Nani zaidi, wabunge au NEC?


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 08 September 2009

Printer-friendly version
Tafakuri
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC) Jaji Lewis Makame

UJASIRI unaozidi kuonyeshwa na kundi la wabunge wanaoitwa ‘kimbelembele’ wa vita dhidi ya ufisadi ni jambo linalostahili pongezi.

Kundi la wabunge hawa wakiongozwa na Spika wa Bunge la Jamhuri, Samwel Sitta, si tu limekuwa jasiri wa kuendeleza mapambano hayo, ila wamethubutu kufanya hivyo licha ya mbinu zilizoshindwa za Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kujaribu kuwatisha.

Sitta na wale walioitwa wabunge 11 walisulubiwa ndani ya NEC kwa madai kwamba “Wameuza mapambano dhidi ya ufisadi kama vita yao binafsi.”

Lakini mwishoni mwa wiki, kundi hilo la liliwasha moto katika jimbo la Nzega linalokashikiliwa na mpambanaji mwenzao, Lucas Selelii. Ilikuwa ni katika kile kilichoitwa, “kuunga mkono Selelii asimezwe na mafisadi.”

Wabunge waliohudhuria ni pamoja na Dk. Harrison Mwakyembe (Kyela), Beatrice Shellukindo (Kilindi), Christopher ole Sendeka (Simanjiro), James Lembeli (Kahama) na Fred Mpendazoe (Kishapu). Mwingine aliyehudhuria ni Nape Nnauye, kada mwingine wa CCM anayejitambulisha kuwamo katika timu hiyo.

Ujumbe wa wabunge hawa umekuwa wazi, kwamba wataendelea kupambana na ufisadi kwa sababu ni kikwazo cha maendeleo ya wananchi.

Walisema wazi kwamba hawapigi vita ufisadi kwa sababu ya kutafuta umaarufu kama ambavyo wanazushiwa, ila ni kutaka rasilimali za taifa zitumike kwa ajli ya kuleta maendeleo ya wananchi kwa ujumla wao.

Kama ilivyo kwa wabunge hao, Sitta alikuwa mkoani Singida ambako naye aliwasha moto kama uliowashwa na wabunge hao, ingawa malengo ya ziara yalitofautiana.

Nimeamua kuwapongeza wabunge hawa kwa sababu naamini wamejitoa muhanga kiukweli. Nasema haya kwa sababu nyingi, lakini iliyowazi ni tabia ya CCM kusulubu wabunge wao.

Kwa wale wanaokumbuka vizuri, wanajua kilichompta aliyekuwa mbunge wa Njombe Magharibi, Thomas Nyimbo, ambaye alikuwa mwiba kwa chama na serikali.

Nyimbo mwanasiasa aliyewahi kujiunga na chama cha upinzani cha PONA, Julai mwaka 2007 lipigwa marufuku kugombea nafasi yoyote ya uongozi ndani ya chama hicho.

Uamuzi wa kumsimamisha Nyimbo kugombea uongozi ulifikiwa na kikao cha Kamati Kuu (CC), hatua zilizokwenda sambamba na kuvuliwa uanachama aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, mkoani Ruvuma, Burhan Makonje, pamoja na madiwani wengine wanne kwa madai ya utovu wa nidhamu.

Nimekumbuka matukio haya ya kushughulikiana ndani ya CCM baada ya kuanza kuona dalili kwamba juhudi za NEC kama ilivyoonekana hivi karibuni kuwafunga mdomo wabunge wake na kumtisha Spika Sitta, zimegonga mwamba.

Mwamba huu umeonekana kuwa mgumu na unaweza si tu kuleta madhara makubwa kwa chama, ila pia umeonyesha wazi ufa ulioko ndani ya chama hicho juu ya makundi yanayosimamia ukweli dhidi ya yale ambayo yameamua kukumbatia ufisadi.

Hatua yao ni wazi itakuwa ni pigo kwa Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba na katibu wa uenezi, John Chiligati waliotoa kauli tofauti juu ya Sitta.

Wakati Makamba amejiapiza kumdhibiti Sitta, Chiligati amenukuliwa akisema Sitta amekuwa refa anayeumiza serikali bungeni.

Sitta na baadhi ya wabunge hao waliokuwa Nzega mwishoni mwa wiki, ni kundi linalofananishwa na akina Nyimbo wa mwaka 2007. Hata hivyo, tofauti na mwaka 2007, mwaka huu kundi hili lina wabunge wengi. Kwa ujumla wao wanakadiriwa kuwa zaidi 70.

Kundi hili bila huruma limeamua kuweka kando itifaki za kinafiki za chama na kutaka kila mwenye tuhuma ya ufisadi awajibike kwa uchafu wake. Wanataka chama kisiwe kichaka cha kusafisha watu wenye tuhuma nzito za ufisadi, wanataka chama chao kiishi kama maandiko yake yanavyosema- kimbilio la wanyonge, si kunyonga wanyonge.

Kwamba kama kweli hakuna nafasi ya ufisadi ndani ya chama hicho na iwe hivyo; kwamba kama rushwa ni adui wa haki na ionekane hivyo; kwamba cheo ni dhamana na hakuna atakayekitumia kwa maslahi binafsi na iwe hivyo; kwamba CCM ni kimbilio la wanyonge wote na iwe hivyo.

Wabunge hawa wameamua kuendeleza mapambano licha ya juhudi zilizosukwa na makuwadi wa mafisadi kutaka kila mbunge kuwa bubu. Hawa wameamua kujitenga na kusimama wahesabiwe.

Wabunge wote hawa ni wa CCM, wanakifahamu chama chao, wanajua michezo michafu ya ndani na nje, lakini wamekataa kuwa wasanii kama NEC ilivyoagiza.

Lakini kama maandiko yanavyosema, wabunge wamechagua fungu lililo jema, wameamua kuwa upande wa wananchi- wadai haki.

Wanajua fika kwamba nia ovu za kifisadi za kutaka wabunge wafunge midomo ili wezi waendelee; wahujumu wapete; wenye mawaa ya kila aina wasafishwe, ni kazi ngumu kwao. Ni sawa na kuweka rehani dhamiri zao na kuhalalisha hujuma dhidi ya taifa lao.

Tukikwa tunasubiri jaribio la pili la mafisadi la kuwanyamazisha wapiganaji hawa, tayari salamu zimepokelewa na wahusika kutoka Nzega na Singida, kwamba hawako tayari kuwa sehemu ya uchafu na watapambana.

Hakika picha hii ndiyo kwanza inaaza, makubwa zaidi yaja na tunayasubiri kwa shauku. Wananchi wanasubiri matokeo. Nguvu ipi itasimama? Ile ya ufisadi au ya umma?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: