Natamani fainali za CCM 2010


Yusuf Aboud's picture

Na Yusuf Aboud - Imechapwa 22 September 2009

Printer-friendly version

NATAMANI mwaka 2010 ufike haraka ili nione mshindi kati ya makundi mawili “hasimu” ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Ni kundi la wanaoitwa wapambanaji katika “vita vya kutokomeza ufisadi,” dhidi ya lile linalotuhumiwa “ufisadi” na ambalo linahaha kuzima kelele za wapambanaji.

Haya ni mapambano ya aina yake yanayopasa kushuhudiwa. Pengine yanaweza kuwa mapambano ya kihistoria katika nchi yetu. Ndiyo, ni historia katika nchi hii kuona mapambano ndani ya chama kimoja, tena kile kilichoko ikulu.

Ni hivi: Makada wa CCM, wametofautiana, tena kwa kulumbana ndani kwa ndani na hatimaye kelele zimepenya mpaka nje na sasa wanapambana hadharani.

Hapa ndipo “uongo” wa CCM na serikali yake utakapojidhihirisha. Majukwaani wanatangaza kukemea rushwa na kusema wanapinga ufisadi. Kwenye vikao vyao vya ndani wanawaandama wapinga ufisadi na kufikia hatua ya kutaka kuwafukuza kwenye chama chao.

Fainali za mapambano haya ni Mei 2010 wakati CCM itakapokamilisha mchakato wake wa kuwapata wagombea ubunge katika majimbo nchini. Hapa tutaona kama jitihada za mafisadi na wapambe wao kuwaangamiza wapambanaji, zitakuwa zimefanikiwa au kugonga mwamba.

Mafisadi wanafanya juhudi za kuwango’a wapambanaji madarakani ili kuzima kelele. Wapambanaji nao hawalali kuhakikisha wanashinda vita hivi. Vita vinaonekana kuwa vya watu wachache lakini vyenye hisia na manufaa kwa wengi.

Kugonga mwamba kwa jitihadi za mafisadi kutakuwa na maana ya ushindi kwa kundi la wapinga ufisadi. Ushindi huu hautakuwa wa wapinga ufisadi pekee. Utakuwa ushindi wa wananchi wote - wale wanaopinga ufisadi na hata wale wanaowaunga mkono mafisadi.

Kwani kuwashinda wala rushwa, wakwapua mali za taifa, wanaovuna rasilimali za taifa peke yao na kwa pupa, wanaodidimiza uchumi wa taifa kwa manufaa yao binafsi; ni ushindi wa wananchi wote wapenda maendeleo.

Ni ushindi mkubwa ambao kila Mtanzania anauhitaji hata kama hajui faida zake wakati huu. Ni ushindi wa kizazi cha sasa na kijacho na kingine.

Lakini iwapo mafisadi watafanikiwa katika jitihada zao za kuwanyamazisha na kuwang’oa wapambanaji, maana yake mafisadi watakuwa wamewashinda wananchi wote.

Ushindi wa mafisadi ni pigo kubwa kwa wananchi. Ni pigo kwa kizazi cha sasa na kijacho, maana athari za ufisadi unaofanywa leo zitaendelea kukiathiri hata kizazi kijacho.

Uwezekano wa mafisadi kushinda ni mkubwa zaidi kuliko kushindwa. Hii inatokana na baadhi ya viongozi wa ngazi za juu wa CCM kuwakingia kifua wasiguswe au kusemwa.

Somo linalopatikana kwa wananchi hapa ni CCM kukumbatia ufisadi na mafisadi. Wananchi wanajiuliza: Ziwapi hatua walizochukuliwa wahusika wa ufisadi wa Richmond wakati Bunge lilijiridhisha kwamba kulikuwa na taratibu zilizokiukwa katika kuipatia mkataba kampuni hiyo?

Ukimya wa serikali unataka ijengeke hoja kwamba sakata la kampuni hiyo, ya kufua umeme wa dharula, lilikuwa njama tu za kumwondoa Edward Lowassa katika kiti chake cha waziri mkuu. Hii ni makusudi.

Kama si kweli, mbona hakuna hatua nyingine zilizochukuliwa kwa wahusika wengine, waliobainika katika kashfa hiyo?

Na kwa serikali kutochukua hatua dhidi ya wahusika wa ufisadi, ndiyo sababu ya kuongeza uhondo katika mapambano ya makundi mawili ndani ya CCM – kundi la mafisadi na wapinga ufisadi.

Tunasubiri tuone mshindi. Lakini kama nilivyotangulia kusema, ushindi wa mafisadi ni kiama cha wananchi. Na kushindwa kwa mafisadi ni ushindi kwa wananchi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: