Nape amgeukia Kikwete


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 13 July 2011

Printer-friendly version
NAPE Nnauye

NAPE Nnauye, katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) amemjia juu Rais Jakaya Jakaya Kikwete na kusema, “ni sehemu ya chimbuko la migawanyiko inayokikumba chama chake,” imeelezwa.

Amesema, “Pamoja na kwamba hatuwezi kumwajibisha mwenyekiti kwa sababu ni wajibu wetu kulinda hadhi yake, lakini naye hawezi kujinasua katika tuhuma za kuvurugika kwa chama chetu hadi kufanya vibaya katika uchaguzi mkuu uliopita.”

“Ni kweli ndani ya CCM hakuna umoja kwa sasa. Sehemu kubwa ya migawinyiko hii imesababishwa na Rais Jakaya Kikwete mwenyewe. Mtandao wake uliomuingiza madarakani ndio umekivuruga chama hiki. Sasa ili tukinusuru, sharti wote waliohusika na kukivuruga chama chetu waondoke.”

Nape alitoa matamshi hayo ya kwanza kusikika kwa kiongozi aliyepo ndani ya usukani wa uongozi wa chama, Jumatano iliyopita alipotembelea chumba cha habari cha kampuni ya New Habari Corporation inayochapisha magazeti ya Rai, Mtanzania, Bingwa, Dimba na The African.

Kampuni ya New Habari Corporation Limited, inamilikiwa na Rostam Aziz, mmoja wa watuhumiwa watatu wa ufisadi wanaotakiwa na CCM kuachia uongozi. Wengine ni Edward Lowassa na Andrew Chenge.

Katika ziara hiyo, Nape alikutana na mtendaji mkuu wa New Habari, Hussein Bashe na baadhi ya wahariri wa magazeti ya kampuni hiyo.

Mjadala wa mtandao kuvuruga chama, taarifa zinasema, uliibuliwa ndani ya mkutano na waandishi ambapo Nape alijitosa kuushambulia mtandao wa Kikwete akisema, “ndiyo chanzo cha CCM kufika hapa kilipo.”

Akimgeukia mwenyeji wake alisema, “Wewe Hessein (Hussein Bashe) unafahamu jinsi mtandao wenu ulivyokivuruga chama hiki. Ulikuwa mwanachama wa kundi hilo, unafahamu mlichokitenda. Kama kweli tunataka kukinusuru chama hiki, ni sharti wote waliohusika na mtandao, waachie ngazi.”

Hata hivyo, MwanaHALISI lilipowasiliana na Nape kufahamu undani wa alichokisema aling’aka, “Najua kuna watu wanataka kupika maneno ili kutekeleza mkakati wao wa kunichafua kutumia baadhi ya waandishi wa habari na vyombo vyao vya habari.” Nape hakutaja anaosema wana mkakati wa kumchafua.

Lakini amekiri suala hilo lilizungumzwa katika mkutano huo, bali alisema, “Suala hilo lilitokana na maoni ya mmoja wa waandishi wa magazeti hayo.” Alisema, “Sitaona tabu kuchukua hatua nikihisi nimelishwa maneno, maana tumerekodi kila kitu,” alieleza.

Hata hivyo, MwanaHALISI lina uhakika kwamba suala la mtandao lilijadiliwa kwa kina kati ya wahariri wa New Habari Corporation, Nape na Bashe.

Alisema, “Mimi nafahamu kila nilichozungumza. Siamini kama rais anahusika au ana mchango wowote katika hili…Kama ingekuwa hivyo basi tusingemsikia akikemea migawanyiko ndani ya chama.”

Alisema, “Ndiyo maana kwa kuhofia mkakati wa kunichafua, kila ninapopita narekodi mazungumzo yetu na wahusika. Nilipokuwa New Habari, tulizungumza kwa uwazi, lakini Bashe alipokuwa anazumgumza ya kwake, ndiyo akawaambia waandishi wake watoke, lakini mimi maofisa wangu walikuwapo”.

Mhariri mmoja mwandamizi wa magazeti hayo ameliambia gazeti hili, “Bashe na Nape wamezungumza mambo makubwa sana, ambayo kawaida yasingejadiliwa katika mkutano wa aina ile. Ni vema wangekutana faragha kuliko kueleza yale kwa kisingizio cha off record.”

Naye Bashe alipoulizwa juu ya suala hilo, haraka alihoji, “Hizo habari mmezipata wapi?”

Alipoelezwa zimetoka ndani ya chumba chake cha habari, kwanza Bashe alishusha pumzi na kisha akasema, “Tuacheni jamani. CCM ina matatizo mengi na tunakoelekea ni kugumu.”

Akiongea kwa njia ya kusisitiza, Bashe alisema, “Kaka, kaka, kaka, nakuomba niko chini ya miguu yako, tuna matatizo mengi yanatutosha. Tunapitia katika wakati mgumu. Mkiandika haya mtatuweka pabaya…”

Kwa mujibu wa mtoa habari wetu, Nape alisema ni mtandao wa Rais Kikwete uliofanikisha mkakati wake wa kuingia ikulu mwaka 2005 ambao umesababisha matatizo na kudhoofisha umoja ndani ya CCM.

Nape amenukuliwa akisema, “Chama hakina umoja. Kimeuawa na mtandao; bali pamoja na hayo, hatuwezi kumbebesha mzigo huu mwenyekiti peke yake; lakini naye ni sehemu ya tatizo lililopo ndani ya chama. Ili tuweze kuondoka hapa tulipo sharti yeye na wenzake, Lowassa, Rostam na wengine waachie ngazi.”

Hata hivyo, Nape alisema kwa kuwa Kikwete ndiye mwenyekiti wa chama na rais wa nchi, haiwezekani kumbebesha mzigo huo. Akatoa mfano wa John Malecela alipojiuzulu kwa kubariki kuwapo kwa serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano, akisema “Huwezi kusema yale yalifanyika bila baraka za Mzee Mwinyi (rais mstaafu Ali Hassani Mwinyi).”

Mtoa taarifa anasema wakati Nape alikuwa akimtaja Rais Kikwete kama sehemu ya mgawanyiko ndani ya chama, Bashe yeye alikuwa akituhumu viongozi wapya wa sekretarieti ya CCM walioteuliwa katika mabadiliko ya Aprili mwaka huu, kwa kusema wanakipeleka chama hicho mahali siko kutokana na kusimamia kaulimbiu ya “kujivua gamba.”

Imeelezwa kuwa Bashe alithibitisha katika mjadala huo kuwa ni kada aliyepo kundi la kina Lowassa, Chenge na Rostam.

Awali Nape alimtuhumu Bashe kwamba amekuwa akitetea watuhumiwa hao watatu ambao chama kilishaelekeza wajivue uongozi wa chama ili kukirejesha katika umoja wake.

Lakini Bashe akijibu hoja ya Nape, pamoja na kukiri kutetea wanaoitwa na CCM kuwa “mafisadi,” alipinga wazo la kuwafukuza watuhumiwa hao kwa madai kwamba matatizo ya CCM hayawezi kumalizwa kwa njia hiyo.

Alisema, “Nape, mnachokifanya ni unafiki na hakiwezi kumaliza matatizo yetu. Tutaendelea kutafunwa na makundi hadi tumalizike.”

Kufika hapo, ndipo Nape akasema, “…Wote wana makosa na kama tunataka kuokoa hiki chama, hatuwezi kurudi nyuma. Ni lazima waondoke.”

Kuhusu hilo, Bashe ameripotiwa kusema, anachokifanya Nape ni kutaka kuingiza mgombea wake ikulu mwaka 2015. Naye alijibu kuwa ana msimamo, hayumbi kwa analolisimamia.

Mwaka 2005 Nape anatajwa kuunga mkono Profesa Mark Mwandosya katika uteuzi wa ndani ya chama.

Nape hakuishia hapo. Aligusia hata mwenendo wa uchaguzi ndani ya Umoja wa Vijana (UV-CCM), kwamba alimuunga mkono Bashe ambaye aliamini kuwa ni mtu huru, lakini alipobadilika alimpinga katika harakati zake za kuwania ubunge jimbo la Nzega.

Alisema “Mimi sifichi ninachokisimamia. Inawezekana maamuzi tulikosea, lakini sharti twende mbele. Katika uteuzi wa ubunge jimboni Nzega, nilikupinga. Nilimuunga mkono Lucas Selelii.

Akiongea kwa sauti ya upole, Bashe alisema, “Tunakuwa wanafiki. Kila mtu amebeba briefcase (mkoba) yake yenye wagombea.”

Bashe aliendelea kusema kuwa kuwatuhumu Lowassa, Rostam na Chenge ni kuwaonea kwa kuwa karibu viongozi wote wa CCM ni wachafu.

Vyanzo vya taarifa vinasema Bashe alimwambia Nape, hoja ya ufisadi si agenda ya CCM. Ni agenda ya upinzani, hususani Chadema. “Siku zote tumekuwa tukitetea kwamba ndani ya chama chetu hakuna ufisadi. Sasa tumetangaza tunao mafisadi. Tukimaliza hili, wananchi watatuuliza, je, ‘mafisadi’ ni hawa watatu tu?,” aliuliza.

Akitetea watuhumiwa hao watatu, Bashe alisema, “Hatujadili mambo ya msingi, kwanini? (Hii) ni hoja ya Chadema.”

Bashe alinukuliwa akizidi kujenga hoja yake kwa kumuuliza Nape kama katika tuhuma za rushwa ya rada, mtuhumiwa ni Chenge peke yake.

Bashe alikaririwa akilaumu namna serikali inavyoshindwa kutazama hali za wananchi masikini kufuatia kitendo chake cha kuachia ushuru wa kiwango cha juu wa petroli uwiane na ule wa mafuta ya taa, nishati inayotegemewa na sehemu kubwa ya wananchi masikini.

Akionyesha athari za matatizo ya msingi yanayokabili uongozi wa juu wa CCM na kuathiri utendaji wa serikali, Bashe alisema, “Tumepandisha bei ya mafuta ya taa kwa sababu ya kudhibiti petroli. Mnakiri udhaifu wa serikali kuumiza wananchi?”

“Turudi chini. Kutoka asilimia 80 tumepata asilimia 61 kwa sababu ya makosa, vidonda vya kura za maoni na wagombea wasiofaa. Haya ndiyo matokeo ya makosa yetu katika chama,” alinukuliwa Bashe akilalamika kama kuonea huruma chama.

0
Your rating: None Average: 4.5 (2 votes)
Soma zaidi kuhusu: