuchukiwa na watoto wa siku hizi, zikapatikana habari Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa, naye kakumbwa na kashfa.

Kwa mujibu wa habari hizo zilizotolewa bungeni, Msekwa ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCA) amekuwa akifanya mambo yanayopaswa kufanywa na mtendaji mkuu wa hifadhi hiyo kama kuruhusu ujenzi wa mahoteli ya kitalii mbugani. Tuhuma zinasema Msekwa amekuwa akifanya kiholela na kinyume cha sheria! Msekwa amepuuza madai hayo.

Kwa wasiomfahamu vizuri Msekwa, ni  yule bwana mkubwa katika CCM ambaye alipata kuwa Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri kwa miaka mingi na baadaye kuwa spika kamili akirithi nafasi ya Adam Sapi Mkwawa.

Amekuwa spika kwa miaka mingi hadi aliposhindwa katika kinyang’anyiro cha Januari 2006 kwa Samwel Sita.

Msekwa alikuwa katika kamati ya waungwana watatu walioteuliwa kuunganisha kambi mbili zilizokuwa zinasigana ndani ya kambi ya wabunge wa CCM – kundi moja la wabunge wa CCM wakipinga ufisadi na mashabiki wao na jingine la wabunge wa CCM wakituhumiwa kwa ufisadi na mashabiki wao.

Msekwa pia ndiye muungwana aliyeonekana anafaa kuwahoji watuhumiwa wakuu wa ufisadi ndani ya CCM ambao baadaye waliamriwa kujiuzulu nafasi zao za uongozi wa chama hicho tawala katika zoezi maarufu waliloliita “kujivua gamba.”

Watuhumiwa hao wanaojulikana kama “mapacha watatu” waliohojiwa na Msekwa ni aliyekuwa mbunge wa Igunga na mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM, Rostam Aziz na Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond na mbunge wa Monduli, Edward Ngoyai Lowassa. Pia yumo mwanasheria mkuu wa zamani na mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, maarufu kama mzee wa vijisenti.

Hadi hivi karibuni Chenge alikuwa mwenyekiti wa kamati ya maadili ya halmashauri kuu ya CCM!  Hapo ndipo CCM ilipofikishwa na tuhuma za ufisadi zisizokwisha.

Kila mwaka zinatolewa tuhuma za ufisadi bila uongozi wa CCM kuchukua hatua kwa watuhumiwa kiasi kwamba sasa chama hicho kinaonekana mbele ya macho hata ya watoto wa shule za msingi kuwa ni chama cha mafisadi!

Kutokushughulikia tuhuma za ufisadi na tabia ya uongozi wa CCM kuonekana kuwatetea watuhumiwa eti hakuna ushahidi wa kuchukua hatua za kisheria na watuhumiwa wengine kupandishwa vyeo wakawa wakuu wa nidhamu kwenye chama hicho ndiko kulikokifikisha chama katika hatua hii ya kuchukiwa hata na watoto wa shule za msingi!

Wakati uongozi na wanachama wa CCM wanashangaa kutokubalika kwao kwa vijana wa vyuo vikuu, kule kunakotolewa digrii, shahada za uzamili na shahada za uzamivu, stashahada na astashahada, nashangaa kutokubalika kwa CCM hata kwa watoto wa shule ya msingi na chekchea!

Siku moja Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, alinung’unikia katika mkutano CCM kukosa mvuto kwa vijana yaani wanavyuo waliokataa hadharani kukiunga mkono chama hicho, lakini sasa anapaswa kunung’unika chama chake kuchukiwa na watoto siyo wanavyuo tu.

Wanavyuo ni watu wazima wenye uwezo wa kufanya uamuzi kama chama kipi ni bora kulingana na sera na tabia ya viongozi na wananchama wake hivyo wakiamua kutounga mkono chama fulani, basi hilo linaelezeka siyo watoto wadogo.

Kufikia hatua watoto wadogo kuchukia chama cha siasa maana yake mvuto wake hauzungumziki tena, hicho ni chama kilicho katika hatua za mwisho za kusambaratika. Dalili ni hizo kuwa wanaotegemewa kuhoji watuhumiwa wa ufisadi nao wanatakiwa kuhojiwa kwa tuhuma za kuhujumu nchi!

Kama Msekwa ambaye alionekana Mr. Clean ndani ya CCM naye anatuhumiwa, nani msafi aliyebaki katika CCM atawahoji watuhumiwa waliopo ndani ya CCM waliokwiba wanyama hai na kuwapakia kwenye ndege KIA?

Nani mtu msafi CCM atakayehoji wenzake? Mtu ambaye hakuchukua nyumba za serikali kwa bei sawa na bure! Mtu ambaye hahusiki kwenye kashfa ya ndege ya rais; hahusiki kwenye kashfa ya rada; hahusiki kwenye kashfa ya migodi; Meremeta, Mwananchi Gold, Deep green, majengo pacha ya Benki Kuu; hahusiki kuiba kura; hakukodiwa ndege na Barrick?

Simwoni hata mmoja, maana CCM imefika ukingoni, imekwisha.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: