Naomba uanachama wa CCM


Nyaronyo Kicheere's picture

Na Nyaronyo Kicheere - Imechapwa 18 July 2012

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

Kwa Wilson Mukama,
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi
Makao Makuu Rasmi ya Chama,
Mtaa wa Lumumba, Dar es Salaam.

Ndugu Katibu Mkuu, Salaam sana, ama baada ya salaam, nakuarifu kwamba mimi, mke wangu Martina na wanangu hatujambo, hofu na mashaka ni juu yako wewe na viongozi wenzako makao makuu rasmi ya chama, hapo mtaa wa Lumumba Dar es Salaam.

Ndugu Katibu Mkuu, nimeamua kuleta barua hii moja kwa moja ofisi ndogo ya makao makuu ya CCM, kwa sababu nafahamu na hata wewe unafahamu kwamba ndiyo makao makuu rasmi ya CCM, na kwamba ile kutaja kwenye katiba ya CCM kwamba makao makuu ni Dodoma ni geresha tu.

Kama unavyofahamu chama chetu bila posho hakiendi. Lazima kwanza zitafutwe mbinu za kulipana posho ili watu wawe na uhakika wa maisha na watoto wao waweze kubadilisha mboga. Hata serikalini posho ni mtindo unaoeleweka.

Ndugu Katibu Mkuu, usishangae ninaposema posho serikalini ni mtindo mmoja kwa sababu watu wote wanajua na hata wewe unajua kwamba tunatamba kuwa Dodoma ndio makao makuu ya nchi ili wafanyakazi, mashushu na viongozi wa nchi hii waweze kupata posho Dar es Salaam au Dodoma.

Watumishi wanachagua, kama makazi yao rasmi yawe Dar es Salaam au Idodomya (Dodoma). Bila makao makuu kuwa Dodoma mambo yote yakafanyika Dar es Salaam watu hawatatuelewa, kwani posho zitapatikanaje, na sisi chama chetu sera yetu kuu ni posho?

Si unaona yule mbunge wetu mpenda posho aliyehamia CHADEMA anavyohangaishana na wenzake huko? Jina simtaji lakini anajulikana na hata wewe unamfahamu. Mwenzetu yule akahamia chama cha njaa kali, “no posho;” naye ananga’ang’ania sera za CCM za posho ugenini, taabu kwelikweli.

Najua unashangaa sana mie kusema CCM chama changu au chama chetu. Huna haja ya kushangaa na uwe na amani tu. Kwa taarifa yako na wenzako wote hapo makao makuu ya CCM, chama tawala, mie nimeamua kuritadi. Kuritadi ni kukana dini yako rasmi.

Ndugu Katibu Mkuu, nimeamua kuritadi na kuhama kambi kutoka ushabiki wa upinzani na kuanza rasmi kushabikia Chama cha Mapinduzi, na yote haya kwa siri moja na sababu kadhaa. Nitazitaja.

Kwanza kabla hatujaenda mbali, nikumbumbushe kwamba wewe na mimi tunatoka kanda moja, mkoa mmoja, na hata kabila moja. Kwani wewe kabila gani? Ukiwa Mwikizu, Mngoreme, Mtimbaru, Mnyabasi, Mkwaya, Mnata, Mwikoma, Msweta, Mnyamongo na hata Mjita, Mkabwa au Mruri, kwa vile wote tunatoka Mara basi wote ni Wakurya tu tusiangushane.

Usitoe siri yangu kwa wanoko kama akina Nape Nnauye. Unapaswa kutukumbuka sisi tunaotoka kanda moja na mkoa mmoja, si unaona wengine wanavyopendeleana kikanda siku hizi. Unaona siku hizi barabara ya Mugumu – Loliondo inazungumzwa? Sababu ni kwamba wahusika wengi hawatoki huko.

Sasa siri yenyewe ni hii. Nimegundua kwamba mtu ukiwa CCM unapata manufaa mengi ambayo watu wa vyama vya upinzani hawayapati. Sasa wewe ndugu yangu utapenda niendelee kukosa manufaa yoyote nchini? Mura weito naomba kadi ya CCM kabla ya mambo mengine yote.

Mtu unapokuwa CCM hata ukipatwa na zahama au makosa ya dhahiri unashughulikiwa na vyombo vya dola kwa nidhamu na utaratibu unaotakiwa kisheria na kikatiba unafuatwa. Na si lazima upate adhabu yoyote kwa mujibu wa sheria. Si umeona yaliyowapata watuhumiwa na washutumiwa wa kashafa ya rada.

Ndugu Mukama, si unafahamu kwamba watuhumiwa wa rada hawajawahi kuguswa na serikali kwa kujua kwamba ni wana-CCM safi ? Jamhuri haikuwahi hata kujaribu kuwachunguza. Hata wale waliojitokeza hadharani na kudai kuwa mabilioni yaliyopo kwenye akaunti zao za Ughaibuni ni VIJISENTI TU hawakuguswa.

Hata wale watuhumiwa wa kashfa ya EPA nao hawakuwahi kufanywa chochote badala yake waliitwa, sielewi wapi; wambea wanadai waliitwa Sheraton, Kilimanjaro au Holiday Inn, kuzungumizia namna ya kurudisha pesa walizokwapua au kwa lugha nyepesi walizokwiba.

Wewe uliona wapi mwizi anakaribishwa mbele ya viongozi wa nchi na kuhojiwa kwa ulaini kabisa kama “utarejesha lini mali uliyopora?” Hayo ndiyo manufaa ya CCM ninayotafuta.

Halafu, mtu ukiwa mwanachama wa CCM tena msomi na mwandishi mzuri kama mimi, si ajabu siku moja nikasikia redioni jina langu linatangazwa kuwa nimeteuliwa ujumbe wa Tume ya Katiba au Tume ya madawa ya Kulevya au Tume ya madini au Tume ya mali asili kwenye posho kibao, kikao kimoja milioni moja safi.

Na mimi najiunga CCM nikijua kuwa Mlenchoka mwenzangu upo hapo makao makuu tena una cheo kikubwa, nitafaulu tu malengo yangu. Mbona waandishi wenzangu wanaojua kucheza vema tayari wamekuwa wakuu wa mikoa, wilaya na hata mawaziri na marais, sembuse mie! Au wewe huwajui?

Ndugu katibu Mkuu, ni bahati mbaya sana kuwa nilipotoshwa na akina Wilbroad Slaa, Philemon Ndesamburo, Freeman Mbowe na ha hata Mabere Marando tangu enzi za NCCR. Wenzangu walioshituka mapema mbona wamewini. Akina Akwilombe, Amaan Kaborou na hata Mbunge wa Temeke, Abbas Mtemvu.

Sasa wa poti, bora kuchelewa kuliko kutofika kabisa. Mie nimechelewa lakini ni afadhali kuliko nikibakia huku kukavu, hakuna kitu na wabunge wake hawataki posho na vilevile kuna hatari ya kubambwa kwenye maandamano. Sie tutakula maandamano? Naomba kadi ya CCM nitulie nisubiri cheo labda Mheshimwa atanikumbuka.

Pia mambo yaliyofanyika pale msitu wa Pande karibu mara mbili hivi katika utawala wa awamu ya nne yanatisha. Ndugu katibu Mkuu, nani atahimili kuendelea katika upinzani huku akijua siku atakapopatikana ataishia msitu wa Pande ambako nasikia meno yanang’olewa na kucha zinanyofolewa bila ganzi?

Ni afadhali niwe kama yule rafiki yangu Mhaya kutoka Bara ambaye “alidaiwa kuwa na matongotongo” lakini mwenye akili sana. Anaitwa Dk Lutta Nelson, sasa usiniuze kama ni daktari wa meno, vidonda au dakitari wa kusomea. Alipogombea kwa tiketi ya CHADEMA kwanza aliibiwa kura pili, akanyang’anywa tenda serikalini.

Alichokifanya Dk. Luta ni kukiri makosa akarejea CCM na akapiga marufuku siasa katika maeneo yake ya biashara na kuanza kulipia michango ya mwenge, afya, mshikamano na kadhalika. Kilichofuata Dk Lutta alirejeshewa tenda yake ya ‘kusaplai’ vifaa vya sayansi katika maabara za shule za sekondari na sasa katulia kimya anafaidi matunda ya CCM.

Kwa sababu hizo na nyingine ambazo sikuziandika hapa, tafadhali ndugu yangu nifanyie mipango ya kadi ya CCM na unifanyie mipango ya kunikutanisha na watu muhimu chamani wanaoweza kunitoa kama vile Mwenyekiti wa Taifa (safari za nje), wanachama mashuhuri kama Rostamu (mitaji ya biashara) na mawaziri nipate angalau wanangu kuajiriwa Benki Kuu au mashirika ya pensheni.

Wasalaamu,
Nduguyo Mwanamara mwenzako, Nyaronyo.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: