Nani kairoga serikali ya Kikwete?


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 26 May 2010

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli

SERIKALI ya Awamu ya Nne, inaumwa ugonjwa wa “kupenda sifa.” Hata pale inapokuwa kwenye matatizo, bado viongozi wake hawataki kukiri. Wanaendelea kung’ang’ana kuwa “mambo ni mazuri.”

Mifano miwili mikubwa inathibitisha hilo. Wiki iliyopita Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, aliweka bayana kuwa mapato ya serikali yameshuka kwa wastani wa asilimia sita.

Alisema Mamlaka ya Mapato (TRA) haikusanyi kama awali; uuzaji wa bidhaa nje umepungua; katika bajeti ijayo serikali inakusudia kukopa Sh. 346 bilioni kutoka mabenki binafsi ili kufidia kile ambacho kinakosekana.

Kiasi ambacho kinakopwa na serikali ni sawa au zaidi kidogo ya makusanyo ya TRA kwa mwezi.

Hata hivyo, Mkullo alijitetea kuwa uchumi wa nchi umeimarika kiasi cha kuwa na nguvu ya kukopa fedha hizo na kwamba hata washirika wa mawandeleo - Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha Duniani (IMF) hawana kikwazo kwa maamuzi hayo.

Wakati Mkullo akipiga siasa zake, wiki hiyo hiyo sarafu ya Tanzania imeporomoka kwa kasi ambayo haijawahi kufikiwa. Katika kipindi cha wiki moja tu, sarafu hiyo imepoteza thamani yake kwa wastani wa Sh. 60.

Huku ni kuporomoka kwa kasi ya kutisha. Bado Mkulo hakuweza kuona athari za wazi za mserereko huo wa sarafu.

Kwa maelezo mafupi, kuporomoka kwa thamani ya sarafu ina maana kwamba mfumuko wa bei nao utapanda; bei mafuta – petroli, dizeli na yale ya taa – itakwea kila kukicha.

Matokeo yake, sekta nzima ya uzalishaji, kuanzia kwa mkulima, mfanyakazi kiwandani hadi kwa mfanyabiashara, itaathirika kwa kiwango kikubwa.

Katika mazingira ya namna hiyo, inakuwa ni vigumu sana kusikia na kusadiki maelezo kwamba eti “tupo salama kiuchumi.”

Lakini la pili ni maamuzi ya serikali ya kutuma mawaziri wake mikoani kueleza kinachoitwa, “mafanikio ya serikali tangu ilipoingia madarakani miaka mitano iliyopita.”

Hii ni mara ya pili kwa serikali kutuma mawaziri wake mikoani kueleza mafanikio yake. Ilifanya hivyo mara baada ya bajeti ya 2007/08. Wakati huo, serikali ilisema kwamba fedha nyingi zilitengwa kwenda kwa wananchi, hivyo ilikuwa ni muhimu kufanya hivyo.

Hakuna mafanikio yaliopatika katika safari hizo. Wengi wa mawaziri waliishia kuzomewa. Ni kwa sababu serikali ilikwenda kuhubiria watu wenye njaa, kiu ya maji wao na mifugo yao.

Sasa serikali inatumia mbinu zile zile zilizoshindwa za kuwaghiribu wananchi, kwamba serikali inawajali.

Je, nani asiyejua kuwa serikali hii imeshindwa kutekeleza majukumu yake kwa kiwango kikubwa?

Wakati serikali hii ikiingia madarakani, nchi ilikuwa imefikia hatua ya kugharimia baadhi ya miradi yake ya maendeleo kama vile ujenzi wa barabara kwa fedha zake za ndani.

Ilikuwa imejenga uwajibikaji wa kutosha kwa TRA; ilikuwa imeshusha mfumuko wa bei chini tarakimu mbili – kwa hakika chini ya asilimia sita; sarafu ya taifa ilikuwa imeimarika ikilinganishwa na dola ya Marekani.

Si hivyo tu, serikali ilikuwa imepunguza kwa kiwango kikubwa kukopa kutoka mabenki kwa kuwa huo ni mzigo usiobebeka kwa wananchi wake.

Lakini sasa tukiwa tunakimbilia mwaka wa tano wa utawala wa Rais Jakaya Kikwete, ni vigumu kutazama nyuma na kutaja kwa yakini ni yapi mafanikio ya serikali hasa kwa maana ya kujenga uchumi imara; kujitegemea zaidi na kuendeleza maelewano na washirika wetu wa maendeleo.

Miaka mitano inakatika huku, lakini hatuna la kujivunia katika kusimamia mipango ya kuwakomboa wananchi kutoka lindi la umasikini na kuvutia uwekezaji mkubwa.

Iko wapi mipango ya kujenga ajira, kuwawezesha wakulima kuachana na kilimo cha kudra na kwenda katika kilimo cha kisasa na mbiundombinu ya kuaminika?

Kwa hiyo safari hizi za mawaziri kwenda mikoani ambazo tayari imekwisha kumtokea puani Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Mary Nagu, huko Mbeya baada ya kukumbana na maswali magumu ya wananchi, si kitu kingine isipokuwa ni kuibuka upya kwa ule ugonjwa wa serikali – “ kusaka sifa. Sifa.”

Ni vigumu kutambua ujasiri wa kwenda kuongopea wananchi mwaka baada ya mwaka unatoka wapi kwa viongozi wa serikali?

Inakuwa vigumu zaidi kujua kama wanawaona wananchi wa nchi hii kama ni mazuzu tu ambao kumbukumbu zao ni fupi na hivyo hawaoni, hawakumbuki na wala hawana maumivu ya hali ya ugumu wa maisha ambayo kila siku iendayo kwa Mungu inakuwa afadhali ya jana!

Huu ni mwaka wa uchaguzi. Ni mwaka wa wananchi kuwapima waliopewa madaraka, wamefanya nini kuwaondoa pale walipokuwa?

Ni kwa kiwango gani wamewezesha kujitegemea na kujielekeza kwenye njia bora za maendeleo. Hao walioaminiwa kwa miaka yote hiyo, wameonyesha uaminifu wao kwa kutumia vema rasilimali za taifa?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: