Nani kateua mhuni kampeni za CCM?


Anthony Mayunga's picture

Na Anthony Mayunga - Imechapwa 22 September 2010

Printer-friendly version

MTENDAJI mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yussuf Makamba ametetea chama chake, kwamba hakihusiki na tukio la kufukuzwa kwa waandishi wa habari, wiki tatu zilipita mjini Bukoba.

Alisema, “CCM ni chama makini. Hakiwezi kufukuza waandishi wa habari.”

Makamba alikuwa akijibu tuhuma kwamba chama chake kilishiriki katika kufukuza waandishi wawili wa habari wa magazeti ya Mwananchi na The Citizen.

Katika kutetea chama chake, Makamba alisema, “Ili uamuzi wa chama uwe wa chama, ni lazima ufikiwe na Kamati Kuu (CC), Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), au aufanye katibu mkuu. Vikao hivi havikufanyika kokote na mimi katibu mkuu sijaagiza mtu awafukuze waandishi.”

Aliongeza, “Fuatilia vizuri habari yako, ni lazima utagundua kuwa yupo mhuni amekosana nao akawafukuza.”

Makamba hataki kumtaja huyo anayemwita mhuni ambaye ameongozana na mgombea wa chama chake. Wala hataki kujadili hatua ambazo chama makini kitamchukulia mhuni anayetajwa kufukuza waandishi wa habari.

Aidha, Makamba hataki kueleza ulimwengu, kwa nini chama chake kimeteua mhuni na kumwingiza katika msafara wa mgombea urais.

Hataki kujadili kwa nini yeye na chama chake wameshindwa kumwondoa mhuni huyo. Hataki kueleza kwa nini chama kinachoelekea ikulu kimebeba wahuni.

Ni kwa sababu, alichokisema sicho anachokiamini. Makamba anajua kuwa uhuni si sifa nzuri. Anayeitwa mhuni hafai kukaa na watu makini; hawezi kuruhusiwa kufanya kazi zao wala hawezi kuwasemea.

Kama afisa wa habari wa mgombea wa urais ni mhuni, habari zinazotoka zitawezaje kuaminiwa? Je, nani anaweza kuziamini? Kwa vigezo vipi?

Ni muhimu hili likafahamika. Kama mhuni yupo katika msafara wa mgombea urais, tena ambaye yuko madarakani, wahuni wengine wangapi wamejazana ikulu? Akibahatika kushinda uchaguzi, ataunda serikali gani na iliyolenga kundi gani?

Je, mgombea ambaye amekusanya wahuni katika timu yake ya kampeni, atawezeje kuaminisha wananchi, kwamba serikali atakayoiunda haitajaa wahuni?

Kauli ya Makamba ni tata kwa ujumla wake na inatafsri nyingi kwa watu; maana haiwezekani chama makini kinachoongoza serikali kuchukua mhuni na kumlipa fedha ili kuratibu waandishi wa habari.

Mtu aliyemtaja Makamba kwamba ni mhuni bado anaendelea na kazi yake. Anaendelea kufukuza waandishi. Amekabidhiwa fuko la fedha ambazo zimechangwa na wanachama.

Bila shaka Makamba anajua maana ya mhuni; ni kapera, mseja, mpora wake za watu, asiye na makazi maalum, mwizi, kibaka, mvunjaji wa sheria, mnyang’anyi, mchopozi na ambaye anaishi kihuni.

Kutokana na hali hiyo, Makamba anataka kuwambia wanachama wake, kwamba amekosa watu makini wa kufanya kazi ya kuratibu vyombo vya habari. Ndiyo sababu amelazimika kuchukua mhuni kufanya kazi hiyo.

Vinginevyo, Makamba anataka kutuambia kuwa CCM yote imejaa “manyani” – wanaoweza kuruka pamoja.

Lakini hili nalo linahitaji mjadala. Inakuwaje ndani ya chama makini chenye viongozi makini, utawala makini, unaojali na kutekeleza majukumu yake bila ubabaishaji, kusiwepo mtu mwadilifu wa kufanya kazi makini?

Je, nani aliyeruhusu demokrasia kubinafsishwa kwa kundi la wahuni ambao moja ya kazi yao kubwa ni kuzuia wananchi kufahamu mgombea yupi kasema nini na yupi ameahidi kipi?

Maana hata kwa kuwatimua hao bado kunazidisha maswali kutoka kwa wananchi wanaokabiliwa na hali ngumu ya maisha chini ya serikali ya chama makini, lakini chenye kuzungukwa na wahuni.

Je, nani ataamini kuwa si Makamba aliyeagiza huyo anayeita “mhuni” kufukuza waandishi? Kama si hivyo, amechukua hatua gani kumdhibiti?

Mwandishi wa makala hii, Anthony Mayunga, amejitambulisha kuwa msomaji wa MwanaHALISI. Anapatikana kwa imeili:antonymayunga@gmail.com Simu: 0787-239480 na 0713290944
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: