Nani dhaifu: Rais au Mnyika?


Mohamedi Mtoi's picture

Na Mohamedi Mtoi - Imechapwa 27 June 2012

Printer-friendly version“NASIKITISHWA na jambo moja. Tumefika hapa kutokana na udhaifu wa Rais Kikwete, uzembe wa bunge na wabunge; na tumefika hapa kutokana na upuuzi wa CCM. Nasemahivi, nina uhakika…”      John Mnyika, Mb.     (CHADEMA, Ubungo)

JOHN Mnyika amekisema kile kinachosemwa na baadhi ya wananchi wenye ujasiri. Tofauti yake na yetu ni kwamba, yeye kasemea bungeni; sisi tunasemea vijiweni tukinywa kahawa. Kama hivi sivyo basi, Mnyika ndio mdhaifu kwa kutoa kauli kame bila kuichuja.

  • (Bali) Kama udhaifu ni kutokujua kwa nini wananchi wako ni maskini wakati wako (katika) nchi tajiri, Mnyika yuko sahihi.
  • Kama huwezi kumuwajibisha au  kuona madudu ya katibu mkuu au katibu kiongozi mpaka bunge lishikilie bango na kushinikiza wang'oke ndio uzinduke kufanya maamuzi, basi Mnyika yuko sahihi.
  • Kama kweli watu wameliibia taifa kupitia dili za magumashi halafu una watangazia warejeshe fedha ili wasichukuliwe hatua; na wakati huohuo vibaka wanauawa au kuchomwa moto kwa kuiba kuku na simu, basi ni dhahiri kuna udhaifu wa kiuongozi, Mnyika yuko sahihi.
  • Kama ndege inaingia kwenye anga ya nchi yako na kubeba wanyama kupeleka Arabuni bila hatua zozote kuchukuliwa, ni dhahiri kuna udhaifu wa kimfumo uliokubuhu serikalini; Mnyika yuko sahihi.
  • Kama rais anafunga safari kwenda kuomba misaada na wakati huohuo misaada anayopewa hailingani thamani na raslimali zinazovunwa kwenye nchi yake; basi Mnyika yuko sahihi.
  • Kama rais anadiriki kutoa ahadi 99 ambazo thamani yake ni zaidi ya trilioni 9 huku akijua kuwa hazitekelezeki, ni hadaa kwa wananchi, chama na serikali. Hapa Mnyika yuko sahihi.
  • Kama taasisi ya ikulu na mfumo wake wa utawala umehusika kuingilia maamuzi ya mhimili wa haki kwa kutoa hukumu ya upendeleo ili kumkomoa au kumnyang'anya mbunge wadhifa, kama ilivyolalamikiwa; Mnyika yuko sahihi.
  • Kama serikali inatenga 70% kwa matumizi kwenye bajeti yake na 30% kwenye maendeleo; ni dhahiri kuwa ni aina ya serikali dhaifu yenye viongozi wavivu wa kufikiri.

Kama hivyo ndivyo, nasimama na kijana mwenzangu kwa ukakamavu na kupaza sauti yenye mwale mkali. Namuunga mkono Mnyika.

mouddymtoi@gmail.com at mabadilikotanzania@googlegroups.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: