Nape: Kondoo wa kafara


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 09 September 2008

Printer-friendly version
Nape Nnauye

HALMASHAURI Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), inakutana mjini Dodoma. Huu ni mkutano wa pili wa kawaida tangu chama kilipomaliza kikao cha NEC kilichofanyika kijijini Mwitongo, Butiama mkoani Mara, Aprili mwaka huu.

Katika mkutano wa Mwitongo, hoja kubwa iliyotawala kikao ilihusu “chama kukumbatia mafisadi.” Hoja ya kukumbatia mafisadi ilitolewa kikaoni na wanasiasa shupavu, Cleopa Msuya na Makongoro Nyerere.

Msuya na Makongoro hawakutafuna maneno, bali walitaka “watuhumiwa wa ufisadi waondolewe” katika chama.

Wakiongea kwa uchungu, Msuya na Makongoro walisema ni vema chama chao kikawaweka pembeni watuhumiwa wa ufisadi ili kulinda hadhi yake mbele ya jamii. Hawakusikilizwa!

NEC ni chombo muhimu. Hiki ndicho chombo kinachotunga sera; kinachosimamia utekelezaji; na ndicho kinachowajibika kwa mkutano mkuu wa chama.

Ni kutokana na umuhimu huo, wananchi watataka kujua chombo hiki kinachokutana kitafanya nini? Kitaagiza nini na kitaamua kipi?

Hata hivyo, kikao cha NEC kinafanyika huku Baraza Kuu la Umoja wa Vijana (UV-CCM) likiwa tayari limetangaza kumvua uanachama wa umoja huo, mjumbe wake Nape Nnauye.

Baraza hilo linamtuhumu Nape kwa kile lilichosema “kuongea mambo ya chama nje ya vikao vya chama.”

Nape alipatwa na zahama hiyo Jumapili iliyopita, baada ya Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, mwanasiasa mkongwe Kingunge Ngombale-Mwiru na Mwenyekiti wa UV-CCM, Emmanuel Nchimbi “kufunga ndoa” ya kumsulubu Nape.

Kosa la Nape analoadhibiwa kwalo ni kutetea mali ya chama chake. Katika mazungumzo yake na waandishi wa habari siku alipotangaza kugombea uenyekiti wa umoja huo, Nape alituhumu Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la UV-CCM, Edward Lowassa kwa kuingiza jumuiya yao katika mkataba wa kinyonyaji.

UV-CCM imeingia ubia na makampuni mawili ya M.M. Integrated Steel Mills (MMISML) na Estim Construction Company Limited (ECCL) kwa ajili ya ujenzi wa kitegauchumi cha jumuiya hiyo.

Lowassa anatuhumiwa kutoshirikisha Baraza la Wadhamini katika mkataba huo. Tayari wajumbe wote wa Baraza wamekana Lowassa.

Katika hali ya kawaida, chama hicho kilipaswa kumshukuru Nape kutokana na hatua yake ya kukemea ufisadi hadharani.

Hoja ya Makamba kwamba Nape alipaswa kuzungumzia utata wa mkataba ndani ya vikao vya chama chake, wala haina mashiko.

Je, Makamba anataka Nape aende katika kikao gani ili aleze hayo, wakati kila mmoja anajua kwamba wenye mkataba hawakuwa wanafuata vikao?

Je, Makamba anataka kusema hapa kwamba hafahamu kuwa Lowassa alikuwa waziri mkuu na amepata kushika madaraka mbalimbali ndani ya serikali, na hivyo anajua taratibu zote za kuendesha mambo ya umma?

Kinachoonekana hapa, ni kwamba Makamba anataka kuziba masiko na kujifanya kiziwi. Anajifanya hajui kuwa mkataba ambao Nape anaupinga, haukufuata vikao vinavyotakiwa.

Makamba nataka kujifanya hajui kuwa Lowassa alisaini mkataba huo bila kushirikisha wenzake, jambo ambalo Nape analipigia kelele.

Wala kuzungumza nje ya vikao si jambo geni kwa CCM. Kuna msululu wa wanasiasa ambao kwa miaka nenda rudi wamekuwa wakiongea na vyombo vya habari au katika mikutano ya nje ya chama, lakini hawajachukuliwa hatua. 

Mfano hai, ni mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete. Mwaka 1995 wakati wa mchakato wa kutafuta mgombea urais, Kikwete aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kumtuhumu Katibu Mkuu wa chama hicho, Laurance Gama, kwamba alikuwa anamhujumu.

Kikwete alimtuhumu Gama kwamba anapendelea baadhi ya wagombea na kumtenga yeye. Hakuchukuliwa hatua yoyote ya kinidhamu.

Orodha ni ndefu: Kuna Naibu Waziri Kiongozi wa Serikakali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Ali Juma Shamhuna, ambaye amenukuliwa akikaripia Waziri Mkuu Mizengo Pinda katika kile alichoita, “kutetea Zanzibar.” Hakuadhibiwa wala hakujadiliwa.

Kuna Kingunge Ngombale-Mwiru. Huyu alituhumu wenzake katika chama nje ya vikao. Akihutubia mkutano wa hadhara baada ya kupokea maandamano ya wana-CCM wa mkoa wa Dodoma, Kingunge alituhumu Anne Kilango Malecela na Aloyce Kimaro.

Ngombale alisema Kimaro na Kilango wanakipasua chama chao kutokana na  michango yao bungeni. Hakufuatwa wala kuulizwa.

Kuna Salum Msabaha Mbarouk na Tambwe Richard Hizza. Hawa kwa pamoja walimshambulia mwanasiasa mkongwe na Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba kwamba hana mamlaka ya kuzungumzia mambo ya CCM.

Lakini yupo pia Rostam Aziz ambaye vituko vyake vya kukimbilia kanisani na kushambulia wenzake bado vinakumbukwa. Alipoona hiyo haijatosha aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kumaliza dukuduku lake. Huko alishambulia watu mbalimbali, kuanzia viongozi wa vyama vya siasa hadi wafanyabiashara.

Hata Makamba ni mateka wa hali hii. Siku moja baada ya Nape kuongea na waandishi wa habari, Makamba alimwita Nape ofisini kwake, tena mbele ya waandishi wa habari na kumsuta na kusuta vijana waliokuwa wameonyesha kuungana na Nape.

Makamba alimwambia Nape, mbele ya kadamnasi, kuwa vijana wenzake watamruka. “Watakuruka hawa; ni njaa tupu hawa,” alisema Makamba mbele ya msaidizi wake Said Mtanda ambaye ni mjumbe wa Baraza Kuu la Vijana na Mwenyekiti wa UV-CCM Bagamoyo.

Kutokana na hali hiyo, msingi wa madai ya Nchimbi na wenzake katika hili la Nape hauonekani popote katika hali ya kawaida, labda kama wengi wanavyoona kuwa “kuna ugomvi binafsi.”

Kinachotia mashaka zaidi sasa, ni hatua ya Nchimbi kushindwa kuwauliza wenyeviti wa mikoa sita ambao awali walinukuliwa na gazeti la MWANANCHI wakisema  hawajawahi kupitisha mkataba huo. Hawa walisema wazi kwamba hawaujui mkataba kati ya UV-CCM na wawekezaji na kwamba hawajaubariki.

Walicholishwa hadi kuamua kunyamaza ni wao na viongozi wao wanaojua. Lakini lililodhahiri ni kwamba katika kikao cha Baraza Kuu, wao hawakuulizwa.

Hao ni pamoja na Kyondo Mwenyekiti wa UV-CCM mkoani Tanga, Daniel Porokwa (Arusha), Marwa Matayo (Mara), Mohammed Karia (Kilimanjaro) na Edgar Mkosamali (Kigoma).

Kama kosa la Nape lilikuwa kuzungumza na vyombo vya habari, basi hata viongozi hawa wa mikoa nao walifanya hivyo. Sasa mbona hawa hawakujadiliwa? Mbona hawakuhukumiwa? Mbona hawakuulizwa? Mbona hawakunyang’anywa uanachama?

Sasa kwa nini watu makini wasihusishe hatua hizo na kinyang’anyiro cha uchaguzi na hatua ya CCM kukumbatia ufisadi?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: