Nani mlinzi wa albino?


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 21 January 2009

Printer-friendly version
Uchambuzi

JAPHET Kaliita ameuawa. Ni albino. Wamezaliwa albino watatu katika familia. Mmoja ndiye ameuawa. Wamebaki wawili – mmoja mwanamke.

Bado albino wanasakwa. Kwa gharama yoyote ile. Wanakatwa viungo vya mwili. Wanauawa kikatili. Hivyo ndivyo alivyouawa Japhet Kaliita.

Ilikuwa Jumamosi iliyopita. Kundi la watu wasiojulikana idadi lilikwenda kwake; kijiji cha Itongo; kitongoji cha Kisana katika wilaya ya Muleba. Kikajeruhi na kuua.

Wauaji walikuwa na jiwe kubwa. Wanaliita “fatuma.” Walilitumia kuvunja mlango wa nyumba walimolala Japhet na mkewe. Wakaingia. Wakamkamata mke wake Japhet. Wakampiga. Wakamburuta nje. Wakampiga kwa kitu kizito kichwani. Akazimia. Ndipo wakageukia mume wake.

Hakuna kilichosalia. Walikata mikono miwili ya Japhet. Wakakata mguu mmoja. Katika kiwewe sikuuliza ni wa kulia au kushoto. Wakakata korodani zake na kiongozi wake. Wakamwacha afe. Akafa. Amezikwa.

Japhet ni mtoto wa Laurian Kaliita na mjukuu wa Mzee Matobo. Mama yake anaitwa Ntumbya. Ni wakazi wa Kisana, Itongo.

Marehemu ameacha mjane aliyejeruhiwa vibaya na watoto wawili ambao siyo albino. Ndugu yake ambaye pia ni albino anaitwa James Kaliita. Hajaoa. Hana mtoto.

Dada yake marehemu, Nyamichwa Kaliita ambaye pia ni albino, aliishaolewa kijiji cha mbali kidogo cha Igabilo. Lakini hakai huko. Amerudi nyumbani kwao alikozaliwa. Anaishi na wazazi wake. Hakurudi na watoto wake.

Hakuna ambaye amemuuliza Nyamichwa kwa nini amerudi kwa wazazi wake. Au kuna majirani wanaojua siri ya binti huyo kurudi na kuishi na wazazi zaidi ya miezi minane sasa? Au aliishadokeza baadhi ya ndugu na marafiki au hata wazazi wake juu ya uamuzi huo? Je, ulikuwa uamuzi au ilikuwa shuruti?

Sikilizeni kilio cha albino Nyamichwa aliyerejea kwa wazazi wake kijijini Itongo. Aliyepoteza kaka. Anayetunza na kuliwaza wifi yake – mke wa marehemu kaka yake.

Nyamichwa analo la kusema. Kwamba ametishiwa. Kwamba ameelezwa kuwa hawezi kuendelea kuishi wakati yeye ni “mali” inayoweza kutajirisha wengine na kufanya wasife masikini.

Kwamba Nyamichwa atauzwa. Au atauawa. Au atabadilishwa na bidhaa. Lakini hawezi kuendelea kuishi na wale anaoishi nao wakaendelea kuwa masikini. Ni maapizo katili. Ya kijinga lakini jinai tupu.

Nyamichwa hali chakula kikazama. Hanywi maji yakateremka. Halali akapata usingizi. Haketi na kutulia. Hatumwi jirani bila msindikizaji. Woga umetanda. Harufu ya mauti imemzonga na anaona kama haoni.

Ni ukweli unaosikika kama hadithi; lakini ndiyo hali halisi inayomkumba Nyamichwa, kaka yake James Kaliita na albino wengine kijijini Itongo, wilayani Muleba na nchi nzima.

Sasa nyumba ya mzee Laurian Kaliita inanyemelewa na mauti. Yuko wapi wa kuhojiana na Nyamichwa na kudadisi wahusika ili kupata msingi wa kumlinda binti huyu na kaka yake?

Polisi wa mji mdogo wa Nshamba? Wale wa makao makuu ya wilaya, Muleba? Au polisi mkuu wa mkoa? Au iteremke amri kutoka kwa Said Mwema? Wako wapi wa kulinda Nyamichwa na kaka yake na albino wengine?

Yuko wapi wa kutambua nyayo za walioua; kuwafuatilia walikotokomea na viungo vya Japhet ili kujua walikotokea; waliowatuma na wanaowalinda?

Uko wapi uongozi wa kijiji – wanaita serikali ya kijiji – ukatao mashauri ya mashamba, ugomvi wa mipaka na matusi ya nguoni; lakini kimya pale washenzi wanapochukua roho za wanetu?

Ziko wapi nyumba kumi – au ishirini au hata arobaini – za vyama vya siasa za kuvunia wapigakura wakati wa chaguzi lakini zenye makengeza wakati wa kulinda uhai wa “malaika?”

Ingia kila kijiji. Sikiliza taarifa. Kila kijiji kina “kamati ya ulinzi.” Ziko wapi kamati za ulinzi za vijiji za kulinda uhai wa albino – vitoto vyetu vipendwa vyenye ulemavu wa ngozi? Ngozi tu!

Uko wapi uratibu wa ulinzi unaofanywa na kamati za ulinzi za wilaya? Zipo? Zinafanya nini na lini? Zinasubiri wizi wa mifugo na mitafaruku ya wanafamilia? Hazijasikia kilio cha albino?

Nyamichwa anahema bila kukimbia. Anatoka jasho bila kufanya kazi. Kumbe roho yake iko kazini. Kumbe akili yake imo mapambanoni. Kumbe amejaa fikra za kujikinga na maadui na utaona misuli yake ikituna, mishipa myembamba ya damu ikiranda ngozi yake nyeroro mikononi na shingoni.

Yako wapi mashindano ya vyama vya siasa katika kuhubiri mabadiliko yanayohitajika; kwamba ni pamoja na kuacha mauaji ya albino? Kwamba adui wa nchi siyo albino.

Iko wapi serikali inayoona kuwa mauaji ya albino ni janga kubwa la kitaifa na lenye gharama kubwa kwa utawala na watawaliwa? Serikali inayokataa kulea ushenzi katikati ya ustaarabu?

Iko wapi serikali inayokubali, na mara moja, kuweka utaratibu wa nchi nzima wa kujua albino yuko wapi – amezaliwa wapi, anaishi wapi, anapata wapi elimu na anafanya nini?

Uko wapi utaratibu unaoendana na uratibu wa shughuli za ulinzi wa albino – kutoka ngazi ya familia, kitongoji, kijiji, kata, wilaya hadi taifa?

Kifo kije kwa albino kama kinavyokuja kwa mtu yeyote; vinginevyo uhai wa albino, kama ulivyo uhai wa raia mwingine, ulindwe kama mboni ya jicho.

Liko wapi jeshi la asasi za kijamii la kuranda na kutanda hadi vijijini; likielimisha wananchi na kushawishi kila mmoja kuwa mlinzi wake mwenyewe na mlinzi wa albino?

Nani awafikie waganga wanaotaka viungo vya mwili wa albino ili wawape watu utajiri; wakati waganga wenyewe hawajawahi kutajirika, kuelimika wala kustaarabika?

Tukubali. Bila kuweka mfumo wa ulinzi wa maisha ya wananchi, wakiwemo albino, raia hawawezi kufurahia uhuru walionao katika nchi yao.

Na utawala ukishindwa - kwa ngazi yoyote ile – kitongoji, kijiji, kata, wilaya na taifa – kuhakikisha kunakuwa na mipango na uratibu wa ulinzi wa maisha ya kila mmoja, utakuwa umepoteza hadhi; utakuwa unaandika maombi ya kufukuzwa kazi.

0
No votes yet