Naona Chenge akimfuata Mramba, Yona


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 15 September 2009

Printer-friendly version
Tafakuri
Andrew Chenge

DUNIA ina mambo. Kuna siku moja rafiki yangu wa karibu sana alinisimulia kisa cha kuchekesha na kushangaza. Hiki hakikuwa kingine isipokuwa kilihusu ugomvi wa mwanasiasa maarufu nchini, Andrew Chenge na mwandishi wa habari mwandamizi, jina ninahifadhi, kilichotokea katika klabu moja jijini Dar es Salaam miaka ya hivi karibuni.

Rafiki yangu alinieleza kwamba kisa cha ugomvi huo ni mwandishi kumuuliza kwa njia ya kumshangaa Chenge kwamba bado yu uraiani na hajafungwa jela au walau kuwa mahabusu ya polisi kutokana na mfululizo wa matendo yake ya ukiukaji wa sheria, maadili na matumizi mabaya ya ofisi ya umma akiwa mwanasheria mkuu wa serikali kwa miaka 10.

Chenge ambaye kwa mara ya kwanza aliteuliwa na rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, kuwa mwanasheria mkuu wa serikali mwaka 1995, akijipatia kinywaji chake kwenye klabu hiyo ya usiku, ambapo mwandishi huyo mzalendo aliamua kumpasha Chenge 'live' kwamba anashangaa bado yu uraiani akitanua wakati kwa mwenendo wa matendo yake alistahili kuwa jela!

Mpashaji wangu alisema kwamba Chenge alikasirika sana. Alikasirika kiasi cha kutaka kurusha ngumi kama si waungwana waliokuwako eneo hilo, leo hii tungekuwa tunasimulia mengine kabisa.

Nimekumbuka kisa cha Chenge cha kwenda jela hasa baada ya kusikia jinsi Rais Jakaya Kikwete alivyojibu maswali mbalimbali ya wananchi wiki iliyopita hasa lile lililohusu ufisadi na jinsi anavyoendesha vita hiyo, lakini wananchi wakihisi kwamba kuna mapapa ya ufisadi ambayo hayajafikishwa mahakamani kwa sababu ya kuwa karibu naye, yaani marafiki wake!

Kiwete alisema wazi, kwamba hana ndugu wala rafiki katika vita dhidi ya ufisadi, kila mmoja atabeba mzigo wake. Rais alieleza wazi kwamba hana mpango wa kumlinda yeyote, na kueleza wazi kwamba hata kesi za wizi wa fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), zinaendeshwa na mkurugenzi wa mashitaka (DPP). Hana cha kufanya kama Rais.

Wakati rais akijibu swali hili alisema kuna "kesi mbili au tatu" zinatarajiwa kufikishwa mahakamani na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru). Binafsi niseme tu si mtabiri, lakini kwa vyovyote itakavyokuwa ninanusa kesi hizi katika maeneo makuu matatu hivi.

Moja, sakata la rada ambalo limenguruma nchini tangu mwaka 2002 hapana shaka kwa uchunguzi uliofanywa na makachero wa makosa makubwa ya jinai wa Uingereza (SFO) ambao wamemuunganisha kwa karibu sana Chenge na rushwa katika ununuaji wa rada hiyo, itakuwa ni moja ya kesi hiyo.

Ya pili, inawezekana kuwa watumishi kadhaa wa umma watafunguliwa kesi kuhusu mkataba tata wa kufua umeme ambao Tanesco iliingia na kampuni ya Richmond Development Corporation (LLC).

Watumishi hawa ingawa hadi sasa wamethibitika kuishauri vibaya serikali hadi kujitumbukiza kwenye mkataba huo ulioitingisha serikali ya awamu ya nne hadi baraza la mawaziri likasambaratika baada ya kujiuzuku kwa Waziri Mkuu Edward Lowassa, wameonekana wazi kuwa wazembe kwa kiwango kikubwa. Hili limesemwa na limethibitishwa na serikali mara kadhaa na juzi rais Kikwete mwenyewe alisema kwamba watumishi hawa walikuwa wazembe, tena uzembe mkubwa.

Tatu, suala la kuanzishwa kwa kampuni ya Mwananchi Gold iliyoundwa na makada wa CCM, ikachotewa fedha BoT na aliyekuwa gavana wake, Daudi Ballali, wana hatari ya kufunguliwa mashitaka kwa sababu hadi sasa imeshindikana kueleweka ilikuwaje fedha kiasi cha Sh. bilioni tatu, zichotwe tu hivi hivi.

Pamoja na hisia kutanda kwamba kesi hizo alizotoboa Rais Kikwete zitafikishwa mahakamani muda si mrefu ujao, ubashiri mkubwa unaelekezwa kwa rada.

Sakata la rada kwa muda mrefu sasa limekuwa mwiba kwa serikali kwa maana mbili; kwanza imethibitika pasi na shaka kwamba katika Sh bilioni 40 hivi zilizotumika kununua rada hiyo, kiasi cha Sh. 12 bilioni zilikuwa ni rushwa ambayo iligawa kwa makundi mbalimbali ya watu, lakini muhimu zaidi Chenge akiwa mwanasheria mkuu wa serikali akitajwa na SFO kwamba alinufaika na rushwa hiyo.

Ingawa Chenge amekuwa akidai kwamba hana hatia katika suala zima la sakata la rada, na pia akikanusha kuwa akaunti yake ambayo iko ughaibuni kisiwani Jersey ikiwa na kitita cha Sh 1.2, bilioni kuwa ni mapato ya rushwa, bado imekuwa ni vigumu kuthibitisha pasi na shaka yoyote jinsi alivyopata mapato hayo anayodai ni yake na familia.

Chenge bila kutafuna maneno amekuwa ni mzigo kwa CCM baada ya kubainika kuwa mzigo pia ndani ya serikali ya awamu ya nne, ambako alilazimika kujiuzulu nafasi ya Waziri wa Miundombinu mwaka 2008, kutokana na suala la rada.

Mwanasiasa huyu ambaye anajua kwa undani kila mkataba ambao serikali iliingia na nchi, mashirika au makapuni mengine yoyote ya ndani na nje katika kipindi chote cha utawala wa serikali ya awamu ya tatu, alithibitika pia kusema uongo kwa kamishna wa maadili ambako viongozi wote huwasilisha fomu maalumu za kutangaza mali na madeni yao.

Katika fomu hizo, Chenge akiwa mwanasheria mkuu wa serikali tangu 1995-2005, hakusema lolote kuhusu fedha hizo alizojihifadhia ughaibuni. Hata akiwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki na baadaye Miundombinu, pia hakutaja fedha hizo.

Chenge ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, ni mwenyekiti wa kamati ya maadili ya chama hicho, lakini wakati huo akiwa amebeba zigo la tuhuma kuhusu uadilifu wake yeye mwenyewe na pengine maamuzi ambayo aliyafikia akiwa mwanasheria mkuu wa serikali au hata ushauri alioutoa akikalia kiti hicho.

Baada ya kusikia Rais Kikwete akitaja kesi 'mbili au tatu' nilimkumbuka Chenge, lakini nilipofikiria zaidi, nikamkumbuka yuke mwandishi wa habari mwandamizi aliyemweleza Chenge kuwa anashangaa bado yuko uraiani badala ya kuwa anakula dona mahabusu kutokana na mawaa yaliyogubika utumishi wake serikalini.

Wapo viongozi wengine waandamizi wa serikali wanaokabiliwa na kesi kortini, kuna Basil Mramba, mwanasiasa mkongwe na waziri aliyeshika nafasi mbalimbali ikiwamo Fedha; Viwanda na Biashara; Miundombinu; Kazi na Maendeleo ya Vijana bila kusahau nyadhifa nyingine katika mashirika ya umma kama SIDO na kwingineko.

Pia yumo Daniel Yona anayekabiliwa na kesi sawa na Mramba. Yona alishikikilia nyadhifa mbali za uwaziri kama Uchumi na Mipango, Fedha na Nishati na Madini.

Kama Chenge ataungana na wakongwe wengine, basi orodha ya mawaziri walifikishwa kortini kukabiliwa na mashitaka ya matumzi mabaya ya ofisi za umma itaongezeka na huenda ukawa ujumbe kwa wengine wengi.

Lakini kama haya yatatimia, yule mwanandishi mwandamizi atakuwa na hali gani kuona ndoto yake ikitimia? Tusubiri.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: