Nape Nnauye amebeba ‘gunia la kokoto’


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 18 May 2011

Printer-friendly version
Gumzo la Wiki
Nape Nnauye

KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye sasa amebeba “gunia la kokoto” na hajui mahali pa kulitua.

Hadi sasa Nape amejiingiza katika mgongano wa ndani kwa ndani katika chama chake; amepanua wigo wa maadui kwa kuandama anaowaita “watuhumiwa wakuu wa ufisadi;” na anabembea katika malumbano na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Tangu kukabidhiwa wadhifa wa ukatibu mwenezi wa CCM, Nape amekuwa akisisitiza, “…kung’oa mafisadi ndani ya CCM, ni jambo ambalo halina tena mjadala.”

Amesema, “Kinachosubiriwa sasa ni suala la utekelezaji tu; NEC imetoa siku 90 kwa mafisadi kuondoka” katika chama hicho.

Katika hili, Nape alijiapiza kuwa barua za kujulisha mafisadi kuondoka katika chama tayari zimeandaliwa na zitatolewa kabla ya kumalizika Sikukuu ya Pasaka. Hazijatoka.

Viongozi ambao wametajwa na Nape kuwa wanatakiwa kujiondoa kwenye uongozi au chama ndani ya siku 90 kwa kuwa ni “mafisadi wanaochafua sura ya chama mbele ya jamii,” ni Edward Lowassa, Rostam Aziz na Andrew Chenge.

Wote watatu ni wajumbe wa NEC na wabunge wa Bunge la Muungano.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama aliwaambia waandishi wa habari wiki mbili zilizopita jijini Dar es Salaam, “…hakuna mahali popote katika maazimio ya NEC panapotaja siku 90.”

Alisema, “Kama ni muda basi ni pale mwenyekiti wetu aliposema NEC ijayo. NEC hukutana kila baada ya miezi minne na kwa hiyo kama ni siku, basi ni 120 na siyo 90.”

Hatua ya Nape ya kutamka kuwapo kwa barua za kufukuza mafisadi ndani ya chama chake au azimio la NEC, lilikuwa kosa la kwanza kisiasa.

Hata kama Nape alikuwa ametumwa na mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete kusema aliyosema, bado alipaswa kuwa makini na mzigo aliobebeshwa.

Kwa wanaomfahamu Kikwete tangu alipokuwa Tanga Sekondari, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) hadi ikulu, wanajua jinsi alivyo bingwa wa kutumia wenzake na kisha kuwaacha njiani pale maslahi yake yanapoguswa.

Hili linathibitishwa na hatua yake ya kuridhia kujiuzulu kwa Edward Lowassa katika wadhifa wake wa waziri mkuu.

Lowassa ambaye mwaka 1995 aliandamana na Kikwete kuchukua fomu ya kuwania urais na kufanikisha harakati zake za kuingia ikulu katika uchaguzi wa mwaka 2005, alitoswa huku akiona.

Kisa: Kikwete alihofia kile kilichoitwa na aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge, Dk. Harrison Mwakyembe “hatukusema yote, ili kuokoa serikali na rais.”

Taarifa zinasema, Kikwete aliamua kuepusha malumbano ambayo yangeweza kumhusisha na ujio wa makampuni tata ya Richmond na Dowans.

Si hivyo tu. Kikwete ameridhia kuondoka katika nafasi yake ya uspika, Samwel Sitta ambaye tangu mwaka 1995 walikuwa wote katika kutafuta urais.

Ni Sitta aliyemjengea Kikwete msingi wa mbio za urais tokea mwaka 1995 alipokubali kumpeleka kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kupata baraka za kugombea urais.

Katika uchaguzi wa mwaka 2005, Sitta alikuwa makamu mwenyekiti wa kundi la mtandao uliomuingiza Kikwete madarakani.

Lakini bila sababu za msingi zenye kuathiri maslahi ya taifa, Kikwete aliamua kuweka sharti la kutaka spika mwanamke; sharti ambalo lilimuondoa Sitta katika kinyang’anyiro hicho.

Wengine ambao walitumiwa na Kikwete na wakaachwa njiani kwa sababu hizohizo au zinazofanana, ni pamoja na Bernard Membe, Amos Makalla na Zakia Meghji.

Makala ndiye alikuwa katibu wa mtandao wa Kikwete, huku Meghji akitajwa kuwa ni miongoni mwa watu waliofanikisha, kwa kiasi kikubwa, kampeni za urais wa Kikwete.

Wakati Membe alitumika “kufanikisha mkakati” wa kuwafukuza Rostam, Lowassa na Chenge katika vikao vya maamuzi, Kikwete katika staili yake ya kuuma na kupuliza, aliamua kutopeleka jina lake katika kinyang’anyiro cha uchaguzi wa wajumbe wa Kamati Kuu (CC) na sekretarieti ya chama.

Hata kuondoka kwa Yusuf Makamba na kuingizwa kwa January Makamba, mtoto wake, kumefanywa kwa njia hiyohiyo.

Hivyo basi, hatua ya Nape ya kujiingiza katika mgongano wa ndani kwa ndani na wenzake ; na kung’ang’ania hoja ya kufukuza wanaoitwa “mafisadi ndani ya chama,” inaweza kumgharimu.

Kikwete anaweza kuamua kumuacha Nape solemba kwa kuwa kibarua alichompa kimemshinda; hawezi kutetea alichoagizwa; hafahamu anachotakiwa kufanya na hajui anachotenda.

Kwanza, badala ya kujibu hoza zilizosheni takwimu na uhalisia wa maisha ya kila siku ya wananchi zinazotolewa na CHADEMA, kwa mfano “serikali kufilisika,” yeye amejiingiza katika hoja dhaifu ya posho za watendaji wa chama hicho akiwamo katibu mkuu Dk. Willibrod Slaa.

Anasema Dk. Slaa analipwa mshahara wa Sh. 7.5 milioni kila mwezi. Anadai kitendo hicho ni sawa na ufisadi. Anamtuhumu kuwa huko nyuma aliwahi kunukuliwa akisema mishahara ya wabunge ipunguzwe kwa kuwa inaangamiza taifa.

Nape haishii hapo. Amezungumzia pia kile anachoita “ununuzi wa magari chakavu” yaliyonunuliwa kutoka kwa mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.

Hatua ya Nape kunyooshea kidole CHADEMA, haiwezi kukisaidia chama chake katika mkwamo wa tuhuma dhidi ya ufisadi, badala yake imekizamisha chama chake katika tope.

Kwa mfano, wakati Nape anasema mshahara wa katibu mkuu wa CCM, ni Sh. 1.5 milioni, ukweli ni kuwa kima cha mshahara kwa watendaji wakuu wa chama hicho, kinategemea mhusika ametokea wapi kabla ya kupewa kazi hiyo.

Yusuph Makamba, katibu mkuu aliyeondoka madarakani, alikuwa anatakiwa kulipwa Sh. 1.5 milioni. Huu ni mshahara ambao alikuwa anapata wakati akiwa mkuu wa mkoa.

Lakini Makamba aliamua kuachana na mshahara huo kwa kuwa yeye tayari alikuwa mbunge. Alibaki na mshara wake mmoja wa ubunge ambao ni zaidi ya Sh. 7.1 milioni anazolipwa Dk. Slaa.

Aidha, katibu mkuu wa CCM anamiliki magari matatu – la kwake, linalotumiwa na wasaidi wake katika msafara wake na lile linalotumiwa na mkewe. Magari yote haya matatu huhudumiwa na CCM.

Mbali na Makamba kupewa magari matatu, alikuwa analipwa posho ya Sh. 135,000 (laki moja na elfu thelathini na tano) kwa kila siku ambayo anakuwa nje ya Dodoma. Hapa Makamba atakuwa amejichukulia kitita cha zaidi ya Sh. 11.5 milioni kwa mwezi.

Kwa kuwa Makamba alikuwa mbunge, aliendelea kunufaika na stahiki zote za mbunge. Alilipwa mafuta – Sh. 2.5 milioni kila mwezi. Alilipwa posho ya dereva – Sh. 400,000 kila mwezi, huku chama chake kikigharamia dereva, mafuta na baadhi ya safari zake zikiwamo zile za nje ya nchi.

Hata safari yake ya matibabu nchini India, pamoja na safari za kikazi mkoani Dodoma, zote hizo ziligharamiwa na Bunge na chama chake.

Ndivyo ilivyokuwa pia kwa Jaka Mwambi aliyekuwa naibu katibu mkuu wa chama hicho. Mwambi alilipwa Sh. 1.5 milioni kwa mwezi kwa kuwa kabla ya kushika wadhifa huo alikuwa mkuu wa mkoa wa Rukwa.

Baada ya muhula wake wa ubunge kumalizika, ndipo Makamba akaanza kulipwa fedha hizo, lakini alijilipa mamilioni mengine ya shilingi kama posho ya kujikimu.

Katibu mkuu mpya, Wilson Mukama, kwa kuwa ameacha utumishi akiwa katibu mkuu serikalini, atachota kitita cha Sh. 3.8 milioni; posho ya Sh. 135,000 kwa kila siku asiyokuwapo Dodoma na atakuwa na wasaidizi sita wanaolipwa posho ya kati ya Sh. 30,000 na 55,000 kwa siku.

Mukama amekabidhiwa magari matatu yanayohudimiwa na chama chake – mawili yake na moja la mkewe – na atakuwa anaendelea kulipwa stahiki yake ya kiinua mgongo kama katibu mkuu mstaafu.

Je, Nape alikuwa anafahamu haya kabla ya kuamua kuangamiza chama chake? Anajua kuwa maelezo haya yametosha kuwapa mtaji wa kisiasa wapinzani wake?

Kimsingi kabla ya Nape kuzungumza alichokusudia, alipaswa kupima maelezo yake. Alipaswa kuangalia athari zitakazokipata chama chake.

Matokeo yake, sasa analazimika kufanya kazi tatu kwa mpigo – kuokoa chama chake, kujiokoa yeye mwenyewe na kuendelea na kibarua cha Kikwete kwa kuhubiri “mwisho wa mafisadi” usiowadia.

Badala ya kusisitiza umuhimu wa chama chake kuachana na mafisadi, analazimika sasa kujibu madai yaliyoporomoshwa na CHADEMA na kuthibitishwa na Fred Mpendazoe juu ya ushiriki wake katika kuunda, kusajili na kutumikia Chama cha Jamii (CCJ).

Badala ya kutumia muda na akili yake kueleza wanachama na viongozi wenzake jinsi chama hicho kilivyodhoofika kisiasa kwa kukumbatia ufisadi na mafisadi, sasa anapaswa kujibu hoja juu ya jinsi alivyonufaika na fedha za wizi wa EPA kupitia kwa mmoja wa watuhumiwa, Jeetu Petel.

Badala ya kujenga chama chake, Nape anapaswa kujielekeza sasa katika tuhuma juu ya usaliti kwa chama chake; na hatua yake ya kutaka kugombea ubunge katika jimbo la Ubungo, kupitia CHADEMA.

Atachoka au tuseme tayari amechoka asubuhi. Amejitwisha vineno asivyoweza kutetea na amekitumbukiza chama chake katika mbio ambazo hawezi kushinda.

Huyo ndiye Nape Nnauye. Kijana anayedhani anaweza kuokoa CCM kwa kuvurumisha madai dhidi ya upinzani.

Waswahili husema aendaye mbio za Nape, amebeba gunia la kokoto. Je, Nape anapeleka wapi gunia hilo? Atamuuzia nani?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: