Nani dhaifu, Ndungai au Kikwete?


Kondo Tutindaga's picture

Na Kondo Tutindaga - Imechapwa 27 June 2012

Printer-friendly version
Uchambuzi

HATA baada ya juma moja kupita, bajeti ya serikali kupitishwa na mawazo ya wananchi kuelekezwa kwingine, bado napata shida kuelewa kitendo cha Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri, Job Ndugai, kumtoa nje ya bunge, John Mnyika (CHADEMA – Ubungo).

Mnyika alitolewa nje ya bunge baada ya kutamka maneno mbele ya bunge yaliyoashiria kuwa amemtukana rais wa nchi – Jakaya Mrisho Kikwete kwa kumwita “dhaifu.”

Alipotakiwa afute maneno yale kabla ya kuendelea kutoa mchango wake, aliomba apewe nafasi afafanue alikuwa anamaanisha nini. Alipolazimishwa afute bila kufafanua, alisema hawezi kufuta maneno hayo; na ndipo amri ya kumtoa nje ikatolewa.

Mengi yamesemwa baada ya hapo na sitaki kuingia undani wa yaliyosemwa na wengine.

Swali langu la msingi katika makala hii ni: Neno “udhaifu” limekuwaje tusi kwa mtu yeyote, ukiacha mbali kwa Ndugai na rais wetu?

Huko nyuma niliwahi kuandika katika safu hii nikijadili dhana ya “udhaifu wa Kikwete na ubaya wa Lowassa.”

Nilisema wakati ule kuwa taifa letu lina rais dhaifu wa kufanya maamuzi magumu, anayekumbatia uswahiba kuliko misingi ya uadilifu na utendaji, na kwamba, rais wetu si mpole bali ni dhaifu.

Unaoitwa uungwana na ustaarabu wa rais ni kejeli anayopewa na marafiki zake wanaofaidi udhaifu wake wa kutofanya maamuzi magumu.

Dhana hii ya udhaifu wa rais kimaamuzi siyo tu kuwa imeenea miongoni mwa watendaji wakuu, bali hata washauri wake wa karibu wamefikia kujenga uhasama na baadhi ya marafiki wa rais wanaoendekeza kumwita muungwana na mstaarabu bila kumsaidia kufanya maamuzi magumu.

Baadhi ya marafiki zake hao hivi sasa “wamewekewa ngumu” katika jitihada zao za kuonana naye kwa sababu washauri wa rais wanaona hawamsaidii wakati jahazi linazama.

Wakati wa sakata la David Jairo, yule aliyekuwa katibu mkuu wa wizara ya nishati na madini; na hasa baada ya ikulu kuamuru arejeshwe kazini, Ndugai aling’aka akidai kuwa kama ni uzembe ufanyike “hukohuko” na si bungeni.

Ilikuwa ni wakati wa hoja za wabunge kutaka iteuliwe kamati maalum kuchunguza sakata hilo. Baadaye usiku huo, nikiwa na baadhi ya wenzangu, tulikutana na Ndugai na kumuuliza alikuwa ana maana gani kusema hayo mambo yafanyike “hukohuko.”

Mheshimiwa Ndugai bila kusita alitanabaisha kuwa alimaanisha hukohuko serikalini na hasa ikulu ambako mambo yanakwenda “ovyoovyo.”

Alilalamika kuwa serikali hii inataka kulichezea bunge na kuwa yeye binafsi kama sehemu ya uongozi wa bunge hayuko tayari kukubaliana na udhaifu huo.

Sikuamini macho yangu wiki iliyopita nilipomwona Ndugai akitokwa na pofu mdomoni kushinikiza Mnyika atolewe nje ya lango la bunge.

Huu ni udhaifu mkubwa kwa Ndugai, na sidhani kama nimemtusi kwa kusema hivyo kwa sababu, wiki iliyopita alionekana wazi kutekeleza kitu asichokiamini toka moyoni mwake.

Tabia ya viongozi na watendaji wetu kulalamika nyuma ya migongo ya wakuu wao, haiwasaidii wakuu wao wala wao wenyewe wanaolalamika.

Alichokifanya Mnyika bungeni ilikuwa kuvunja ukimya na kusema kile wanachokisema wengi maofisini na kwenye mijadala isiyo wazi.

Kama kuna alilofanya Mnyika, basi ni kuanika wazi, kile kinachoaminika kuwa msingi wa matatizo ya taifa letu kwa miaka sita iliyopita. Kama Ndugai angemuacha Mnyika afafanue kauli yake ilikuwa na maana gani, angekuwa amelitendea haki taifa.

Utamaduni wa kutosema kweli au kufumbafumba mpaka kupoteza maana nzima ya kile kinachomaanishwa, inawadhalilisha wabunge wetu bila kubadili hali ya maisha ya wananchi waliowachagua. Tabia hii haimsaidii hata kiongozi wetu anayeitwa dhaifu.

Ni sawa tu na mtoto mwenye tabia ya kukojoa kitandani, ambaye mama yale alichukizwa na tabia yake akamwita kikojozi. Mtoto huyo akalia sana na kulalamika kuwa mama yake amemtukana.

Baba yake alipokerwa na kelele za mtoto, alimwita na kumpakata. Kisha akaanza kumwuliza kwa nini analia.

Mtoto akasema kuwa mama yake amemwita kikojozi. Baba yake akampoza kwa kumwambia, “…pole mwanangu, wewe siyo kikojozi ila unakojoa kitandani.”

Mtoto aliacha kulia na kuanza kucheka kisha akaondoka kwa furaha kwa kuwa amebembelezwa na baba yake.

Maneno ya baba kwa mtoto anayekojoa kitandani hayakubadili tabia ya mtoto huyo. Na ndivyo Ndugai asivyoweza kuibadili tabia ya udhaifu wa kiongozi wetu asiyefanya maamuzi magumu kwa kumtoa nje Mnyika.

Mbunge Mnyika alitoka nje akimuacha rais wetu na udhaifu wake, akarejea tena ndani ya jengo la bunge na kuukuta tena huo udhaifu wa rais.

Nimekuwa nawasikia wabunge wengi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakimlalamikia mbunge Tundu Lissu kuwa ana ujumbe mzuri, lakini anausema kwa maudhi sana.

Hata baadhi ya mawaziri wamefikia kuanzisha kampeni maalum kwenye baa za pombe kuwataka wabunge wa CCM kumzoea Lissu kila anapopata fursa ya kuchangia chochote bungeni.

Kinachowaudhi wabunge hao, si uwongo wa Tundu, bali ni ukweli wa maneno yake lyanayowasilishwa kwa kile wanachoita “namna mbaya.” Kwao, ukweli sharti upakwe sukari ili usimuumize mpokeaji.

Bunge letu limegeuzwa kituo cha kutolea nasaha ambako, wahudumu wamebobea kuupaka ukweli sukari hadi mgonjwa anapokea habari za kifo chake kwa kushangilia.

Wakati mwingine, wagonjwa mahututi hujengewa matumaini bandia na hata kudiriki kuanza kupanga mipango ya miaka kumi mbele wakati wamebakiza saa chache kuaga dunia.

Nilipoongea na baadhi ya marafiki zangu, wakiwamo watu wazima ninaowaheshimu sana ndani ya bunge na serikali, waliniambia kuwa Mnyika amesaidia sana kusema kile ambacho wao hawawezi kukisema ndani ya vikao vya chama; wala ndani ya baraza la mawaziri kisha wakabaki salama.

Nikagundua kuwa kile kilichosemwa na Mnyika na kutafsirika kama tusi kwa rais na Ndugai, si tusi kwa rais bali ni tusi kwa Ndugai asiyezoea kusikia wala kusema ukweli hadharani.

Huu ni ukweli ambao unazungumzwa na balozi zote za nje hapa nchini, vyombo vyetu vya dola, mihimili yote ya dola na hata maadui zetu wanajua ukweli huu.

Spika Samwel Sitta aliwahi kuudokeza ndani ya bunge pale alimpomsihi rais aongeze ukali kidogo au alete bungeni muswada maalum wa kumwongezea makali ya kufanya maamuzi magumu. Matamshi yale yanamgharimu mpaka leo!

Matamshi ya sasa yamemgharimu Mnyika kwa adhabu ya siku moja; lakini kibaya zaidi, kutoyasema na kuyashughulikia, kunaligharimu taifa zima, siyo kwa siku moja, bali hata kwa karne nzima au zaidi.

tutikondo@yahoo.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: