Nani hana imani na Pinda, wabunge au Rais?


Kondo Tutindaga's picture

Na Kondo Tutindaga - Imechapwa 25 April 2012

Printer-friendly version

WAKATI naandika makala hii, Watanzania wengi walikuwa wanasubiri kwa hamu tamko la serikali kutoka kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda. Tamko hilo linahusu hatima ya mawaziri wanane wanaotajwa kwenye vyombo vya habari kuwa wamejiuzulu ili kumwokoa yeye Pinda asipigiwe kura na wabunge ya kukosa na imani naye.

Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kikao chao na kupitia pia kamati ya wabunge waliwataka mawaziri hao wajiuzulu kwa sababu wizara zao zimeshindwa kutatua kero mbalimbali za wananchi na kusababisha maisha magumu kila mahali. Ugumu wa maisha umesababishwa pamoja na sababu nyingine nyingi, ikiwamo ya ufisadi wa kupindukia katika wizara hizo.

Wakati tamko la Pinda likisubiriwa kwa hamu sana, zipo tetesi kuwa Rais Jakaya Kikwete amesita kukubaliana na kujiuzulu kwa mawaziri wake hao kwa sababu kadhaa.

Binafsi nashindwa kujizuia kuziamini tetesi hizi kwa sababu zinataja mambo yanayofanana sana na tabia ya Rais Kikwete katika masuala tete kama haya. Tetesi zinadai Rais amekataa kwa sababu baadhi ya wabunge na watendaji katika kamati ya uongozi wa bunge wameingiza ajenda binafsi na fitina katika shutuma zao dhidi ya mawaziri wanaotakiwa kujiuzulu.

Inasemekana rais ameambiwa na watu wengine nje ya Waziri Mkuu Pinda, kuwa idadi ya mawaziri waliolalamikiwa na kamati za wabunge na kutakiwa kujiuzulu ni ndogo kuliko ile inayotajwa na baadhi ya wanakamati wa kamati ya uongozi wa bunge.

Aidha imedaiwa kuwa Rais Kikwete anaamini hili ni wimbi la upepo mbaya ambao Waziri Mkuu na serikali wakivuta subira litapita kama mengine yalivyopita.

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais imekanusha tetesi hizi lakini imekuwa kawaida ya Kurugenzi hii kukanusha taarifa za kweli na kuthibitisha mambo ya uongo au ya ujanja ujanja.

Imekuwa kawaida ya Waziri Mkuu Pinda kukumbana na dhoruba za kisiasa zinazotishia kuvunjiwa heshima kila mara Rais wake anaposafiri na kuacha fukuto la kisiasa. Itakumbukwa wakati wa sakata la Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, Rais Kikwete alikuwa Afrika ya Kusini.

Jairo alituhumiwa kwa ushahidi kuwa alikuwa amekusanya fedha toka mashirika na makampuni ya wizara yake kwa kisingizio cha “kuwezesha” bajeti ya wizara hiyo kupitishwa na bunge. Utaratibu huo ulijaa mazingira ya rushwa mbaya.

Huku nyuma Waziri mkuu alilazimika kutoa matamshi bungeni kuhusu hatima ya Jairo. Matamshi yake yalibainisha kuwa kama Jairo angekuwa katika mamlaka yake basi angeamuru mara moja kuwa Jairo hana kazi tena.

Matamshi yale mpaka leo yanamuuma na kumnyima ujasiri wa kusimamia serikali bungeni kwa sababu si tu Rais alibatilisha maneno yake, bali pia hata matokeo ya  kamati teule ya bunge iliyoteuliwa kuhusu kashfa hiyo hayajashughulikiwa.

Mara ya pili Rais Kikwete akasafiri kwenda Davos Uswizi huku nyuma mgogoro mkubwa wa mgomo wa madaktari ukiwa unarindima.

Waziri Mkuu alijitahidi kwa kadri ya uwezo wake kushuhgulikia mgomo huo na hata alipofanikiwa kukaa nao alijikuta akilazimika kuwaahidi kuwa Waziri wa Afya na Naibu wake wangejiuzulu au kuondolewa katika nafasi zao.

Alilisema hili baada ya kutangaza kusimamishwa kazi kwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo pamoja na Mganga mkuu wa wizara hiyo. Baada ya Rais kurejea nchini, siyo tu kuwa alipuuza ahadi ya Pinda kwa madaktari bali alikataa hata kupokea barua ya kujiuzulu iliyoandikwa na Waziri wa Afya.

Tofauti za kimtizamo kati ya Waziri mkuu na Rais katika masuala ya utendaji wa serikali yanaashirikia kitu kimoja tu kuwa Waziri mkuu ni tarishi tu na wala si kiongozi wa shughuli za serikali bungeni kama inavyotakiwa kwa mujibu wa katiba.

Ingekuwa ni tofauti za mitizamo baina ya wanandoa tungeelewa, lakini katika masuala ya kiserikali ambayo yamejengwa katika uwajibikaji wa pamoja, Waziri mkuu Pinda amedhalilika kiasi cha kuridhisha.

Safari hii Rais alikwenda Brazil. Huku nyuma bunge likachachamaa dhidi ya ufisadi katika baadhi ya wizara. Hii ilitokana na mjadala wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) iliyohusu mahesabu ya serikali za mitaa, serikali kuu na mashirika ya umma.

Mawaziri wahusika waliitwa mafisadi, wezi wakubwa na kwamba walistahili kunyongwa hadharani kwa sababu wanawatesa wananchi wasio na hatia. Wizara zilizoongoza katika shutuma hizo ni Wizara ya Fedha, Nishati na Madini, Uchukuzi, Afya, Tamisemi, Maliasili na Utalii, Kilimo na Viwanda na Biashara.

Hatimaye Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe (CHADEMA) akaja na jipya lililomkosesha raha Waziri mkuu Pinda.

Akaanzisha ukusanyaji saini za wabunge ili kuweka pendekezo la kupiga kura ya kukosa imani na Waziri Mkuu Pinda. Zitto akasema hatua hiyo inaweza kusitishwa tu, endapo mawaziri wahusika watajitolea wenyewe kujiuzulu ili kumwokoa waziri mkuu.

Kusita kwa mawaziri hao kujiuzulu kungelazimu Waziri Mkuu mwenyewe kujiuzulu au kulazimishwa na kura ya imani. Kuguswa kwa Waziri Mkuu kwa namna yoyote katika hizo kungekuwa na maana moja tu, yaani serikali nzima itakuwa imevunjika.

Waziri mkuu alijikuta njia panda. Bungeni kunawaka moto kwa mijadala na tishio la kukosa imani naye, Ikulu kulikuwa na Kaimu Rais (Dk. Gharib Bilali) anayedaiwa kusema hawezi kujihusisha na uamuzi wa mawaziri kujizulu.

Upande mwingine yuko Rais aliyekuwa safarini Brazil na kutoa hotuba ugenini kupongeza utaratibu wa wabunge kuibana serikali na kuisimamia. Pinda alijikuta anaungana na wabunge kuwataka mawaziri wajiuzulu ili kuokoa chama na serikali nzima.

Akachukua muda wa kutosha kuongea na mawaziri hao mmoja mmoja isipokuwa yule wa fedha ambaye hakuwa nchini. Wengi wao wakamkubalia na wachache sana wakamgomea. Kitendo cha mawaziri kumgomea Waziri mkuu, kiongozi wao na mkuu wa shughuli za serikali bungeni, kingetosha kumfanya awaweke pembeni ili rais akirudi toka safari awarejeshe kazini au athibitishe hatua ya Pinda kama anamheshimu. Haikutokea hivyo. Jibu la hatua hii analo Pinda.

Baada ya Rais kurudi nchini alikwenda kuhani misiba kadhaa ya hapa nchini kisha kuondoka kwenda kwenye mazishi ya Rais wa Malawi huku nyuma akiacha sintofahamu katika baraza lake la mawaziri.

Hata kama tamko la Waziri mkuu litatoka likikubaliana na matakwa ya bunge kuwa wajiuzulu, ni sahihi kusema Pinda amedhalilishwa vya kutosha chini ya mtindo wa utawala unaotumiwa na Rais Kikwete.

Pinda amelazimika kujibu hoja nzito ili kuokoa uso wa serikali lakini kila wakati, kama nilivyoeleza hapo juu, amejikuta akitelekezwa na Rais wake. Inatosha mtu kujiuliza, Waziri mkuu Pinda anataka adhalilishwe mara ngapi ili atambue kuwa hatakiwi na Rais wake hata kama alimteua?

Katika hali ya kawaida, tungetemea Waziri mkuu  ajiuzulu bila kushauriwa wala kulazimishwa na yeyote kwa sababu kuu mbili.

Kwanza, serikali aliyopewa kuisimamia haimtii wala kumheshimu. Amejikuta katika hali ya kuwabembeleza na kulialia ili kuwafanya wakubaliane naye.

Pili, Rais aliyemteua hamheshimu wala kumhurumia. Baadhi ya mawaziri wanajiunga na vijiwe vinavyodai Pinda hafai, ni “Padri” na hawezi kuumiza hata sisimizi.

Ikiwa Pinda ana huruma na serikali, chama na Rais aliyemteua angetangaza kujiuzulu ili heshima yake ndogo iliyobaki iweze kuhifadhiwa.

Kinyume na ushauri huu, ni yeye kusubiri Rais wake achukue hatua itakayomweka pembeni na hiyo itakuwa  aibu zaidi kuliko kama angejiondoa mwenyewe.

Tutikondo@yahoo.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: