Nape amepewa rungu kulipa kisasi


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 27 April 2011

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli

NGUMI za mitaani hazina sheria, kanuni, uwanja wala klabu za kujifunzia. Pambano linaweza kusababishwa na watu wawili, mara nyingi kwenye muziki au klabu za pombe. Kisa kinaweza kuwa bibi au bwana.

Ugomvi huo unaweza kukua ukaenea na kuwakumba hata washangiliaji, wazomeaji au wanaojitolea kuamua.

Uzoefu unaonyesha mtu akianzisha ugomvi halafu akataka kumpiga yeyote anayemwona mbele yake awe mbaya wake au la, hata kama ana nguvu, mwisho wake huwa mbaya kwani wale anaowapiga bila sababu zozote wanaweza kuungana na kumshambulia.

Mara nyingi mabondia wa mitaani hupata ushujaa wa muda mfupi kabla ya kuadhiriwa na kuvuna aibu kuu au kifo.

Kinachofanyika sasa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) tangu watoke Dodoma kukamilisha walichoita kujivua gamba, ‘mabondia’ wao wapya chini ya kocha Wilson Mukama, wanapiga kila wanayemwona njiani—  mafisadi, madhehebu ya dini na vyombo vya habari.

Tangu Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM ilipowavua glovu (kufukuza) mabondia wakongwe chini ya Yusuf Makamba, mabondia wapya chini ya Wilson Mukama wameanza makeke.

Sekretarieti ya Makamba ilifananishwa na mabondia wakongwe wanaopigwa na mabondia vijana kutoka ndani ya klabu yao na klabu nyingine kama CHADEMA, NCCR-Mageuzi, CUF na TLP. Ushahidi ni mijadala ya bungeni.

Ufumbuzi waliopata, baada ya kupitia ripoti kadhaa ikiwemo ya Prof. Eginald Mihanjo, ni kuvua gamba kuukuu. Idara ya Itikadi na Uenezi ya CCM, ambayo ni ya propaganda akapewa Nape Nnauye na Idara ya Mambo ya Nje ikarejeshwa kiaina kwa Makamba; akapewa mtoto wake, January Makamba.

Nape hakupewa nafasi hiyo kwa bahati nasibu, bali ni kutokana na imani aliyonayo mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete kwake. Mwenyekiti amekuwa akimpa fursa ya kupumua kila aliposema jambo lililowakera waliojiona wamiliki wa klabu.

Kwanza ni alipokumbana na mkono wa mafisadi aliponyanyua kichwa chake kutaka kuwania uenyekiti wa Umoja wa Vijana (UV-CCM).

Kwa kuwa, aliingiza kwenye klabu mapambano kwa kuibua kashfa alipodai mkataba wa uwekezaji kwenye jengo la makao makuu ya jumuiya hiyo ni wa kifisadi, alivuliwa uanchama wa UV-CCM.

Baadaye alikata rufani akarudishiwa; akagombea nafasi ya ubunge katika Jimbo la Ubungo ndani ya CCM akaangushwa na Hawa Ng’umbi. Kikwete akampoza kwa kumteua kuwa mkuu wa wilaya ya Masasi.

Pili Kikwete ameamua kumpa kijana huyo rungu dhidi ya mafisadi. Huenda akaanzia alipotupiwa taulo ashuke na apotee kwenye ulingo wa siasa—kashfa ya mradi wa uwekezaji kwenye jengo la makao makuu ya CCM.

Katika kashfa ya mradi huo, Nape aliwatuhumu baadhi ya viongozi wa umoja huo na wadhamini kuwa walibariki mradi huo wa kifisadi kwenye viwanja vya jengo la makao makuu ya UV-CCM, jambo ambalo Makamba alisema ni utovu mkubwa wa nidhamu. Na hiyo ndiyo sababu Makamba amefunguliwa mlango wa kutoka, Nape akafunguliwa kuingia.

Katika madai yake, Nape alidai mwenyekiti wa baraza la udhamini wa UV-CCM, Edward Lowassa alibariki mradi huo alioutuhumu kuwa wa kifisadi na alimrushia konde aliyekuwa mwenyekiti wa umoja huo, Emmanuel Nchimbi kuwa pamoja na wenzake waliingia mkataba ambao haukuwa na maslahi kwa UV-CCM.

CCM wakatumia falsafa ya Waziri Mkuu Majivuno katika “Kusadikia” kwamba mchwa ukiotesha mabawa unataka kuangamia—Nape akaangamizwa.

Mbali na baraza kumvua uanachama, pia lilipendekeza kwa vikao vya juu vya CCM kuwa mwanasiasa huyo  avuliwe madaraka yake yote ndani ya chama, ambayo ni pamoja na ujumbe wa halmashauri kuu ya CCM. Hilo halikutekelezwa.

Hilo ndilo jinamizi linalomsumbua Nape kupambana na mafisadi anaojua walionufaika kwa mradi wa jengo la UV-CCM huku akisubiriwa na watu hao hao ambao wanatuhumiwa katika Richmond/ Dowans na vijisenti vya rada.

Halafu atakanyaga moto wa masalia ya mafisadi 11 ambao CHADEMA waliwataja Septemba 15, 2007. Humo wamo walioingiza nchi katika mikataba mibovu ya madini, IPTL, EPA, Meremeta, Deepgreen Finance.

Kibarua cha kuwatoa wote hao kutoka ndani ya CCM kinapaswa kukamilika kwa siku 90—kuanzia Aprili 12 hadi Julai 10.

Katika hali ya kushangaza na labda kwa vile idara yake ni ya propaganda, mwanasiasa huyo amepanua wigo wa mapambano. Amerusha ngumi kwa vyombo vya habari na madhehebu ya dini kwamba yanatumiwa na wabaya wao (mafisadi) eti kwa lengo la kumchafua mwenyekiti wake.

Fadhila

Labda kwa vile analipa fadhila za kubebwa na Kikwete, wanachama wote wa CCM wanajua mwenyekiti wao hakuanza kuchafuka leo. Kinachofanywa sasa na vyombo vya habari ni kuwajulisha wananchi kwamba baadhi ya matatizo yamesababishwa na Kikwete kabla na akiwa rais.

Hakuna kosa kwa vyombo vya habari kuwafahamisha wananchi kwamba Rais Kikwete yumo kwenye orodha ya mafisadi 11 iliyotangazwa na CHADEMA Septemba 15, 2007
Aidha, si kosa magazeti kuwaambia wananchi kuwa aliyetia saini kuruhusu IPTL kuingia nchini ni Kikwete alipokuwa waziri wa madini na nishati.

Vilevile, ni sahihi vyombo vya habari kueleza kwamba mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri lililoidhinisha Richmond/ Dowans ni Rais Kikwete.

Tena, vyombo vya habari vinatenda haki kuwajulisha wananchi kwamba vyombo vya upelelezi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) si lolote, vinapaka mafuta rushwa zinazohusu vigogo.

Ubaya uko wapi kuwajulisha wananchi kwamba Rais Kikwete anapata kigugumizi kuteua wakuu wa mikoa na wilaya kiasi kwamba wanaokaimu wanalia pembeni kuelemewa?

Nape aelewe kwamba mafisadi anaonyukana nao kwa miaka kadhaa wanamiliki vyombo vya habari. Kama CCM ilikuwa inafurahia vyombo hivyo vilipokuwa vinapangua hoja za ufisadi, anataka viandike nini leo -  viwatose wamiliki kwenye shimo la ufisadi au vimjibu Kikwete na CCM yake?

Wakati ule magazeti hayo ndiyo yalishupalia kwamba hakuna ushahidi dhidi ya tuhuma za ufisadi, leo kwa hoja zilezile yatamtaka Nape aweke wazi tuhuma hizo na ushahidi.

Madai mengine hayajaenda shule eti baadhi ya magazeti yanaisaidia CHADEMA! Ebo, kuna mahali imeandikwa magazeti yakisajiliwa yaisaidie CCM tu? Ipo siku Nape atahitaji msaada wa magazeti haya katika vita vyake na atakosa.Itakuwa busara akipunguza wigo wa vita hii.

0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: